Baba mzazi mbaroni akidaiwa kufukua kaburi la mwanaye

Kyerwa. Baba mzazi wa mtoto wa mwaka mmoja, Faston Innocent anashikiliwa na Polisi akituhumiwa kufukua kaburi la mwanaye huyo na kuweka jeneza likiwa na mwili mlangoni mwa nyumba ya babu yake.

Mkuu wa Wilaya ya Kyerwa, Zaituni Msofe amelieleza Mwananchi leo Septemba 19, 2024 kuwa mtoto huyo alifariki dunia kwa ugonjwa wa malaria na alizikwa kijijini Magoma, Kata ya Bugomola nyumbani kwa babu yake, Venant Zabron.

Septemba 17, 2024 baada ya tukio la kufukua kaburi, uongozi uliamuru mtoto huyo azikwe upya.

New Content Item (1)

Innocent Chichoncho raia wa nchini Uganda wilaya ya Ntungamo mkoa wa Mbarara anayehusishwa kushikiliwa na Jeshi la Polisi kwa tuhuma za kuhusika na tukio la kufukua kaburi la mtoto wake na jeneza kuliweka mlangoni mwa nyumba ya babu yake.

Msofe amesema alfajiri ya Septemba 18, 2024 Jeshi la Polisi lilimkamata na kumfikisha Kituo cha Polisi Kyerwa baba wa mtoto huyo, Innocent Chichoncho ambaye ni raia wa Uganda akituhumiwa kuhusika na tukio hilo. Amesema uchunguzi unaendelea.

Msofe amesema mama wa mtoto huyo aliolewa nchini Uganda alikokuwa akiishi na mume wake, baada ya miaka mitatu walitengana akarudi nyumbani kwao Kyerwa.

Amesema mtoto huyo aliugua malaria akafariki dunia ndipo baba wa mtoto alipojulishwa akahudhuria mazishi.

Baada ya matanga amesema yalifanyika mazungumzo mwanamume huyo akaomba kurudi Uganda na mkewe ambaye alikataa hivyo kulizuka majibizano, mwanamume huyo akimweleza atamkomesha.

Mwenyekiti wa Kijiji Magoma, Kata ya Bugomola, Venance Nicholas amesema saa saba usiku wa kuamkia Septemba 17 alipigiwa simu na mkazi wa maeneo hayo kuwa kuna mtu amekuja kwake akihitaji msaada wa chakula na kulala, ambaye anamtilia shaka.

Amesema aliujulisha uongozi wa kata wakaenda ndipo walipomkuta Chichoncho, ambaye anadai alikiri kuhusika na tukio hilo kwa sababu mke wake amekataa kwenda Uganda.

Amesema asubuhi polisi walimchukua kwa hatua zaidi.

Mkazi wa Kijiji cha Magoma, Tulakila Twijuke amesema akiwa amelala nyumbani kwake alisikia mtu akigonga mlango alipouliza ni nani anagonga akajibiwa “Inzze Innocent Nsaaba obuyambi” (yaani mimi Innocent naomba msaada wa chakula na kulala hapa).

Amesema alikaa muda kidogo kisha akafungua mlango akamuona kijana anayekadiriwa kuwa na miaka 25 au 26 akiwa amevaa kofia ya nguo na koti jeusi lililo chafu. Amesema alimpatia maji ya kunywa na chakula kisha akamuonyesha sehemu ya kupumzika.

“Nilipomchunguza nikaona kwenye mfuko wa koti alikuwa na kitambulisho cha nchini Uganda na mihogo mibichi, huku nguo zake zikiwa zimelowa maji ya umande,” amesema.

Amedai alipomuuliza baada ya mazishi alikwenda wapi alimjibu alijificha vichakani akidai anaogopa kuonekana kwa kuwa alikuwa na mpango wa kumkomesha mke wake.

Amedai alimweleza yeye ndiye amefukua kaburi la mtoto wake na kupeleka jeneza kwenye mlango wa nyumba ya babu yake, akidai alifanya hivyo kwa hasira ya mke wake kukataa kwenda naye Uganda.

Related Posts