Temesa yaziita sekta binafsi  uwekezaji vivuko, utengenezaji magari

Dar es Salaam. Baada ya kusuasua kiuendeshaji, hatimaye Wakala wa Ufundi na Umeme Tanzania (Temesa), imetangaza kubadili mfumo wa utekelezaji wa majukumu yake, kwa kushirikiana na sekta ya umma na binafsi kupitia ubia (PPP).

Kutokana na mabadiliko hayo, Temesa imewaita wawekezaji wa sekta binafsi kutoka ndani na nje ya nchi kuwasilisha mapendekezo ya ushirikiano huo katika huduma za vivuko, karakana za ufundi magari na ufundi umeme.

Kwa mujibu wa taarifa za Temesa, wakala unakuja na mpango huo ikiwa ni miezi mitatu tangu Mwananchi iliripoti mfululizo wa ripoti maalumu zinazoonyesha wakala huo kulemewa na majukumu, kuathiriwa na mifumo na hata kujikuta ikiangukia katika madeni.

Ripoti hiyo iliyotokana na uchunguzi uliofanywa kwa takriban miezi mitatu, inaweka Temesa kukiuka mpango wa matengenezo ya vivuko na kudaiwa zaidi ya Sh30 bilioni na wasambazaji wa vipuli kwenye karakana zake za ufundi magari.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, ubia wa sekta ya umma na binafsi ndiyo ulioonekana kama suluhu ya changamoto zote zinazoukabili wakala huo na sasa hatimaye umeanza kulitekeleza hilo kwa kushirikiana na Kamishna wa Ubia wa Sekta ya Umma na Binafsi (PPP), David Kafulila.

Hata hivyo, pamoja na ubia huo kuwa fursa kwa sekta binafsi, baadhi ya watu wamesema kunahitajika uhuru wa kuamua baadhi ya mambo ili kuzalisha faida kwa pande mbili.

Ushirikiano katika vivuko

Kwa mujibu wa taarifa hiyo ya ndani ya Temesa, wakala huo umewaalika wawekezaji wa ndani na nje ya nchi kuwasilisha mapendekezo yao kwa ajili ya kuwekeza kwenye uendeshaji wa vivuko kupitia mpango wa PPP.

Taarifa inaeleza kuwa, mwekezaji ana fursa ya kuwekeza kwa njia ya kukodisha vivuko vyote, kuunda ubia wa pamoja au kuendesha vivuko vyake sambamba na vile vya Temesa.

Kwa mujibu wa taarifa, mwekezaji anayeonyesha nia, anapaswa kuwasilisha nakala zilizothibitishwa za hati za kisheria za taasisi husika na muhtasari wa maelezo ya awali ya uwekezaji.

Pia,  mwekezaji huyo anapaswa kuwasilisha maelezo ya awali ya uwekezaji, kutoa muhtasari wa mradi uliopendekezwa na uwezo wake wa kufikia ufanisi, unafuu wa kifedha na thamani.

Katika pendekezo hilo, mwekezaji anatakiwa kutuma idadi ya vivuko atakavyoendesha na idadi ya abiria na magari yatakayohudumiwa kwa mwaka.

Kwa mujibu wa Temesa katika tangazo hilo, mradi uliopitishwa utapaswa kuanza ndani ya miezi 24 kwa kusaini mkataba wa utendaji na kuwasilisha dhamana ya benki, kiasi kitakachokubaliwa kati ya Temesa na mwekezaji mtarajiwa.

Pia, taarifa hiyo inataka ulinganifu na Dira ya Maendeleo ya Taifa ya Tanzania 2025 na mipango ya kitaifa ya maendele.

“Thamani ya fedha kwa manufaa kwa Serikali, ikihusisha kuchochea maendeleo ya kiuchumi, kuongeza huduma, ajira na ukuaji wa uchumi, mageuzi ya teknolojia na kuongeza mapato ya Taifa,” inaeleza taarifa hiyo.

Ushahidi wa uwezo wa kifedha wa wawekezaji kwa kuwasilisha ripoti za fedha zilizokaguliwa kwa miaka mitatu, uzoefu wa mwekezaji katika kutekeleza miradi kama hiyo ni vigezo vingine vilivyobainishwa.

Pia, uwezo wa kuboresha na kuendesha vivuko kwa kutumia teknolojia ya kisasa, makadirio ya gharama za mitaji ya uwekezaji, faida zinazopendekezwa kulipwa kwa Temesa na faida za kijamii zinazopendekezwa kwa jamii inayozunguka mradi huo.

Kwa upande wa karakana, Temesa imewatangazia wawekezaji kushirikiana nayo katika uendeshaji wa karakana 13 kupitia mpango wa PPP. Ni kati ya 30 zilizopo kwenye mikoa 26.

Limesema baada ya hatua hiyo, Temesa itachagua wawekezaji watakaokidhi vigezo vya tathmini na baadaye kuwaalika waombaji waliofanikiwa.

Tangazo hilo hilo pia limetolewa kwa sekta binafsi itakayoshirikiana nayo katika ufundi wa umeme.

Alichosema Kamishna wa PPP

Kamishna wa PPP, David Kafulila akizungumza na Mwananchi leo Jumatano, Septemba 18, 2024 amesema ushirikiano huo unalenga kufanywa katika uendeshaji wa karakana 13 kati ya 30 za wakala huo, sambamba na majukumu mengine kama vivuko na ufundi.

