‘Hospitali’ ya Cradle yafikishwa kortini madai kifo cha pacha wa kupandikizwa

Dar es Salaam. Kituo cha Afya cha Cradle (Cradle Speciality Heath Centre), kilichopo Msasani, jijini Dar es Salaam kimeburuzwa mahakamani kikidaiwa fidia ya zaidi ya Sh3.6 bilioni kwa madai ya uzembe uliosababisha kifo cha mmoja wa watoto pacha waliozaliwa hapo kwa njia ya upasuaji.

Kesi hiyo imefunguliwa Mahakama Kuu Masjala Ndogo Dar es Salaam na Julieth Baigana (49), mama wa kichanga hicho kilichofariki, huku pacha aliyesalia  Glory Narcis Lubamba amefungua kesi akiwakilishwa na baba yake, Narcis Lubamba.

Mbali na kituo hicho cha afya, mdaiwa mwingine katika kesi hiyo ya madai namba 11691/2024 ni daktari wa kituo hicho, Vindhya Pathirana aliyemuhudumia wakati wa kujifungua pacha hao. 

Julieth anadai pacha wake hao ndio walikuwa watoto pekee ambao aliwatafuta na kuwapata kupitia Huduma ya Upandikizaji Mimba (IVF), kwa gharama kubwa, baada ya kutafuta ujauzito kwa muda mrefu kwa njia ya kawaida bila mafanikio.

Anadai lakini alimpoteza mtoto wake huyo mmoja, kutokana na kufanyiwa huduma ya upasuaji katika kituo hicho wakati hakina vifaa wala huduma kwa ajili au watoto wanaozaliwa kabla ya wakati (njiti).

Akizungumza na Mwananchi jana Jumanne, Septemba 17, 2024 kuhusu kesi hiyo, Wakili wa mdai, Deogratias Butawantemi amesema kesi hiyo inayosikilizwa na Jaji Butamo Philip, mara ya mwisho ilitajwa Septemba 4, 2024, imepangwa kuanza kusikilizwa Septemba 26, 2024.

Butawantemi amesema kesi hiyo ilifunguliwa na kusajiliwa Mei 20, 2024 na  ilipotajwa mara tatu zote za mwanzo mfululizo wadaiwa hawajawahi kufika mahakamani.

Kutoka na hali hiyo amesema, waliwasilisha maombi mahakamani hapo akiomba Mahakama itoe wito wa kuwatangaza gazetini ili kufika, ombi ambalo Jaji Philip alikubaliana nalo.

Hivyo walitoa wito kwa wadaiwa kupitia gazeti la Mwananchi na The Citizen ya Agosti 27, 2024, wakitakiwa kufika mahakamani hapo Septemba 4, 2024, na kuwasilisha maelezo ya majibu ya madai hayo pamoja na vielelezo wanavyotarajia kuvitumia katika utetezi wao.

Kutokana na wito huo wa tangazo la gazetini, tarehe hiyo wadaiwa hao ambao wanatetewa na mawakili Steven Bwana na Anna Amon, walifika mahakamani na waliamuriwa kuwasilisha majibu yao ya utetezi kwa maandishi kabla ya tarehe hiyo ya kuanza usikilizwaji, Septemba 26.

Simulizi ya msingi wa kesi

Kwa mujibu wa hati ya madai ya kesi hiyo, Julieth alikuwa na ujauzito wa kupandikizwa, huduma aliyofanyiwa katika Kituo cha huduma hizo jijini Nairobi, Nairobi IVF Centre Limited na alikuwa anatarajia kujifungua watoto wawili.

Ujauzito wa watoto hao pacha ulithibitishwa na mdaiwa wa kwanza Dk Pathirana, Septemba 15, 2023, wakati Julieth alipokwenda kituoni hapo kwa ajili ya huduma za uzazi na matibabu mengine.

