Salum Chuku kuikosa Fountain Gate

WAKATI kikosi cha Tabora United kikianza maandalizi ya kuiwinda Fountain Gate, inatarajia kuikosa huduma ya nyota wake, Salum Chuku.

Chuku ambaye alifunga bao moja wakati Tabora United ikishinda 2-1 ugenini dhidi ya Namungo, aliumia katika mchezo uliopita dhidi ya Tanzania Prisons ambapo alishindwa kuendelea.

Keshokutwa Ijumaa, Tabora United itakuwa mwenyeji wa Fountain Gate kwenye mwendelezo wa Ligi Kuu Bara mchezo utakaopigwa Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi, Tabora.

Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa Tabora United, Christina Mwagala, amesema: “Tumeanza maandalizi ya mchezo mwingine kwa sababu ule tayari umeshapita, tuliwapa mapumziko wachezaji kwa sababu baada ya kumaliza mechi dhidi ya Kagera Suger hatukuwa na muda wa kupumzika na badala yake tuliendelea kujiandaa dhidi ya Tanzania Prisons, kwahiyo baada ya mapumziko wachezaji wamerudi na nguvu mpya ya kuendeleza mapambano.

“Maandalizi yaliyoanza yanahusisha wachezaji wote isipokuwa Salum Abdalah Chuku ambaye aliumia kwenye mchezo dhidi ya Tanzania Prisons na kushindwa kuendelea, hivyo alipelekwa hospitali na kwa sasa anaendelea vizuri.”

Mwagala alibainisha kwamba, katika maandalizi hayo, kocha mkuu wa kikosi hicho, Francis Kimanzi anaanza kuyafanyia kazi mapungufu yaliyojitokeza mchezo uliopita nyumbani walipotoka 0-0 dhidi ya Tanzania Prisons lengo ni kuendelea kufanya vizuri.

Related Posts