Tauossi ataja mambo matatu, Azam ikiivaa KMC

KIKOSI cha Azam FC kinatarajiwa kushuka uwanjani kesho jioni kuvaana na KMC katika mechi ya Ligi Kuu Bara, huku kocha Rachid Taoussi akifichua kuwa ameanza kuielewa ligi baada ya kuisoma na kubaini anahitaji mambo matatu kutambulisha falsafa yake.

Rachid aliyeanza kibarua kwa suluhu na Pamba Jiji, alisema mambo anayotaka wachezaji wake wayafanye wakati wakikabiliana na KMC saa 10:00 jioni ni kuzuia ipasavyo, kumiliki na kushambulia kwa kasi wanapokuwa eneo la wapinzani.

Kocha huyo, raia wa Morocco aliyetua hivi karibuni kuchukua nafasi ya Youssouf Dabo, kabla ya kuja Azam alifanya tathmini ya kikosi na kubaini ana wachezaji wenye uwezo mkubwa wa kuyatekeleza.

“Tunaweza kuanzia hapo. Naamini tutajenga timu bora na imara ambayo itapigania makombe na siyo kumaliza tu katika nafasi za juu. Natambua ujenzi wa timu sio jambo la siku moja lakini tutajitahidi kuhakikisha suala la ujenzi na timu likiambatana na matokeo mazuri,” alisema Taoussi.

“Nina uzoefu wa kutosha na bahati nzuri nilipata nafasi ya kuongea na wachezaji niliwaeleza wazi mimi ni kocha wa aina gani, nini napenda kuona kwenye kikosi. Niliwaambia kila mmoja ana nafasi ya kucheza itategemea na vile anavyojituma kunzia mazoezini.”

Kimbinu kocha aliyepita wa Azam, Dabo alijenga kushambulia zaidi huku ikionysha upungufu katika kujilinda hasa mwanzoni mwa msimu huu ambapo iliruhusu mabao manane katika michezo minne ya kwanza ikiwemo miwili ya Ngao ya Jamii.

Juu ya mechi ya leo, Taoussi alisema: “Mechi dhidi ya KMC itatupa mwelekeowa kile ambacho tunahitaji kukifanya, tumekuwa na siku kadhaa za kujiandaa naamini tutapata ushindi wetu wa kwanza.”

Kocha wa KMC,  Abdihamid Moallin alisema: “Tunakutana na miongoni mwa timu bora katika ligi lakini sisi ni KMC, tumejiandaa kukabiliana nao. Tunahitaji kuwa na muendelezo wa matokeo mazuri.”

Azam ya Dabo msimu uliopita ilivuna pointi sita dhidi ya KMC –  mchezo wa kwanza ikishinda mabao 5-0 na marudiano walishinda kwa mabao 2-1.

Related Posts