Kopunovic aanza kujistukia Pamba | Mwanaspoti

WAKATI presha ya kutopata ushindi kwenye Ligi Kuu Bara ikizidi kuiandama Pamba Jiji, Kocha Mkuu, Goran Kopunovic amekiri huenda mbinu zake ndiyo tatizo huku akigoma kumtupia lawama yeyote na kuahidi kujitathmini na kutimiza wajibu wake ili kuwapa furaha mashabiki.

Timu hiyo ambayo haijapata ushindi chini ya kocha huyo tangu alipopewa majukumu Julai, mwaka huu akitokea Tabora United, Jumanne ilipata kichapo cha kwanza Ligi Kuu kwa kufungwa bao 1-0 na Singida Black Stars katika Uwanja wa CCM Kirumba, jijini Mwanza.

Katika mechi nne za Ligi Kuu msimu huu, Pamba Jiji imeambuliwa suluhu dhidi ya Azam FC, Dodoma Jiji na Tanzania Prisons huku ikichapwa 1-0 na Singida Black Stars, huku mechi tatu za kirafiki ikifungwa 2-1 na Geita Gold, sare ya 1-1 na Vital’O na suluhu dhidi ya Biashara United.

“Ukiuliza tatizo ni nini tatizo ni kocha labda sielewi mpira wa miguu au huenda sifanyi kitu kizuri, labda sifanyi maandalizi mazuri na mbinu bora za mechi kwa wachezaji wangu lakini siwezi kukimbia wajibu wangu na sijipi presha lakini ukiniuliza tatizo ni nini labda ni kocha,”  alisema Kopunovic bna kuongeza;

“Mimi sio kocha wa kubadilisha kikosi kila siku mfano mchezo wa leo (dhidi ya Singida Black Stars) niliwaamini wachezaji walioanza dhidi ya Azam FC na kufanya vizuri, najua vizuri sana kikosi changu na namna ya kuwatumia wachezaji.”

Akizungumzia kipigo dhidi ya Singida, Kopunovic alisema huenda kikosi chake kiliathiriwa na uchovu wa safari baada ya mchezo dhidi ya Azam FC ugenini Septemba 14 jijini Dar es Salaam kisha wakacheza tena Septemba 17 saa 8 mchana jijini Mwanza.

Related Posts