Kanisa Anglikana lawapinga Askofu Mokiwa, wenzake wasitoe ushahidi mahakamani

Dar es Salaam. Bodi ya Wadhamini wa Kanisa la Angikana Tanzania pamoja na Askofu Jackson Sostenes wa Dayosisi ya Dar es Salaam, wamewasilisha pingamizi Mahakama Kuu Divisheni ya Ardhi, wakipinga mashahidi watano akiwemo aliyekuwa Askofu Mkuu wa Kanisa la Anglikana Dayosisi ya Dar es Salaam, Valentino Mokiwa, wasitoe ushahidi katika kesi ya ardhi iliyofunguliwa na Bernardo Sepeku.

Mbali na Mokiwa, mashahidi wengine wanaopingwa na kanisa hilo wasitoe ushahidi wao ni askofu wa Oscar Mnung’a wa Dayosisi ya Newala na John Mwamazi ambaye ni mchungaji mstaafu wa kanisa la Anglikana Dar es Salaam.

Wengine ni Blandina Sepeku (74), ambaye ni dada yake mkubwa na Bernardo pamoja na Abdallah Mtema ambaye ni mlinzi katika shamba lenye ukubwa wa ekari 20 lililopo Buza.

Bernado, ambaye ni mtoto wa marehemu John Sepeku aliyekuwa Askofu Mkuu wa kwanza wa Kanisa Anglikana Tanzania, Dayosisi ya Dar es Salaam, alifungua kesi hiyo ya ardhi namba 378/2023, akipinga kunyang’anywa zawadi ya kiwanja alichopewa baba yake mwaka 1978 na kanisa hilo.

Mtoto huyo alifungua kesi dhidi ya Bodi ya Wadhamini wa Kanisa Anglikana Tanzania, Askofu Jackson Sostenes wa Dayosisi ya Dar es Salaam na pamoja na Kampuni ya Xinrong Plastic Waste Industry Co Ltd.

Katika kesi hiyo, Bernardo anadai alipwe Sh3.72 bilioni ambayo ni fidia ya hasara ya kifedha iliyopatikana kutokana na uvamizi wa mali ya ardhi katika kiwanja hicho.

Pingamizi hilo limewasilishwa leo, Alhamisi Septemba 19, 2024 na wakili Dennis Malamba anayemtetea mdaiwa wa kwanza na wa wa pili katika kesi hiyo, wakati kesi hiyo ilipoitwa kwa ajili ya usikilizwaji.

Wakili Malamba amewasilisha pingamizi hilo mbele ya Jaji Arafa Msafiri anayesikiliza shauri hilo, ambapo anapinga mashahidi watano kati ya 10 wanatarajia kutoa ushahidi wasitoe ushahidi katika kesi hiyo.

Katika pingamizi hilo, Wakili Malamba amedai viapo vya mashahidi wao watano vina kasoro za kisheria kwa sababu mashahidi hao wakati wanaapa hawakusema wameapa wapi na wala viapo vyao havionyeshi wameapa tarehe gani.

“Mheshimiwa Jaji, kama mashahidi hawa watano tuliwataja hawakuapa wapi wala kuweka tarehe, hivi viapo vinakuwa havina nguvu kisheria,” amedai.

Amedai anaomba mahakama mashahidi hao wasitoe ushahidi wao katika kesi hiyo kwa sababu viapo vyao vinakinzana kisheria na kwamba walikosea kuapa kulingana na sheria ya viapo.

Akijibu madai hayo, wakili wa Bernardo, Deogratias Butawantemi akishirikiana na Gwamaka Sekela, amedai wao wameapa kwa usahihi kulingana na taratibu za kuleta ushahidi.

“Mheshimiwa Jaji, sisi tumefuata sheria kwa mujibu wa Tangazo la Serikali namba 761 la mwaka 2021 ambalo limetoa muongozo wa namna ya kujaza ushahidi wa maandishi,” amedai wakili Butawantemi.

Mutawantemi amedai mleta pingamizi alidai mashahidi hao walitakiwa watumie sheria ya viapo.

“Mheshimiwa Jaji, sheria ya viapo, kifungu namba 101 inampa mamlaka Jaji Mkuu kuweza kutoa namna gani ya kutoa muongozo katika sheria ya mwenendo wa mashauri ya madai,” amedai Butawantemi.

