DC Shaka awaonya wanaojichukulia Sheria mkononi.

Mkuu wa Wilaya ya Kilosa Shaka Hamdu Shaka ambaye ni mwenyekiti wa kamati ya Usalama wa Wilaya hiyo amewataka wananchi kuacha kujichukulia Sheria mkononi badala yake wafuate utaratibu wa kufikisha changamoto zao kwenye mamlaka husika ili zipatiwe ufumbuzi.

DC Shaka ameyasema hayo wakati akizungunza na wananchi wa Kijiji cha Dumbalume kilichopo Kata ya Berega baada ya kuwepo kwa taarifa za wananchi kutaka kumvamia mmoja wa wakazi wa eneo hilo anayedaiwa kuvamia eneo la hifadhi ya Kijiji na kujimilikisha ekari zaidi ya 230 kinyume na utaratibu.

DC Shaka ametoa onyo Kwa wananchi katika Kijiji hicho na wilaya kwa ujumla kuacha tabia hiyo ya kujichukulia Sheria mkononi na kufanya maamuzi ambayo yanaweza kuhatarisha usalama wa Watu na nchi kwa ujumla.

“Hata kama mtu awe maarufu kiasi gani, awe ana pesa kiasi gani hata kama anajuana na viongozi wa juu , Serikali haitasita kumchukulia hatua yoyote anatakaye bainika kushawishi au kujichukulia Sheria mkononi”

Amesema changamoto zote zinatakiwa zifikishwe Kwa viongozi wa Kijiji, kata na badae Wilaya kama zitakua Bado hazijapatiwa ufumbuzi lakini sio kufunga Barabara, kufunga huduma za kijamii au jambo lolote linaloweza kusababisha kero Kwa Watu wengine.

Kwa upande wake mkuu wa polisi Wilaya ya Kilosa (OCD) Mrakibu mwandamizi wa polisi ( SSP) Samweli Kijanga amesema ni vyema wananchi wakiendelea kuitunza amani iliyopo ili waweze kufanya shughuli za uzalishaji Mali.

Amesema Sehemu yoyote ambayo haina amani hakuna maendeleo hivyo Jeshi la polisi linasisitiza wananchi kushiriki katika Ulinzi na Usalama wa maeneo yao.

Aidha amesisitiza suala la wananchi kushirikiana na polisi kata kwa kutoa taarifa sahihi za uhalifu na wahalifu ili matukio hayo yaweze kudhibitiwa.

Naye Rosemary Mlama mkazi wa kijiji cha Dumbalume amesema wanawake na watoto ndio wanakuwa wahanga wakubwa wa matukio ya kujichukulia Sheria mkononi hivyo amewataka wananchi kuacha kufanya vitendo hivyo.

Related Posts