KOCHA Mkuu wa Stand United, ‘Chama la Wana’, Meja Mstaafu Abdul Mingange amesema mchezo wa kwanza ugenini dhidi ya Kiluvya United utampa ramani ya kikosi chake na uelekeo katika Ligi ya Championship inayoanza kesho Septemba 21.
Chama la Wana litaanzia ugenini keshokutwa (Jumapili) katika Uwanja wa Mabatini, Pwani dhidi ya Kiluvya United ya jijini Dar es Salaam kuanzia saa 10:00 jioni na Septemba 27 itarudi nyumbani Kambarage, Shinyanga kuikaribisha Transit Camp.
Akizungumzia utayari wa kikosi chake, Mingangee alisema wamefanya maandalizi ya kutosha, kupata mechi za kirafiki na kikosi chake kiko tayari kwa mashindano na kilichobaki na kuanza ligi katika mchezo wa kwanza utakaowapa picha ya msimu huu.
Alisema uongozi wa klabu kwa kushirikiana na mdhamini Jambo wameboresha huduma za malazi na chakula kambini kuwapa utulivu wachezaji.
“Nasubiri muda tuone mechi za kwanza zitakuaje japo mechi za mwanzo huwa ngumu. Nimejaribu kusajili wachezaji wazuri vijana wenye ari ya kucheza na tumefanya mazoezi ya kutosha pamoja na ujuzi wangu nilionao tutaona wachezaji watafanyaje,” alisema Mingange aliongeza;
“Japo mwezi mmoja au miwili haitoshi kutengeneza tiimu ya kutisha lakini kadri unavyokaa kwenye timu unagundua makosa ya wachezaji na kuyarekebisha, ukicheza mechi unapata uhalisia wa timu yako. Kwa hiyo ninapokaa na timu, mechi tutakazocheza na na uzoefu wangu tutajua nini kinapaswa kufanyika.”
Kocha huyo wa zamani wa Azam, Ndanda na Lipuli, aliipongeza Bodi ya Ligi (TPLB) kwa kupanga ratiba rafiki inayozingatia mazingira ya Tanzania na uchumi wa timu za Championship na kuzipa muda wa kujiandaa kati ya mechi moja hadi nyingine.