Pia amedai tangazo la Serikali namba 355 la mwaka 2022 linatoa fomu na utaratibu wa kuweza kutumia kwa wakati unajaza maelezo ya shahidi ambaye atakuja kutoa mahakamani katika kesi za madai, ambapo wadaawa waliamua kutumia maelezo ya mashahidi baada ya kufanya kwa mdomo.

Hivyo Butawantemi ameiomba mahakama itupilie mbali pingamizi la kanisa hilo na walipe gharama za usumbufu kwa kuwasumbua kwa kuwa tayari walikuwa na shahidi mmoja ambaye ni askofu Ascar Mnung’a wa Dayosisi ya Newala.

Jaji Msafiri baada ya kusikiliza hoja za pande zote, amesema atatoa umuzi wake Septemba 23, 2024 saa 5:00 asubuhi na kuendelea na usikilizwaji.

Awali, kabla ya kusikiliza pingamizi hilo, wakili Malamba aliomba majibu ya pingamizi hilo yawasilishwe kwa njia ya maandishi, ombi ambalo Jaji Msafiri alikataa na kutaka lisililizwe kwa njia ya mdomo ili kuokoa muda.

Mbali na mashahidi hao watano kuwekewa pingamizi, mashahidi wengine katika kesi hiyo ambao hawajawekewa pingamizi ni askofu Julius Lugendo wa Mbeya; Ernest Mwenewanda ambaye alikuwa ni mzee wa kanisa Kuu la Mtakatifu Albano; Bernado Sepeku; Edward Lwambano ambaye ni mfanyakazi wa kanisa hilo Dayosisi ya Dar es Salaam pamoja na Greogory Mwampute ambaye ni mtathmini aliyefanya tathimini kwenye kiwanja chenye ukubwa wa ekari 20 alichopewa baba yake Bernardo kama zawadi na kanisa hilo.

Katika kesi hiyo, Bernardo ambaye ni msimamizi wa mirathi ya baba yake, aliwasilisha maombi saba mahakamani hapo,  kwanza anapinga kunyang’anywa zawadi ya kiwanja namba 2689 chenye ukubwa wa ekari 20 kilichopo Buza Mtoni, wilayani Temeke ambacho anadai mwaka 1978, waumini na Wakristo wa dayosisi hiyo, walimpa Askofu Sepeku kama zawadi.

Pili, anaomba mahakama hiyo iamuru Bodi ya Wadhamini ya kanisa hilo, Askofu Sosthenes na Kampuni ya Xinrong Plastic Waste Industry Co Ltd kwa pamoja kulipa Sh33 milioni ikiwa ni hasara aliyoipata mlalamikaji kutokana na uharibifu wa mazao yaliyowekezwa katika shamba lililo ndani ya kiwanja hicho.

Mlalamikaji huo alidai mazao yaliyoharibiwa shambani ni pamoja na miti 200 ya malimao, miti 55 ya mikorosho, hekari mbili za mbaaza, hekari mbili za mihogo na hekari mbili za viazi vitamu.

Mazao mengine yaliyoharibiwa shambani hapo ni miti 30 za mapapai, minazi, miti 60 ya miembe, miti 25 ya michikichi pamoja na miti 45 ya minazi.

Tatu, Bernardo anadai alipwe Sh3.72 bilioni ambayo ni fidia ya hasara ya kifedha iliyopatikana kutokana na uvamizi wa mali ya ardhi iliyopo katika kiwanja hicho.

Nne, Mtoto huyo pia, anaiomba alipwe fidia ya Sh493.65 milioni ambayo ingepatikana baada ya kukomaa na mavuno ya mazao yaliyokuwepo kwenye shamba hilo.

Tano, anaomba Mahakama iamuru wadaiwa wote katika shauri hilo wamlipe mlalamikaji hasara ya jumla iliyopatikana.

Vilevile, mahakama hiyo iangalie unafuu mwingine wowote ambao itaona inafaa kutoa.

Pia, Bernado anaomba mahakama iamuru wadai hao walipe gharama za kuendesha kesi hiyo ya madai.

Inadaiwa kuwa Kanisa la Anglikana Tanzania kwa kushirikiana na Askofu wa Dayosisi ya Dar es salaam limechukua kiwanja hicho na kumpatia Kampuni ya Xinrong Plastic Waste Industry Co Ltd.

Related Posts