Kigoma. Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk Doto Biteko ameliagiza Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), kuhakikisha Mkoa wa Kigoma unaunganishwa kwenye gridi ya Taifa ifikapo mwisho mwa mwaka 2024.
Amesema lengo kuu ni kutaka kuondokana na utegemezi wa umeme unaotokana na mafuta mazito.
Agizo hilo amelitoa leo Alhamisi Septemba 19, 2024, kwenye hafla ya uwekaji wa jiwe la msingi ujenzi wa miradi ya uzalishaji na usafirishaji umeme katika Mto Malagarasi (49.5 MW), na ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme wa kV132 kutoka Igamba hadi Kidahwe mkoani Kigoma.
Dk Biteko amesema Serikali inatumia Sh35 bilioni kila mwaka kununua mafuta kwa ajili ya majenereta, wakati makusanyo ya shirika kwa Mkoa wa Kigoma yanafikia Sh16 bilioni, hali inayosababisha hasara.
Amesema hatua ya kuzima majenereta hayo itachukuliwa katika mikoa mingine ambayo bado haijaunganishwa na umeme wa gridi.
“Miradi hii sasa inakwenda kuiweka Kigoma katika historia ya kupata umeme wa uhakika, kwa kuwa sasa itapata umeme kutoka vyanzo mbalimbali ikiwemo Nyakanazi na Malagarasi,” amesema Dk Biteko.
Pia, amesisitiza kuwa vijiji vyote vya Kigoma vitapata umeme kabla ya mwaka huu kumalizika.
Katika kuunga mkono juhudi za wananchi wa Kidahwe, Naibu Waziri Mkuu huyo ametoa mifuko 500 ya saruji kwa ajili ya ujenzi wa kituo cha afya, huku akiahidi kujenga kituo kingine cha afya.
Akizungumzia ujenzi wa barabara, amewaahidi wananchi kuwa Serikali itajenga barabara ya lami ya kilometa 20 katika kijiji cha Igamba.
Awali, Mkurugenzi Mtendaji wa Tanesco, Mhandisi Gissima Nyamo-Hanga alisema lengo la Mradi wa Umeme wa Malagarasi ni kuimarisha hali ya usambazaji wa umeme katika Mkoa wa Kigoma na wilaya zake.
Amesema hatua hiyo itasaidia kupunguza gharama za uzalishaji wa umeme na kwa sasa baadhi ya wilaya za Mkoa wa Kigoma zinategemea umeme unaozalishwa kwa gharama kubwa kupitia jenereta zinazotumia mafuta ya dizeli kutoka mitambo ya Tanesco iliyopo Kigoma Mjini. “Hali hii inasababisha kuongezeka kwa gharama za uendeshaji wa shirika,” amesema Mkurugenzi mtendaji huyo.
Ametaja gharama za jumla katika mradi wa Malagarasi kuwa ni Dola144.14 milioni za Marekani (Sh398 bilioni) na Serikali ya Tanzania inagharamia Dola 4.14 milioni za Marekani na Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) inagharamia Dola 140 milioni za Marekani.
Nyamo-Hanga amesema mradi wa bwawa na kituo cha kuzalisha umeme, unajengwa na mkandarasi Dongfang Electric International Corporation kutoka China na ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme ya kV132 Igamba-Kidahwe (km 54), unajengwa na mkandarasi Shyama Power India Limited kutoka nchini India.
“Mradi pia utasambaza umeme kwenye vijiji saba na kaya 750 zitaunganishiwa umeme,” amesema Nyamo-Hanga.
Amesema mradi huo pia utatoa ajira kwa zaidi ya wafanyakazi 700 na kuchochea biashara ya umeme kikanda.
Naye Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Felchesmi Mramba amesema Mkoa wa Kigoma sasa utaunganishwa na gridi ya Taifa kupitia njia saba za umeme.
Alisisitiza kuwa mradi huo utaifanya Kigoma kuwa kitovu cha umeme nchini, huku Wilaya zake zikifaidika na upatikanaji wa umeme wa uhakika.
Naibu Waziri wa Tamisemi, Zainabu Katimba amesema Mkoa wa Kigoma umepokea Sh11.5 trilioni kwa ajili ya miradi ya maendeleo.
Amesema miradi hiyo inajumuisha sekta ya nishati, ambayo imepokea zaidi ya Sh1.2 trilioni kwa mwaka wa fedha 2024/2025.
Pamoja na hayo, Katimba amewahimiza wananchi kufuatilia ratiba za uchaguzi wa Serikali za Mitaa na kuwachagua viongozi wenye uwezo wa kuleta maendeleo.
Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Thobias Andengenye amemshukuru Rais Samia kwa kutekeleza miradi mikubwa ya maendeleo, ikiwa ni utekelezaji wa ahadi yake ya kuufungua Mkoa wa Kigoma na kuufanya kitovu cha uchumi. Amesema mkoa utaendelea kusimamia kwa umakini fedha zinazotolewa ili kufikia malengo yaliyokusudiwa.
Mradi wa Malagarasi unagharimu dola za Marekani milioni 144.14, ambapo Serikali ya Tanzania inagharamia dola milioni 4.14, huku sehemu kubwa ya gharama ikifadhiliwa na Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB). Mradi huu utachangia upatikanaji wa umeme katika vijiji saba na kaya 750 zitaunganishiwa umeme.