Tanzania yaendeleza mikakati kufikia usawa wa kijinsia

Dar es Salaam. Ili kufikia usawa wa kijinsia nchini kupitia Programu ya Jukwaa la Kizazi chenye Usawa (GEF), Tanzania imejizatiti kutekeleza uwiano sawa kati ya wanaume na wanawake.

Kamati ya Kitaifa ya Ushauri (GEF) ilianzishwa na Rais Samia Suluhu Hassan Desemba 2021 kwa ajili kufuatilia na kushauri kuhusu maendeleo ya utekelezaji wa jukwaa hilo.

Akizungumza leo Jumatano Septemba 18, 2024 jijini Dar es Salaam kwenye mkutano wa ulioandaliwa na Shirika la Umoja wa Mataifa la uwezeshaji wanawake (UN Women), mshauri wa Rais na Mwenyekiti wa GEF, Angellah Kairuki amesema Tanzania inatekeleza mpango wa malezi na makuzi kwa kuhakikisha baba na mama wanafanya biashara ili kutokwamishwa suala la malezi.

“Ili kuhakikisha hayo yanatekeleza ndio maana tunahusisha sekta binafsi na asasi nyingine za kiraia. Tunataka tuone katika ngazi za uongozi kuwe na wanawake na wanaume akitolea mfano bodi za wakurugenzi,” amesema Kairuki.

Amesema waliandaa mpango kazi huo wa miaka sita na Serikali itahakikisha kila hatua inashirikisha sekta binafsi.

“Wanavyotoa fursa za ajira kwa wanawake, uongozi, umiliki wa wanawake kwenye hisa na tunaamini tutaendelea kupiga hatua zaidi kimataifa huku ikiwa ni faida kwa uchumi wa nchi,” amesema Kairuki.

“Tanzania imeahidi kuinua programu za kitaifa katika sekta mbalimbali za malezi ya watoto na kuanzisha vituo vya kulelea watoto katika ngazi ya kijiji, sehemu za kazi na sokoni,” amesema.

Katika programu hiyo, Tanzania imetekeleza ahadi nne kwa kuteua vituo vya GEF katika mikoa yote 26 ya Tanzania bara, mikoa mitano ya Zanzibar na ndani ya mamlaka za Serikali za mitaa nchi nzima.

Mwakilishi wa Mkurugenzi Mkazi wa UN Women, Dk Mitra Sadananda amesema ahadi ya Tanzania ya kuendeleza usawa wa kijinsia imewezesha wanawake kiuchumi.

“Lengo letu ni kukuza sekta ya binafsi inayowajibika kwa kuhakikisha upatikanaji sawa wa wanawake, ushiriki, sauti, wakala na usalama katika sera na desturi zote mahali pa kazi, sokoni na jamii,”amesema  Dk Sadananda.

Aidha, Mtendaji Mkuu wa Chama cha Waajiri Tanzania (ATE) Suzanne Ndomba-Doran, amesema wanataka kutengeneza usawa wa kijinsia katika maeneo ya kazi.

“Chama chetu kina programu maalumu inayotoa mafunzo kwa wanawake waliopo sekta binafsi na hadi sasa wamehudhuria takribani 497.

“Tunafundisha uongozi, mawasiliano, kuingia katika vikao vya bodi lengo ili wapate nafasi mbalimbali za uongozi katika sehemu zao za kazi,” amesema Ndomba-Doran.

Mkurugenzi Mkuu Taasisi ya Sekta Binafsi (TPSF), Raphael Maganga amesema wanahakikisha usawa wa kijinsia ni suala linalopewa kipaumbele katika taasisi za sekta binafsi.

Related Posts