Dar es Salaam. Kama ulidhani kuzaliwa kwako na baba na mama kunakupa uhalali usio na shaka wa kurithi mali walizonazo unakosea, lipo takwa la kisheria linalokuondolea haki hiyo, ingawa mwenye mali ni baba au mama yako wa damu.
Pengine huu unaweza kuwa ukweli mchungu kwa baadhi ya warithi, kutokana na uhalisia wa matukio kadhaa ya ugomvi wa mali za urithi yanayozikabili familia mbalimbali na wengine kufikia hatua ya kukatizana uhai.
Mfano wa hayo ni familia ya Bwire Mathayo ya Kibaha mkoani Pwani, iliyoingia kwenye mzozo wa mirathi, baada ya mama yao kufariki dunia na kuacha mali.
Mzozo huo umetokana na wakubwa kugoma kuwaingiza wadogo zao kwenye mirathi, wakidai hawastahili kwa kuwa mali hizo zilichumwa na baba yao.
Katika familia hiyo, Justine Zuberi alidai baba aliyefariki dunia, ndiye mmiliki wa mali hizo na si baba yao wa kambo (Bwire Mathayo) aliyemuoa mama yao na kumkuta na mali alizoachiwa na baba yao.
Mama yao huyo alifariki dunia Desemba 2023 na kuacha watoto wanne, lakini kwa baba wawili tofauti.
Binti mdogo, Sabrina Mathayo anasema mgogoro huo umeigawa familia, haina maelewano, baadhi ya wanandugu wanaamini watoto wote wana haki ya kupata urithi kwa mama yao, kwani wote ni watoto wa marehemu na wengine wanapinga.
Mkasa mwingine unaikabili familia mjini Morogoro, baada ya baba kufariki dunia, mmoja wa watoto wake aliingia kwenye mgogoro na wenzake akipinga kuenguliwa kwenye mirathi.
Kijana huyo, Deniss Joachim (sio jina lake halisi) anataka kuwa mmoja wa warithi, ndugu zake wanagoma wakisisitiza baba yao akiwa hai alimuengua kwenye warithi wake na wosia aliouacha umebainisha hilo.
Kama hiyo haitoshi, Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Anthony Mtaka alieleza mgogoro wa mirathi wa watoto wa familia moja mkoani humo waliokwenda ofisini kwake kutaka usuluhishi.
Katika mgogoro huo, watoto wadogo watatu walipinga wakubwa zao wawili kuwa wasimamizi wa mirathi, wakitoa hoja kuwa ndugu zao hawakutaka baba yao apelekwe hospitali alipougua, iweje afariki dunia ndiyo wawe wasiwamizi wa mirathi yake.
Katika simulizi hiyo, Mtaka alisema wale wadogo walipoulizwa kwanini hawataki kaka zao wasimamie mirathi, wakasema baba yao alipata kiharusi, waliposhauri apelekwe Muhimbili (Hospital ya Taifa jijini Dar es Salaam), wale wakubwa walikataa wakidai mzazi wao huyo anaweza kufa muda wowote.
“Alikaa kwenye hali ya ugonjwa mwaka mmoja na miezi minne na kufariki, mvutano ulikuwa wadogo hawataki kaka zao kuwa wasimamizi wa mirathi, wakitoa hoja kwamba ndugu zao walikataa baba yao asipelekwe Muhimbili kwa matibabu zaidi, wakati pesa ambazo zingetumika zilikuwa zake, wakidai walitaka afe ili wagawane fedha za baba yao zikiwa nyingi.
“Wakubwa nilipowauliza wakasema mzee wao alikuwa amefikia kwenye koma, hivyo huenda angefia njiani, lakini swali la kujiuliza hata kama wangechukua ambulance wakalipa milioni 80, hela ni ya mgonjwa mwenyewe,” alisema Mtaka.
Akizungumzia sintofahamu hiyo, Ofisa Usajili wa Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (Rita), Joseph Mwakatobe anasema kuna vigezo vinavyomuondoa mtoto kwenye mirathi iwe baba/mama yake aliacha wosia au la.
“Kwa aliyeacha wosia, mwenye mali anaweza asimrithishe mtoto wake, lakini ni lazima amtaje kuwa ni miongoni mwa watoto wake na sababu za kutomuweka kwenye orodha ya warithi wake na ziwe na ushahidi,” anasema.
Kwa ambaye hakuacha wosia, anasema lazima kuwepo na mashahidi wasiopungua wanne kuthibitisha hilo kuwa mtoto husika hastahili kurithi na Mahakama itaviangalia kama vya msingi.
Kinachomuondolea mtoto uhalali wa kurithi
Pamoja na sababu nyingine, hatua ya kuzini na mke au mume na muandika wosia ni moja ya vigezo vinavyomwondolea mtoto haki ya kurithi.
“Hilo likithibitika, linamuondoa mtoto huyo katika haki hiyo kwa kuwa ni mkosefu wa maadili,” anasema.
Kama wewe ni mtoto na unaharibu mali za mzazi wako, hesabu hiyo ni moja ya sababu zinazokuondolea sifa ya kurithi kwa mujibu wa Mwakatobe.
“Mali aliyoharibu ndiyo itahesabika kuwa ni urithi wake, mzazi akiandika au hata kutamka na ndugu jamaa wakawa wanafahamu, hiyo ni moja ya vigezo vinavyomuondoa huyo mtoto katika mirathi,” anasema.
Lakini, ukishindwa kutoa huduma kwa mzazi wao angali hai, anasema ni sababu nyingine inayokuondolea sifa ya kumrithi.
