Simba na refa wa ‘majaribio’

REFA asiye na uzoefu mkubwa wa kuchezesha mechi za kimataifa, Abdoulaye Manet (34) kutoka Guinea ndiye amepangwa kuchezesha mechi ya marudiano ya raundi ya pili ya Kombe la Shirikisho Afrika kati ya Simba na Al Ahli Tripoli itakayochezwa kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Jumapili ijayo kuanzia saa 10:00 jioni.

Manet alipata beji ya urefa ya Fifa mwaka 2020 na alianza kupangiwa mechi za kimataifa, Februari 21, 2021 ambapo alikuwa refa wa akiba wa mechi ya Kombe la Shirikisho Afrika ambayo Jaraaf ya Senegal ilipata ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Platinum ya Zimbabwe.

Mchezo wa kwanza kwa Manet kuchezesha ulikuwa ni wiki iliyopita, Septemba 10 wa kuwania kufuzu fainali za mataifa ya Afrika (Afcon) 2025 baina ya Zimbabwe na Cameroon ulioisha kwa suluhu.

Refa huyo amechezesha idadi ya mechi saba tu,  ambapo sita alikuwa refa wa akiba na moja tu ndio alipuliza kipyenga.
Hakuwahi kuchezesha mechi yoyote ya klabu Afrika akiwa refa wa kati, hivyo mchezo huo wa Simba na Al Ahli Tripoli utakuwa wa kwanza kwake.

Wakati Manet akipangwa kuchezesha mechi ya Simba, refa Abdel Aziz Bouh wa Mauritania yeye amepangwa kuchezesha mechi ya marudiano ya raundi ya pili Ligi ya Mabingwa Afrika baina ya Yanga na CBE ya Ethiopia itakayochezwa Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar, Jumamosi kuanzia saa 2:30 usiku.

Bouh (32) atasaidiwa na raia wenzake wa Mauritania, Brahim H’Made,  Mohamed Youssef na Diou Moussa kuchezesha mechi hiyo ambayo Yanga inahitaji angalau sare tu ili isonge mbele baada ya ushindi wa bao 1-0 ugenini Jumamosi iliyopita.
Refa Bouh alipata beji ya kimataifa ya Fifa kwa mara ya kwanza mwaka 2019.

Hii ni mechi ya nne kwa Bouh kuichezesha Yanga kwani tayari ameshafanya hivyo mara tatu, zikiwamo mbili alikuwa refa wa kati na moja alikuwa mwamuzi wa akiba.

Mechi ya kwanza kwa Bouh kuichezesha Yanga ilikuwa ni dhidi ya TP Mazembe, Februari 19, 2023 na Yanga iliibuka na ushindi wa mabao 3-1, kisha aliichezesha tena Yanga dhidi ya Al Ahly, Desemba 2, 2023 iliyoisha kwa sare ya bao 1-1, pia akiwa refa wa akiba wa mchezo kati ya Mamelodi Sundowns na Yanga, Aprili 5, 2024 ambao dakika 90 zilimalizika kwa suluhu na Yanga kufungwa kwa penalti 3-2.

Katika mechi nane zilizopita za klabu Afrika, Bouh ametoa idadi ya kadi 24 ikiwa ni wastani wa kadi tatu kwa mchezo na katika hizo, moja tu ndio nyekundu.

Msimu uliopita, Yanga na Simba zilifanikiwa kuingia makundi na zilitolewa katika robo fainali ya mashindano ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Yanga ilitolewa na Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini wakati Simba ilitolewa na Al Ahly ya Misri.

Kipa wa zamani wa Yanga, Juma Pondamali alisema kuwa timu hizo za Tanzania hazipaswi kuingiwa wasiwasi na marefa watakaozihukumu wikiendi hii.

“Refa anachezesha kwa kufuata sheria 17 za mpira wa miguu, hivyo kuwa nyumbani haimaanishi kwamba Yanga na Simba zitapendelewa au kuonewa na marefa. Wachezaji wanapaswa kujituma ili kuziwezesha timu zetu kufanya vizuri katika mechi hizo ambazo ni muhimu,” alisema Pondamali na kuongeza;

“Na nina imani timu zote mbili zitafanikiwa kuingia katika hatua ya makundi kwa kishindo maana uwezo zinao na sababu zipo za kufanya hivyo.”

Related Posts