TANZANA inaikaribisha Mali katika mchezo wa kihistoria wa ufunguzi wa michuano ya kufuzu fainali za Kombe la Dunia za kriketi ya mizunguko 20 keshokutwa, Dar es Salaam.
Ni mchezo unaoikaribisha Mali, nchi iliyotawalia na Wafaransa katika mchezo unaochezwa zaidi na nchi za Jumuiya ya Madola ambazo huzungumza Kiingereza.
Mali inajiunga na Msumbiji nchi inayoongea Kireno ambayo imekuwa mshiriki wa kawaida ya michuano ya kriketi ukiwemo ule uliomalizika hivi karibuni wa kufuzu kucheza Kombe la Dunia kwa vijana walio chini ya miaka 19.
Wakishiriki kwa mara ya kwanza nchini Tanzania, Mali ni moja ya mataifa sita yatakayoshiriki michuano ya kufuzu Kombe la Dunia.
Nchi nyingine ni Cameroon, Ghana, Lesotho na Malawi ambazo ni mataifa yanayozungumza Kiingereza kama lugha rasmi.
Ingawa haipo katika mashindano hayo, Rwanda ndiyo nchi ya Kifaransa inayofanya vizuri katika kriketi kwa Afrika na mafanikio yake yalichagizwa na mabadiliko ya nchi hiyo kubadili lugha kutoka Kifaransa kwenda Kiingereza.
Tanzania inaikaribisha Mali baada ya wachezaji wake kufanya mazoezi ya kina na mechi nyingi za majaribio wakijigawa kwa majina ya Mikumi na Serengeti.
“Tuko tayari na vijana wameandaliwa vyema kwa mashindano haya. Naamini hatutawaangusha Watanzania,” alisema Atif Salim ambaye ni ofisa habari wa Chama cha Kriketi Tanzania (TCA).
Katika mashindano hayo, kwa mujibu wa ratiba Tanzania itacheza na Mali Jumamosi, Septemba 21 katika Uwanja wa Dar es Salaam Gymkhana.
Siku hiyo hiyo, Lesotho watacheza na Malawi katika uwanja wa UDSM saa tatu asubuhi na saa saba mchana uwanja huo utaishuhudia Cameroon ikimenyana na Ghana.
Siku ya pili, Tanzania itakuwa kibaruani katika Uwanja wa UDSM dhidi ya Lesotho baada ya kumalizika kwa mechi ya asubuhi kati ya Camertoon na Mali, wakati uwanja wa Dar Gymkhana utakuwa shuhuda wa mechi kati ya Ghana na Malawi.
Septemba 23 itakuwa siku ya mapumziko kabla ya timu kurejea tena uwanjani Septemba 24.
Tanzania itakuwa na mechi ya tatu katika uwanja wa UDSM ikipambana na Cameroon wakati uwanja wa Dar Gymkhana utakuwa ukitimua nyasi kwa mechi kati ya Ghana na Lesotho, baadaye Malawi watakuwa wakikiwasha na Mali. Septemba 24, Tanzania itakuwa tena katika uwanja wa Dar Gymkhana ikipambana na Ghana kabla ya Cameroon kuumana na Malawi majira ya mchana.
Tanzania itamaliza kibarua chake kwa kuikaribisha Malawi katika uwanja wa UDSM baada ya kumalizika kwa mechi kati ya Ghana na Mali na ile kati ya Cameroon na Mali ndiyo itakayofunga dimba la michuano katika uwanja wa Dar Gymkhana.