Dar es Salaam. Serikali imekuja na mikakati kadhaa ikilenga pia kutatua changamoto wanazokumbana kwa kundi hilo na namna ya kuishi baada ya kubaini magonjwa hayo ili kukabiliana na ongezeko la wanaougua magonjwa yasiyoambukiza.
Uanzishwaji wa mitaala ya ufundishaji kuhusu magonjwa yasiyoambukiza shuleni, upimaji kwa wanafunzi, kauli nzuri za watoto kwa wazazi na upimaji wa mara kwa mara ni moja ya mikakati iliyoidhinishwa.
Hayo yamebainishwa katika mkutano ulioandaliwa na Taasisi ya Tanzania Non Communicable Disease Alliance (TANCDA) kuhusu namna ya kutatua changamoto kwa wagonjwa hao, leo Septemba 19, 2024.
Akizungumza Mkurugenzi wa Wizara ya Afya, Kitengo cha Magonjwa Yasiyoambukiza, Dk Omary Ubuguyu ameeleza namna bora ya kutatua changamoto kwa wanaoishi na magonjwa hayo na umuhimu wa elimu kuhusu namna ya kumsaidia mwathirika wa magonjwa hayo apatapo tatizo.
“Moja ya makubaliano tuliyoyafanya leo ni kutengeneza umoja wa wenye magonjwa yasiyoambukiza ili wawe na kauli ya pamoja, lakini pia tumetoa nafasi ya mwakilishi wa kutoa ushauri katika huduma zetu tunazozitoa,” amesema.
Dk Ubuguyu amesema kati ya agenda zilizowasilishwa leo ni elimu kupitia clubs kwenye shule lakini pia kauli za watoto kwa wazazi wao.
“Tunapokea wazazi wengi wenye matatizo ya afya ya akili, ukimuuliza atakwambia mtoto wangu aliniambia ni bora ni singemzaa maana anateseka duniani, kuna kampeni ya “vunja mduara” tumeanzisha kuhakikisha upimaji wa magoniwa yasiyoambukiza shuleni,” amesema mkurugenzi huyo.
Amesema ushauri wao unawapa nguvu katika kufanya maamuzi, lakini pia wagonjwa hao wana jukumu la kutoa elimu kwenye jamii ili wanapopata tatizo wapate msaada wa haraka.
Aidha baadhi ya wagonjwa akiwemo Jacquline Adam (40) anaeishi na saratani ya titi iliyoanza mwaka 2016 na kugundulika 2020 anasimulia tatizo hilo lilivyoanza mpaka kuthibitisha ni saratani.
“Nilikua na uvimbe ambao baada ya kupimwa niliambiwa kuwa ni wa kawaida na kufanyiwa upasuaji ila baada ya miezi minne uvimbe ukaanza upya, baada ya vipimo vingine ndipo mwaka 2020 ikagundulika kuwa ni saratani,” amesema.
“Gharama ninazotumia sizimudu maana ni kubwa na hali hii imeathiri uchumi wangu kwa kupoteza kazi tangu nianze kuugua,” ameeleza.
Mhitimu wa kidato cha sita anaeishi na tatizo la kisukari, Salim Ali amesema kuna umuhimu wa elimu ya magonjwa yasiyoambukiza kufundishwa shuleni.
“Nilianza kwa kuanguka baada ya kuishiwa nguvu bila kujua tatizo ni nini, mpaka siku nilipoishiwa nguvu karibu na wanafunzi wa masomo ya sayansi ila wenzangu wa masomo mengine wa kawaambia huwa wananipatia soda yenye sukari kila ninapopatwa na tatizo hilo, wenzangu wa sayansi wakagundua ni sukari na ndipo nilipimwa ikawa kweli,” amesema.
Ameendelea kusisitiza kuwa kuna umuhimu wa elimu ya magonjwa yasiyoambukiza shuleni ni muhimu sana kwa kila mwanafunzi, kujua dalili na jinsi ya kumsaidia mgonjwa.
Ofisa mradi TANCDA, Happy Nchimbi amesema dhumuni kubwa la mradi huo ni kuhakikisha wanatengeneza umoja, ili tunapotengeneza sera iweze kutatua changamoto zao zote kwa wakati mmoja.
Aidha wagonjwa walioshiriki leo ni wagonjwa wa sukari, shinikizo la juu la damu, moyo, selimundu, saratani na afya ya akili pamoja na chama cha watu wenye kisukari Tanzania.
Baadhi ya changamoto wanazopitia wagonjwa hao ni pamoja na gharama kubwa za matibabu hasa wanapochelewa kugundua tatizo.