Hivyo alisajiliwa kituoni hapo na kukabidhiwa kwa Dk Pathirana, ambaye ni bingwa wa masuala ya uzazi na magonjwa ya wanawake.

Kutokana na tathimini aliyoifanya daktari huyo alisema tarehe ya matarajio ya kujifungua ingekuwa Machi 24, 2024, kwa kuzingatia tarehe ya mwisho kuona siku zake ambayo ilikuwa Agosti 3, 2023.

Baada ya vipimo hivyo, Julieth aliendelea na huduma za kliniki ya uzazi katika kituo hicho chini ya Dk Pathirana ambaye kutokana na uchunguzi wa maendeleo ya ujauzito wake kwa muda wote alikuwa akimweleza ulikuwa unaendelea vizuri.

Hata hivyo, Februari 11, 2024, asubuhi, wakati akiwa nyumbani kwake Kijichi, Julieth alijisikia vibaya, hivyo alimpigia simu Dk Pathirana akamuelezea hali ambapo  alimtaka awahi kituoni hapo, kwa ajili ya uchunguzi zaidi na huduma nyingine muhimu za matibabu kutokana na  hali yake.

Kituoni hapo, Dk Pathirana alipendekeza afanyiwe huduma ya kujifungua wakati akijua kuwa ujauzito huo ulikuwa ni wa miezi saba, hivyo watoto hao wangezaliwa wakiwa njiti.

Hivyo Julieth alijifungua watoto wawili kwa upasuaji, huduma iliyofanywa na Dk Pathirana, bila kuwepo vifaa ambavyo vingewawezesha kuhimili mazingira mapya kulingana na umri wao.

Baada ya kuzaliwa, watoto hao walipambania maisha yao bila msaada wowote kutokana na kutokuwepo kwa kitengo chenye vifaa vya kuwawezesha kuzoea mazingira, kwa muda wa saa 8 kabla ya mwingine kuhamishiwa katika hospitali ya Aga Khan.

Lakini kutokana na kukosa huduma hizo na uangalizi wa karibu wa kitabibu hatimaye mtoto mmoja alifariki dunia, huku mtoto wa pili naye akisalia katika changamoto za kiafya zilizoathiri ukuaji wake.

Malalamiko dhidi ya wadaiwa

Hivyo wadai wanadai, Dk Pathirana alikuwa anajua amefungiwa na Baraza la Madaktari Tanganyika kutoa huduma za kitabibu, lakini aliamua kufanya huduma ya kujifungua kwa upasuaji kwa Julieth ulisababisha kifo cha mtoto mmoja na kumsababishia Julieth madhara ya maambukizi katika majeraha.

Pia wanakilalamikia kituo hicho licha ya kuwa na wajibu katika kulinda afya za wadaiwa, kiliruhusu vifaa vyake kutumiwa na mwajiriwa wake huyo Dk Pathirana kutoa huduma za kitabibu isivyo halali kama daktari bingwa wa uzazi na magonjwa ya wanawake, wakati kikijua kuwa alikuwa amefungiwa.

Pia wadai wanawalalamikia wadaiwa kwa kupendekeza kupata huduma hiyo ya kujifungua katika kituo hicho ambacho hakikuwa na uwezo wa kuwahudumia watoto hao njiti na kutokana na kushindwa kusimamia huduma za kiafya kwa watoto wa aina hiyo, kulisababisha kifo cha mtoto mmoja.

Hivyo wanadai kutokana na vitendo na mwenendo huo wa wadaiwa, wadai wameathirika, wamejeruhiwa na kupata madhara mbalimbali.

Madhara hayo ni pamoja na maradhi ya afya ya akili kama matokeo ya upasuaji huo hasa kwa kufanyiwa huduma za kitabibu na daktari aliyepigwa marufuku, na kumsababishia maumivu yasiyoponyeka na kutendewa unyama.

