Wizara ya Katiba, TLS wakutana, wakubaliana haya

Baraza la Uongozi la Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) likiongozwa na rais wake, Boniface Mwabukusi wamekubaliana na Wizara ya Katiba na Sheria chini ya Waziri wake, Profesa Palamagamba Kabudi kushirikiana katika utekelezaji wa majukumu yanayohusu sekta ya sheria kwa kuzingatia mipaka na taratibu kwa maslahi mapana ya Taifa.

Makubaliano hayo yamefikiwa jana Jumanne, Septemba 17, 2024 baada ya kikao cha majadiliano kilichofanyika kwa zaidi ya saa sita katika ukumbi wa mikutano wizara, Mtumba jijini Dodoma. Hii ni kwa mujibu wa taarifa kwa umma iliyotolewa na wizara.

Katika kikao hicho, hoja mbalimbali ziliibuliwa na kutokana na uzito wa majadiliano hayo, Waziri Kabudi alielekeza baraza hilo la TLS likae kwanza na menejimenti ya wizara ikiongozwa na Katibu Mkuu, Eliakim Maswi kwa lengo la kujadili masuala ya kitaalamu na baada ya hapo ikafuatia awamu ya pili iliyomjumuisha waziri.

Hoja mbalimbali ziliibuliwa katika kikao hicho, mojawapo ikiwemo utekelezaji wa Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia (Mama Samia Legal Aid Campaign – MSLAC) ambapo TLS waliitaka wizara iwahusishe wanachama wengi zaidi wa TLS waliopo katika maeneo mbalimbali nchini.

Lengo ni mwendelezo wa huduma baada ya kampeni inapomalizika eneo husika. Waziri Kabudi alikubali ombi hilo na kuagiza iundwe kamati ya pamoja itakayojumuisha wanachama wa TLS na kuangalia namna bora zaidi ya kuboresha utekelezaji wa kampeni hiyo.

Aidha, jambo la pili lililojadiliwa ni pamoja na uanzishwaji wa Kituo cha Kimataifa cha Usuluhishi (Arbitration Center) ambacho kitakuwa chombo cha kimataifa ambacho kitachohudumia watu wa nchini na kutoka mataifa mbalimbali.

Katika hilo, Profesa Kabudi akaelekeza iundwe kamati na uandaliwe mpango mzuri juu ya uanzishwaji wa kituo hicho.

Katika hatua nyingine, Mwabukusi ameiomba wizara kupitia taasisi zake hasa Tume ya Kurekebisha Sheria kuhakikisha TLS inashirikishwa katika kutoa maoni katika miswada mbalimbali kabla ya kufanywa kuwa sheria, lengo ni kuhakikisha kunakuwa na sheria bora zaidi za kusaidia wananchi. Jambo ambalo Waziri Kabudi, nalo alikubali kama ilivyo kwa hoja nyingine.

Akizungumza baada ya kukamilika kwa kikao hicho, Profesa Kabudi amesema anaamini huo ni mwanzo mzuri, kwani wamekuwa na kikao kizuri chenye majadiliano marefu ya staha ambapo mambo mengi mazuri yenye kustawisha demokrasia ya nchi na ustawi wa jamii kupitia sekta ya sheria yamejadiliwa na kupatiwa ufumbuzi.

Kwa upande wake, Mwabukusi amesema amefarijika kwa kiasi kikubwa, kwanza kwa mapokezi ya heshima waliyopewa tangu walivyopokelewa wizarani hapo na namna mjadala ulivyoendeshwa, huku akisema huo ni mwanzo mzuri na wanatumaini kwa kusikilizana, masuala mbalimbali yanayowahusu wananchi kisheria yatapatiwa ufumbuzi.

Hii ni ziara ya kwanza ya rais wa TLS, Mwabukusi kufika wizarani kwa lengo la kujitambulisha tangu achaguliwe Agosti 3, 2024.

Related Posts