Dar es Salaam. Aliyekuwa ofisa wa Magereza, Josephat Mkama na wenzake wawili wamepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wakikabiliwa na makosa manne likiwamo la kughushi msamaha wa Rais kwa wafungwa.
Washtakiwa wengine katika kesi hiyo ni Sibuti Nyabuya na Joseph Mpangala.
Kesi hiyo inayosikilizwa na Hakimu Mkazi Mkuu Anna Magutu imetajwa mahakamani hapo leo Alhamisi Septemba 19, 2024.
Upande wa mashtaka umeieleza Mahakama kuwa umekamilisha upelelezi wa kesi hiyo.
Mwendesha mashtaka, Wakili wa Serikali, Winiwa Kasala ameiomba Mahakama ipange tarehe ya usikilizwaji wa awali ili washtakiwa wasomewe maelezo ya kesi.
Hakimu Magutu amekubali ombi hilo na kuahirisha kesi hiyo hadi Septemba 26, 2024 kwa ajili ya usikilizwaji wa awali.
Hakimu Magutu amewapa washtakiwa masharti ya dhamana likiwemo kuwa na wadhamini wawili wenye vitambulisho vya Taifa ambao watawasilisha mahakamani fedha taslimu au hati ya mali isiyohamishika yenye thamani ya Sh7.5 milioni. Walishindwa kukamilisha masharti ya dhamana.
Katika shtaka la kwanza wanakabiliwa na kosa la kuongoza genge la uhalifu, wakidaiwan kati ya Desemba Mosi, 2022 hadi Januari 30, 2023 jijini Dar es Salaam, kwa nia ovu, waliongoza genge la uharifu na kujipatia Sh45 milioni kutoka kwa wafungwa namba 585/2019 Song Lei, 205/2019 Xiu Fu Jie na 206/2016 Haung Quin.
Kosa la pili ni la kughushi barua ya msamaha wa Rais kwa wafungwa hao, ambalo linamkabili Mkama na mshtakiwa wa pili, Nyabuya.
Wanadaiwa Desemba 21, 2022 katika ofisi za Gereza la Ukonga waligushi barua yenye kichwa kilichosomeka ‘Nyongeza ya Msamaha kwa wafungwa katika kuadhimisha miaka 61 ya Uhuru’, ya Desemba 21 mwaka 2022.
Inadaiwa lengo la kughushi barua hiyo lilikuwa kuonyesha kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ametoa nyongeza ya msamaha kwa wafungwa hao, wakati wakijua si kweli.
Kosa la tatu ni la kuwasilisha nyaraka ya kughushi linalomkabili Mkama pekee.
Anadaiwa Desemba 27, 2022 katika ofisi za Gereza la Ukonga, Dar es Salaam aliwasilisha barua ya kugushi kwa Ofisa Tawala wa Gereza la Ukonga P7411 A/INSP Lusekelo Mwanjati.
Kosa la nne, washtakiwa wote wanadaiwa kujipatia pesa kwa njia ya udanganyifu.
Wanadaiwa kati ya Desemba Mosi mwaka 2022 hadi Januari 30, 2023 jijini Dar es Salaam, kwa lengo la kudanganya walijipatia Sh45 milioni kutoka kwa wafungwa hao.
Wanadaiwa walijipatia fedha hizo wakijifanya kuwa zitawezesha utekelezaji wa barua hiyo wakati wakijua si kweli.