“Ni kweli huyo mwanao ni mrithi wako, lakini hakukujali labda wakati unaumwa, hiyo inapelekea dhana kwamba pengine anataka ufe ili arithi, na baadhi ya mifano ipo watoto wengine huwaombea mabaya wazazi wao, ili tu warithi mali, kigezo hicho kikiwa na ushahidi kinakuondoa kwenye mirithi,” anasema.
Lakini, anasema mtoto anaweza kupinga mahakamani kama mzazi ameacha wosia na Mahakama itaangalia kama vigezo vilizingatiwa.
Mama mwenye watoto wa baba tofauti
Akifafanua mirathi ya watoto waliochangia mama, Mwakatobe anasema kama mume wa kwanza wa mama huyo alipofariki dunia ulifanyika mgao na kila mmoja (mke na watoto), mama huyo akifariki watoto na mume wake mpya atakuwa na haki ya kumrithi.
“Kama mgao ulifanyika mume wake wa kwanza alipofariki, inamaanisha watoto wakubwa tayari walishapata mgao wao, na kama haukufanyika mali zote zikaenda kwa mama hiyo ni utaratibu anapaswa kufanya mgao bila kuangalia alizaa na nani.
“Mwakatobe anasema kuna migogoro watoto wakubwa wanadai mali alichuma baba yao, lakini kama mali hizo ziligawanywa baba wa kwanza alipofariki, kisha baadaye mama akaolewa na kuzaa, ikitokea huyo mama amefariki wote ni uzao wa tumbo lake na kila mtoto anastahili kurithi na hata huyo mume aliyekuwa amemuoa naye anastahili,” anasema.
Anasema huyo mama akiwa na hekima atawaweka wazi mapema kuhusu mali zake na kueleza hizo mali alichuma na baba gani na warithi wake ni watoto wake na wale wa baba mwingine ataangalia baba yao na mali zao.
“Kama hakufanya hivyo, hakuacha wosia na hakuna maandishi na nyaraka, basi vyote vinakwenda kwa wale warithi wake hata mume aliyekuwa amemuoa anaweza kurithi, kwani anapofariki mwenye mali zake, mali zitangukia kwa warithi wake,” anasema.
Wajukuu wanaweza kurithi?
Mwakatobe anasema katika sheria wanaopaswa kurithi ni wale walioachwa na marehemu, mke, mume, wazazi au watoto.
“Kama watoto wa huyo marehemu walitangulia kabla ya baba yao, lakini nao wameacha watoto (wajukuu wa marehemu) hao hawana nafasi labda kama awe aliacha wosia na kuwaandika kwenye mirathi.
“Kinyume na hapo, hao wajukuu tunasema baba au mama yao alikimbia urithi, kwa sababu walifariki kabla ya mwenye mali na ikitokea wamepata basi ni busara tu inatumika kwenye familia,” anasema.
Unavyoweza kuandika Wosia
Mwakatobe anasema, ili kuandika wosia unakwenda Rita kwanza ukiwa peke yako.
“Haihitaji kitu kingine zaidi ya kuja wewe kama wewe, tutakuelekeza, utaandika mali zako na sisi tutakupangia tarehe ambayo utakuja na mashahidi wawili, ili kuandika wosia,” anasema.
Hata hivyo, Mwakatobe anasema kitu cha muhimu ambacho watu wanapaswa kukifahamu ni kwamba kuandika wosia inaweza isiwe kigezo cha usimamizi wa mirathi yako pale unapokuwa umefariki endapo wosia utakosa vigezo.
“Hii imekua ikileta shida, unaweza kujiuliza inakuwaje Mahakama imekataa wosia na marehemu aliuandika akiwa hai? Ndiyo anaweza kuwa ameandika, lakini haujakidhi vigezo, sisi Rita kabla ya kuandika tunakupa elimu kwanza,” anasema.
Anasema kwenye wosia mbali na mali, unaandika pia madeni na lazima uwaorodheshe watoto wako na kama miongoni mwao yupo ambaye humpi urithi na ueleze sababu na umtaje msimamizi wa mirathi.
“Unapokuja kuandika wosia uthibitisho wa mali zako unao mwenyewe, Rita tunachohitaji ni taarifa na taarifa yako anakua nayo kichwani, kama una vitu vingi, tunakwambia kaa tulia andika summary ya vitu vyako.
“Wosia unaweza kukosa vigezo, kama muandikaji ameandika si kwa hiari yake, kwani kuna watoto huwa wanalazimisha baba aandike, kisa labda kaoa mke mwingine halafu wanaona hizo mali zilichumwa na mama yao,” anaeleza.
Anasema kigezo cha kwanza katika kuandika wosia lazima uwe na hiari nao, pili ni utimilifu wa akili ukijua kile unachoandika na unakikumbuka.
“Pia uwe na mashahidi wasiopungua wawili na lazima uchapwe, usifutwe futwe na kilichoandikwa kisilete utata na usainiwe na muandikaji na mashahidi siku moja na uthibitishwe,” anasema.
Anasema kwenye wosia shahidi anaweza kufariki dunia kabla ya mwenye mali, hivyo wosia unaweza kubadilika mara kwa mara kulingana na uhitaji uliopo.
Kwa mujibu wa Mwakatobe, gharama za kuandika wosia zinaanzia Sh30,000 na kuuhifadhi ni Sh30,000 kwa mali isiyozidi Sh50 milioni.
Kuanzia mali za Sh50 milioni hadi Sh500 milioni kuandika ni Sh100,000 na kuuhifadhi ni Sh100,000.
Kwa mali ya kuanzia Sh500 milioni na zaidi kuandika ni Sh150,000 na kuuhifadhi ni Sh150,000.
“Mali hizo huwa tunazifanyia makadirio na kutathimini kulingana na mazingira,” anasema.