Kwa upande wa magari, amesema karakana hizo 13 zipo katika mikoa ya Katavi, Rukwa, Shinyanga, Kagera, Singida, Iringa, Mara, Manyara, Pwani, Lindi, Ruvuma, Njombe na Simiyu.

Hata hivyo, Kafulila amesema hatua hiyo ya Temesa inaakisi matakwa ya Kanuni ya 36 (b) na (d) ya Ubia kati ya sekta ya umma na binafsi ya mwaka 2020 na marekebisho yake ya mwaka 2023.

Kanuni hiyo inairuhusu Temesa kuwaalika wawekezaji katika utekelezaji wa miradi yake kwa njia ya ubia.

“Mpango wa Temesa kuboresha karakana zake na kutoa huduma kwa njia ya ubia unatoa matumaini ya kukidhi mahitaji ya huduma za matengenezo kwa aina mbalimbali za magari na mitambo,” amesema.

Kafulila amesema hatua hiyo itawezesha kuvutia teknolojia za kisasa, kuchochea ufanisi wa uendeshaji na kuboresha ubora wa huduma. 

“Mageuzi makubwa yatazidi kutokea katika miradi ya ubia baada ya Kituo cha Ubia wa Sekta ya Umma na Binafsi kufikia azma yake ya kutoa huduma zote za ubia ndani ya kituo (one-stop centre),” ameeleza Kafulila.

Akizungumza kuhusu ushirikiano katika uendeshaji wa vivuko, mmoja wa maofisa wa ngazi ya juu kutoka moja ya kampuni binafsi zinazoendesha huduma za vivuko nchini (jina lake limehifadhiwa), amesema hiyo ni fursa kwa upande mmoja lakini inahitaji maelewano kwa upande mwingine.

Kwa upande wa fursa, ameeleza kwa sababu kuna mahitaji makubwa ya abiria kutumia usafiri huo, bila shaka ni biashara nzuri na yenye faida.

Lakini, fursa hiyo amesema haitakuwa kama inavyotarajiwa iwapo Temesa haitatoa uhuru kwa mwekezaji huyo kutoka sekta binafsi wa kupanga baadhi ya mambo kwa maslahi ya pande zote.

Miongoni mwa mambo hayo, alitaja ni nauli kwa abiria, utaratibu wa uendeshaji, mbinu za ukusanyaji nauli na hata mageuzi ya huduma kwa ujumla wake.

“Kiufupi isiwe huduma iwe biashara, sekta binafsi inatafuta faida, wenzetu serikali wanahudumia. Kama wanataka ubia wakubali kukaa pembeni washuhudie biashara ikifanyika wabaki kusimamia ili wachungulie mapato,” amesisitiza.

Mkuu wa Idara ya Usafirishaji na Biashara wa Chuo cha Taifa cha Usafirishaji, Dk Prosper Nyaki ameeleza ushirikiano huo utawezekana iwapo Serikali itaendelea kukusanya nauli na kumlipa mwekezaji kulingana na gharama zake za uendeshaji.

Ikitoa ruhusa kwa mwekezaji kukusanya, amesema itakuwa vigumu kuilipa Serikali kwa kuwa inaonekana gharama za uendeshaji wa vivuko ni kubwa ukilinganisha na nauli inayotozwa.

“Kwa nauli sekta binafsi haitaweza kulipa labda Serikali ije na mbinu ya mwekezaji atoe huduma na Serikali iwe inawalipa,” ameeleza Dk Nyaki.

Hata hivyo, mwanazuoni huyo amesema kwa kawaida usafiri wa umma huwa ni huduma na sio biashara na unapoishirikisha sekta binafsi unalenga kupata faida.

“Napata shida kujua itawezekanaje ukizingatia nauli wanayolipa abiria hailingani na gharama halisi za uendeshaji wa vivuko, sijui mwekezaji atapataje faida,” amesema.

Pia, Dk Nyaki amesema ushirikiano utakuwa na tija iwapo mwekezaji huyo ataamua kuja na vivuko vyake.

Kuhusu karakana, mtaalamu wa ufundi, Salim Msami amesema itakuwa vema kwa sekta binafsi kuunda ubia na Temesa kwa kuwa wadau hao binafsi watajihakikishia upatikanaji wa soko.

“Serikali ina magari mengi kwa hiyo ukishirikiana nao moja kwa moja unakuwa na uhakika wa wateja,” amesema Msami ambaye pia ni ofisa katika kampuni binafsi ya Hyundai.

Ili ushirikiano huo uwezekane, amesema kunahitajika kuwepo na sharti la wadau wote wawili kuwa sehemu ya uongozi na mgawanyo wa majukumu na mapato ueleweke vema.

Amesisitiza sekta binafsi imejikita katika faida zaidi na sio kutoa huduma, ili Temesa ishirikiane nayo vema inahitaji kubadili mfumo wa utendaji wake na kuweka wazi makubaliano ya uendeshaji wa karakana hizo.

Msami amesema kunahitajika uhuru wa uendeshaji wa karakana hizo kwa sekta binafsi iwapo itapewa kazi hiyo.

Related Posts