Majeraha yaliyotokana na upasuaji huo ambayo yalipata maambukizi, yaliyomfanya Julieth alazwe chumba cha wagonjwa mahututi kwa takribani mwezi mmoja.

Kifo cha mtoto wake wa thamani aliyetarajiwa, kusubiriwa na aliyepatikana kwa gharama kubwa na kwa utaratibu wenye maumivu, yaani upandikizaji.

Maumivu ya kisaikolojia kwa ukatili alilotendewa Julieth kwa matendo ya wadaiwa kwa tukio hilo la Februari 24, 2024

Maumivu ya kimwili kutokana na maambukizi yaliyotokana na upasuaji huo yaliyowasababishia gharama zaidi za matibabu zisizo za lazima, yeye Julieth na pacha wake aliyesalia.

Matatizo ya kifedha yaliyosababishwa na gharama alizozitumia na anazotarajia kuzitumia baadaye kwa madhara ya kudumu aliyoyapata yaliyolazimishwa na wadaiwa.

Kutokana na madhara hayo anayodai yalitokana na upasuaji huo na katika kituo hicho ambacho hakikuwa na vifaa kwa ajili ya watoto hao na hatimaye kusababisha kupoteza uhai wa mtoto wake mmoja, Julieth anaiomba Mahakama iwaamuru wadaiwa wamlipe fidia ya Sh3.63 bilioni.

Malipo hayo yanajumuisha fidia ya kituo hicho kukiuka wajibu wake wa kulinda afya za wadai kwa kulazimisha matibabu yenye utata, Sh1.5 bilioni, Dk Pathirana kukiuka wajibu wake na kusababisha kifo cha mtoto huyo, Sh1 bilioni, fidia ya adhabu Sh300 milioni, fidia ya madhara ya jumla Sh200 milioni.

Malipo mengine ni ya gharama za matibabu na huduma mbalimbali za kitabibu alizozitumia kutokana na madhara yaliyojitokeza kutokana na huduma ya upasuaji huo na kujifungua watoto njiti mahali ambapo hakuna huduma Sh 450 milioni.

Vilevile anaiomba Mahakama hiyo iwaamuru wadaiwa wamlipe riba ya malipo hayo.

Kuhusu Dk Pathirana kufungiwa 

Dk Pathirana  alifungiwa kutoa huduma kwa muda wa miaka miwili na Baraza la Madaktari Tanganyika (MCT), baada ya kupatikana na hatia ya ukiukwaji wa kanuni za maadili na utendaji wa kitaaluma.

Mbali na kumfungia kwa muda huo, MCT lilimuelekeza Dk Vindhya kwenda kwenye mafunzo ya weledi, maadili ya kitaaluma na huduma kwa wateja katika hospitali ya kufundishia kwa muda wa mwaka mmoja kwa gharama zake, kabla ya kurudishwa kutoa huduma baada ya muda wa kutumikia adhabu utakapoisha.

Uamuzi wa kufungiwa kwake kujihusisha na utoaji huduma za kitabibu ulitolewa Februari 10, 2024 na Mwenyekiti wa Baraza hilo, Profesa David Ngassapa baada MCT kusikiliza mashauri tisa kati ya Januari 22 hadi Januari 26, 2026.

Dk Pathirana na wenzake watano kutoka katika vituo mbalimbali vya kutolea huduma za afya, walifungiwa leseni zao kutokana na sababu mbalimbali zilizoanishwa na baraza hilo zikiwemo za ukiukwaji wa kanuni za maadili na utendaji wa kitaaluma.

Ukiukwaji huo ulielezwa kuwa ulichangia madhara kwa wagonjwa, ikiwemo kupata ulemavu na vifo.

Dk Pathirana alitiwa hatiani baada ya kumzidishia mgonjwa dawa aina ya Methotrexate licha ya kushauriwa.

Pia alizuia mgonjwa kupatiwa rufaa kwa wakati alipozidiwa, hivyo kusababisha kifo.

Related Posts