Kadiri giza linavyokuwa totoro, maana yake asubuhi imekaribia. Ndivyo unavyoweza kuelezea uamuzi wa aliyekuwa Katibu Mkuu wa chama cha ADC, Doyo Hassan Doyo kuhamia chama cha National League for Democracy (NLD) na kuteuliwa kuwa Katibu Mkuu.
Doyo alitimkia NLD na kupitishwa kuwa Katibu Mkuu wa chama hicho, zikiwa zimepita siku 69 tangu aliposhindwa kwenye nafasi ya mwenyekiti wa ADC Taifa katika uchaguzi uliofanyika Juni 29, 2024.
Katika uchaguzi huo, Doyo alishindwa kwa tofauti ya kura 51 na Shaban Itutu, aliyepata kura 121 katika kinyang’anyiro cha uenyekiti wa ADC, na Jumamosi ya Septemba 7, 2024, aliteuliwa kuwa Katibu Mkuu wa NLD.
Mwenyekiti wa NLD Taifa, Mfaume Hamis Hassan alisema yeye ndiye aliyempendekeza Doyo kujiunga na chama hicho na Septemba 7, 2024 wakati wa uchaguzi wa Taifa wa chama, Halmashauri Kuu ilimuidhinisha kuwa Katibu Mkuu wao.
Kabla ya kukihama chama chake cha zamani, Doyo alifungua shauri Mahakama Kuu akipinga uchaguzi huo, akidai kwamba kulikuwa na ukiukwaji wa katiba na kanuni za chama hicho kwa lengo la kumkosesha ushindi.
Doyo alieleza kutoridhishwa na matokeo yaliyotangazwa na kamati ya uchaguzi, lakini hata alipokata rufaa kwa kamati hiyo, hakuridhika na uamuzi uliotolewa, ndipo alipokwenda kufungua kesi mahakamani kusaka haki.
Mwananchi limefanya mahojiano maalumu na Doyo ofisini kwake, Temeke, Dar es Salaam ambapo amezungumzia mambo mbalimbali, ikiwemo hatima ya kesi ya kupinga uchaguzi huo aliyofungua Mahakama Kuu.
Doyo anasema amefanya tafakuri na tathimini ya kutosha kwa kushauriana na wanasheria wake sita na kufikia uamuzi wa kwenda kuifuta kesi hiyo, kwa kuwa haoni haja tena, kwani tayari amekihama chama hicho na sasa anajielekeza katika kukijenga NLD.
“Shauri nilifungua Mahakama Kuu na ilitakiwa lianze kusikilizwa kuanzia Septemba 25, 2024. Nimeshauriana na wanasheria wangu, wataandika barua kwenda kwa wadai wangu, kwa sababu sitarajii kuendelea nalo tena.
“Sitaendelea na kesi, si kwa sababu nimehamia chama kingine, hapana, lakini nawapisha wafanye maandalizi ya uchaguzi wa serikali za mitaa. Nimetathimini kwa busara itakuwa si vizuri, naweza kuwavuruga zaidi,” anasema Doyo.
Katika maelezo yake, anasema anaona suala hilo litampotezea muda wake, huku akieleza kuwa anakabiliwa na majukumu mengi ndani ya chama kipya, ikiwemo kuandaa ziara na kuingiza wanachama wapya.
“Natakiwa kutengeneza malengo ya chama kujipanga na uchaguzi wa serikali za mitaa na uchaguzi mkuu na muda wangu ni mfupi. Hizo ni sababu kubwa zilizonifanya nikaliondoe lile shauri,” anasema.
Doyo anafafanua msingi wake wa kupeleka shauri hilo mahakamani ilikuwa si kuhitaji madaraka kama wengi walivyokuwa wanadhani, lakini alikuwa anataka haki itendeke na kuhakikisha suala hilo lisijitokeze tena.
Doyo anasema anawapuuza baadhi ya wakosoaji wanaochukulia uamuzi alioufanya wa kuhama kwake kutoka ADC kwenda NLD kuwa ni uchu wa madaraka na siyo kusukumwa na misingi ya itikadi.
“Inawezekana wako sawa kwa sababu wanatoa maoni yao, lakini hakuna mwanasiasa anayepambania ndoto zake halafu akakubali zizuiliwe na wajinga. Ni maneno tu, hayamzuii tembo kunywa maji.
