Ushindi dhidi ya Coastal wampa jeuri Zahera

USHINDI wa kwanza ilioupata Namungo mbele ya Coastal Union katika mechi ya Ligi Kuu Bara, umemfanya kocha wa timu hiyo kutamba ameanza kupata mwanga baada ya awali kupoteza michezo mitatu mfululizo iliyomvuruga akili.

Namungo ikicheza ugenini dhidi ya Coastal kwenye Uwanja wa KMC, Dar es Salaam ilishinda mabao 2-0 yaliyofungwa na Ritch Nkoli na Pius Buswita na kumaliza upepo mbaya ilioanza nao timu hiyo msimu huu.

Timu hiyo ilianza kwa kufungwa 2-1 na Tabora United, kisha kulala 2-0 kwa Fountain Gate ikiwa nyumbani kabla ya kupigwa 1-0 ugeninio na  Dodoma Jiji, matokeo yaliyohatarisha kibarua cha kiocha huyo wa zamani wa Yanga, Gwambina na Coastal Union na juzi ndipo ikashinda kwa Wagosi.

Ushindi huo umemfanya Zahera kuliambia Mwanaspoti Zahera kukosa matokeo mazuri mfulululizo haikumaanisha kuwa ana kikosi kibovu, sema ilikuwa ni upepo mbaya iliyoipitia timu hiyo na sasa mambo yameanza kunyooka taratibu.

Zahera alisema alikuwa anaamini ilikuwa ni suala la muda tu kwa kikosi hicho kukaa katika hali nzuri na kupata matokeo mazuri na ndio maana ikicheza mbele ya Coastal mambo yamekuwa tofauti.

“Safu ya ushambuliaji na kikosi kwa ujumla kilitimiza yote niliyowafundisha kwani walitumia nafasi zote walizopata vizuri. Hatuna kikosi cha kidogo bali tumejipanga vilivyo na tulifanikiwa kufika katika kila nafasi kwa wakati, jambo ambalo litakuwa endelevu na tutafunga sana,”  alisema Zahera.

Kocha huyo raia wa DR Congo alisema kwa sasa wanajiweka tayari kwa mchezo ujao utakaopigwa nyumbani Septemba 28 dhidi ya Tanzania Prisons, baada ya mchezo uliokuwa upigwe wikiendi hii dhidi ya Simba kusogezwa mbele kutokana na Wekundu kuwa na jukumu la kimataifa. Simba inatarajiwa kurudiana na Al Ahli Tripoli ya Libya Jumapili kwenye Uwanja wa Mkapa katika mechi ya raundi ya pili ya Kombe la Shirikisho baada ya wikiendi iliyopita kutoka suluhu ugenini na mshindi wa jumla wa mechi hiyo atafuzu makundi ya michuano hiyo kwa msimu huu.

Related Posts