KOCHA wa Singida Black Stars, Patricks Aussems amempongeza Emmanuel Keyekeh aliyetwaa tuzo ya mchezaji bora wa mechi mara tatu katika michezo minne ya Ligi Kuu Bara akisema inatakiwa kuwa chachu kwa Mghana huyo kufanya makubwa zaidi.
Keyekeh ndiye aliyewafanya mashabiki wa Pamba Jiji kuondoka juzi wakiwa vichwa chini kwenye uwanja wa nyumbani, CCM Kirambu baada ya chama lao kupoteza kwa bao 1-0.
Aussems alisema: “Kiukweli ni mchezaji mzuri na amekuwa na mchango mkubwa kwenye kikosi chetu lakini anatakiwa kupokea hilo kama chachu ya kuendelea kupambana kwa kushirikiana na wachezaji wenzake katika kufanikisha mipango ya timu, mimi sio aina ya kocha ambaye hupenda kuongelea mchezaji mmoja mmoja,”
Alisema: “Kiwango chake ni matokeo ya namna ambavyo timu imekuwa ikicheza. Kama kocha nina wajibu wa kupata kilicho bora kutoka kwa kila mmoja. Tutaendelea kufanya kazi kwa bidii kwa sababu safari bado ndefu, ila nafurahishwa na mwenendo wa timu.”
Kwa upande wake, Keyekeh aliwashukuru wachezaji wenzake na benchi la ufundi akisema: “Sidhani kama binafsi ningeweza kuwa mchezaji bora wa mchezo (dhidi ya Pamba) tulipambana wote kama timu na kufanikiwa kupata kile ambacho tulikuwa tukihitaji.”
Keyekeh siyo tu kiungo anayeweza kupambana kwenye ulinzi, bali ana kipaji cha kusukuma mashambulizi ya timu. Uwezo wake wa kupiga pasi sahihi na kuanzisha mashambulizi kwa kasi ni matokeo ya mazoezi aliyofanya ili kuiga ufanisi wa wachezaji hao.
Kabla ya kutua Singida Black Stars alizichezea Karela United, Asante Kotoko na Samartex za kwao Ghana.