“Nimekuwa mwanasiasa kwa muda mrefu, najua propaganda za kisiasa nchini. Mapambano yaliyonifanya niwe mpinzani tangu zamani ni makali, hayo hayo yananifanya nifike hapa,” anasema Doyo.
Katika maelezo yake, Doyo anatolea mfano sakata lake na ADC lilifikishwa hadi Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa kwa chama chake hicho cha zamani kuandika barua asifanye shughuli za kisiasa hadi apewe maelekezo na viongozi waliopo madarakani.
“Uamuzi wa kuandika barua hiyo ulikuwa nje ya katiba ya chama, kwani kinaeleza kila mwanachama ana haki na wajibu wa kukijenga chama kwa kadiri awezavyo katika eneo analoishi,” anasema.
Anahoji kwamba inakuwaje anahama watu wanadai anapenda madaraka wakati walimzuia asijihusishe na siasa, huku wakijua shughuli hizo anazipenda na zinamfanya aendeshe maisha yake.
Doyo anasema kuna tofauti kubwa kati ya chama chake cha zamani na kipya, huku akitolea mfano itikadi ya NLD ambayo imejikita katika misingi mitatu, ikiwemo haki.
“Inasimama katika uzalendo na maendeleo, hivi vitu vitatu ADC havipo. Uzalendo unalenga kuipigania nchi katika masuala yanayohusu mikakati ya kupiga hatua kiuchumi na kijamii na kupinga ufisadi,” anasema.
Anasema anaona chama alichopo kwa sasa ni sehemu ya msingi na salama zaidi kuliko alikotoka, huku akitoa rai ya kuwashawishi Watanzania kumfuata huko.
“Nilipokuwa ADC kama mtendaji nilifanya mageuzi makubwa, lakini kuna baadhi ya mambo nilikuwa nashindwa kushawishi kwa kuwa nilikuwa mtu wa kupokea na kutekeleza,” anasema mwanasiasa huyo.
Doyo anasema katiba ya chama chake cha zamani, majukumu ya Katibu Mkuu ni kupokea maelekezo kutoka kwenye mkutano mkuu wa chama, kamati na mwenyekiti wa chama na kutekeleza.
“Unakuwa na ngazi tano zinazotoa maelekezo na kutakiwa kuyatekeleza, nilikuwa nakosa muda wa kutoa fikra zangu kutokana na mkwamo wa kiutawala wa kushindwa kupenyeza mambo mzuri,” anasema Doyo.
Anasema baada ya kuona kuna ufinyu wa kuwasilisha mipango mizuri pamoja na kubadilisha katiba mara mbili, alimua kuchukua fomu ili akagombee nafasi ya uenyekiti, nako anasema alipigwa chini.
Doyo anasema malengo yake ndani ya chama chake kipya cha NLD ni kukiona kinakuwa chama kikubwa cha upinzani nchini na kinachovutia, huku akieleza kutumia uzoefu wake alioupata akiwa ADC na Chama cha Wananchi (CUF).
“Nakuahidi, mipango yangu ndani ya NLD ni kuwa chama kikubwa cha ushindani katika vyama vya siasa nchini na tutaanzia kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa kwa kuwa tumeanza kufanya ziara za kichama Zanzibar kujipanga,” anasema.
Anasema mipango yake mingine ni kufanya maboresho ndani ya chama hicho kwa kutafuta chanzo cha kudumu cha mapato cha kisheria kwa kuhakikisha wanachama wanatoa michango na ada kwa mujibu wa katiba.
“Michango na ada ni tatizo nililolikuta hapa NLD, halijatiliwa mkazo, ambalo ni chanzo kikubwa cha mapato kwa chama. Hili nimeliona na nitahakikisha wanachama wanatekeleza ili tupate fedha kujiendesha,” anasema.
Doyo anasema jukumu lake jingine ni kutafuta wafadhili wanaotambulika, wanaoweza kuwasaidia kuwapa fedha, ikiwemo magari kama inavyofanyika kwa vyama vingine.
“Nilikotoka nilikuwa na watu wanaosaidia, nitahama nao, watakuja ili kuziba upungufu ninaouona na malengo yangu ndani ya miezi mitatu, chama kiwe tofauti katika ramani za kisiasa nchini,” anaeleza Doyo.
Anasema chama hicho kina wanachama 125,000, hivyo, ataanza kuwafuatilia waliosajiliwa kwenye rejesta na kusajili wengine wapya kwa kushirikiana na mikoa.
