Dar es Salaam. Wadau wa taaluma ya habari, wameonyesha matumaini ya kuimarika kwa usimamizi wa weledi wa taaluma hiyo, baada ya Serikali kuunda Bodi ya Ithibati ya Wanahabari.
Hatua ya kuundwa kwa bodi hiyo, ni matakwa ya kifungu cha 11 cha Sheria ya Huduma za Habari ya mwaka 2016, iliyotamka pamoja na mambo mengine kutakuwa na chombo hicho.
Maoni hayo ya wadau yanatokana na hatua ya Serikali kuunda bodi hiyo na kuteuwa wajumbe watano na mwenyekiti wake, Tido Muhando.
Wajumbe hao katika tume hiyo ni Msemaji Mkuu wa Serikali, Thobias Makoba, mwanahabari Kingoba Bakari, Mkurugenzi Mkuu wa Chama cha Wanahabari Wanawake (Tamwa), Dk Rose Reuben, Egbert Mkoko na Ladislaus Komanya.
Kwa mujibu wa taarifa kwa umma iliyotolewa na Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, uteuzi wa wajumbe hao umefanywa na waziri wa wizara hiyo, Jerry Silaa na umeanza leo, Septemba 18, 2024.
Akizungumzia hatua hiyo leo, Septemba 18, 2024, Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Deodatus Balile pamoja na kuwapongeza walioteuliwa kuiongoza amesema ni imani yake uwepo wa bodi hiyo utaondoa adha ya wanahabari kupelekwa mahakamani kwa makosa ya kitaaluma.
Amesema kuundwa kwa bodi ya ithibati, kunafungua mlango wa kuundwa kwa Baraza Huru la Habari Tanzania.
“Nafurahi watu walioteuliwa wamekulia kwenye taaluma ya habari na hivyo imani yangu kwao ni kubwa. Naipongeza Serikali kwa hatua hii ambayo imeshindikana tangu mwaka 2016,” amesema.
Amesisitiza hiyo ni hatua kubwa na ushindi kwa wanataaluma kwa kuwa jambo hilo, lilipambaniwa kwa muda mrefu na sasa limekuwa.
Kwa upande wa Mwenyekiti wa Taasisi ya Vyombo vya Habari Kusini mwa Afrika (MISA-TAN), Salome Kitomari amesema kilichofanyika ni utekelezaji wa Sheria ya Huduma za Habari ya mwaka 2016, hivyo ni jambo jema.
“Walioteuliwa ni wenye uzoefu kwenye taaluma ya habari nchini, tunaamini watakwenda kukidhi matakwa na kiu ya wanataaluma kwa kuzingatia majukumu sita yaliyotajwa katika sheria,” ameeleza.
Kwa jicho la kijinsia, amesema bado uwakilishi wa wanawake uko chini kwa kuwa kati ya wajumbe sita ni mmoja tu ndiye mwenye jinsi hiyo.
“Ilitarajiwa kuwe na uwiano fulani hasa tukizingatia idadi ya wanataaluma wanawake waliopo na jitihada za kuongeza idadi ya wananawake kwenye ngazi za maamuzi,” amesema.
Pia, amesema kwa sasa mambo mengi ya kitaalumu yatashughulikiwa na baraza, hivyo ni hatua nzuri kwa taaluma ya habari.