WAKULIMA wa Mkoa wa Ruvuma wamepongezwa kwa kuwa werevu wa kufuata sayansi ya kilimo katika uzalishaji wa mazao.
Kauli hiyo imetolewa na Waziri wa Kilimo, Mhe. Hussein Bashe (Mb) wakati akizungumza kwenye Mkutano wa hadhara tarehe 19 Septemba 2024 baada ya kukagua Kituo cha Kuuzia Mahindi cha Mtyangimbole, Wilaya ya Songea, Mkoani Ruvuma. Vile vile, Waziri Bashe ametembelea Kituo cha Ununuzi wa Mahindi cha Madaba kwenye Kata ya Mahanje.
Aidha, amewaahidi wakulima hao kuwa watapatiwa elimu ya kilimo cha kisasa, kujengewa Kituo cha Zana za Kilimo kitakachokuwa na huduma za matrekta, pawatila, mashine ya kupandia, mbegu na mbolea za ruzuku ambacho kitahudumia wakazi wa maeneo ya Ngumbila, Mtyangiambole na Mkungatema.
“Tumefarijika ujio wako ambao kero zetu umetumalizia. Shukran hizi tunaomba zimfikie Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan,” amesema Mkulima Aston Mwamsatu. Naye Mkulima Peter Komba amemuomba Waziri Bashe kusaidia kuwasiliana na Sekta husika ili watatue tatizo la kutokuwa na umeme kwenye eneo la Kituo cha Ununuzi wa Nafaka cha Mtyangimbole.
Kwa upande wake, Waziri Bashe amewaeleza wakulima kuwa kuanzia mwaka kesho, vituo vyote vya ununuzi wa mazao chini ya Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) vitawekewa mashine za kuchambua mahindi ili kuondokana na kuchambua kwa mikono. “Mbegu za ruzuku pia tunawaletea pamoja na mbolea za ruzuku ili kuongeza tija katika uzalishaji wa mazao yenu,” amesema Waziri Bashe.
Amewaomba wakulima waanze utaratibu wa kuhifadhi mahindi mabovu ili soko likipatikana nayo yaweze kuuzwa kwa matumizi ya kulisha mifugo, huku yakipunguza hasara kwa mkulima. Wakulima wameeleza kuwa kwa kila gunia la kilo 120 kunaweza kuwa na mahindi mabovu takribani magunia 10 hadi 30.
Aidha, kwenye Kituo cha Madaba, Waziri Bashe ameielekeza Mamlaka ya Taifa ya Hifadhi ya Chakula (NFRA) kuongeza watumishi na mizani ya kidigitali ili kurahisisha zoezi la ununuzi kwa wakulima. Pia amewahamasisha wakulima kuuza mahindi yao kwa Vituo vya NFRA ili wapate shilingi 700 kwa kilo, kuepuka madalali wanaonunua mahindi vijini kwa shilingi 300 hadi 350 au chini ya shilingi 600.