Doyo anasema dhana iliyojengeka nchini ya vyama vidogo kutumika na chama tawala kuhalalisha mambo yake, inajengwa na wanasiasa waoga kwa sababu ya mitazamo yao tofauti.
Anasema baadhi ya vyama vingi vya upinzani nchini vimekuwa vikilalamikiwa haviwi mstari wa mbele kuungana na Chadema pale wanapoandamana kudai haki, lakini ukweli ni kwamba hawashirikishwi.
“Tatizo hatuthaminiwi, mfano Chadema wanaandaa maandamano unakuta hawatushirikishi wala kutupa taarifa, sasa unakuta wanasema Watanzania jitokezeni Septemba 23, 2024 tukakomeshe utekaji na mauaji.
“Tunaendaji wakati hatujashirikishwa na hatujui ajenda ya kufanya hivyo na hujui yanaanzia wapi na kuishia wapi? Unasemaje utashiriki maandamano hayo, ili iweje? Unaposema hivyo unaambiwa unatumika,” anasema.
Doyo anasema kila nyumba ina utaratibu wake, hawawezi kushiriki jambo ambalo hawajashirikishwa kiufundi, huku akieleza kama wangekuwa wanashirikiana nao, wengetoa maoni ya namna bora ya kuboresha.
“Waliotekwa na kuuawa ni wengi tangu mwaka 1998, katika mauaji ya Mwembe Chai, Chadema na CUF walikuwepo, alipigwa risasi kijana mmoja anaitwa Chuki Athumani, hakuna aliyetoka kuandamana,” anasema.
Anasema wanashindwa kuungana na Chadema kwa kuwa matukio hayo yanakuwa na ajenda zao binafsi. Ikiwa ajenda ni kukomesha mauaji na utekaji wako wengi walikutana na madhila hayo lakini wanakuwa kimya.
Doyo anasema tangu Rais Samia Suluhu Hassan alipoingia madarakani Machi 19, 2021, kuna mabadiliko makubwa, tofauti na miaka saba iliyopita, ikiwemo kuruhusu vyama vya siasa kufanya mikutano ya hadhara.
“Pili, wanasiasa tumekuwa huru kutoa maoni yetu na ujio wa 4R umetuwekea wigo mpana wa kufanya siasa na kwa mtazamo wangu, hali ya kisiasa inaridhisha kwa sababu tumekuwa tukifanya kazi bila kashikashi,” anasema.
Kuelekea kwenye uchaguzi, anasema chama hicho kitashiriki uchaguzi wa serikali za mitaa kwa kuweka wagombea nchi nzima na kwa sasa wamejifungia kuweka miongozo itakayoratibiwa na kupelekwa mikoani.
“Tunataka wanachama wetu washiriki kikamilifu na kuandaa wagombea kupitia kura za maoni za chama. Tumejipanga kushiriki uchaguzi kwa nguvu zote na kuanzia Oktoba tutaanza ziara nchi nzima,” anabainisha Doyo.
Wito wake kukuza demokrasia nchini
Doyo anasema licha ya Tanzania kuweka mifumo mizuri ya kidemokrasia, wananchi wengi hawana moyo wala mwamko wa kujiunga na vyama vya siasa kushiriki shughuli za kisiasa.
“Wananchi hawana moyo wa kujiunga na vyama vya siasa, ni muhimu kuongeza jitihada za kutoa elimu ya uraia kwa watu wengi ili wavutiwe kushiriki na kufanya siasa,” anasema.
Anasema hata vyama vya siasa vilivyopo nchini, akiondoa chama tawala, utekelezaji wa shughuli zao ni mdogo, huku akishauri kuongeza ushawishi wa ukuaji wa demokrasia, ni lazima kuwepo gharama.
“Serikali iruhusu mashirika binafsi kusaidia vyama vya siasa ili viweze kukua kwa sababu vinahitaji uchumi wa kuweza kujiendesha na kufanya shughuli zao,’” anasema.
Katika maelezo yake, Doyo anasema jambo hilo ni la msingi zaidi kwa kuwa kufanya ziara moja wanahitaji fedha nyingi zaidi ya Sh2 milioni, zote hizo zinaingia kwenye chakula na malazi.
“Hizo ni gharama kubwa, tunaomba sheria katika eneo la kukuza demokrasia, taasisi zisizokuwa za kiserikali ziachiwe ili ziwe huru kusaidia vyama, ingawa kutakuwa na masharti kadhaa,” anasema