Miradi ya umeme kusisimua uchumi wa Kigoma

Dar es Salaam. Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Nishati Vijijini (Rea), Hassan Saidy amesema vijiji 279 kati ya 306 vya Mkoa wa Kigoma vimeunganishwa na umeme.

Taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari leo Alhamisi Septemba 19, 2024 na Rea imeeleza mbali na vijiji hivyo, mchakato wa kupeleka huduma ya umeme katika vitongoji 595 imeanza na wakandarasi wanaendelea na utekelezaji wa mradi huo.

“Katika vitongoji 1,849 vya mkoa wa Kigoma, 1,370 vimeshapata umeme, tunaendelea kuhamasisha wananchi kuendelea kutumia miradi hii kutekeleza na kubuni shughuli za kiuchumi zitakazoweza kuboresha uchumi wao pamoja na kulinda miradi hii,” amesema Saidy.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, Saidy ameeleza hayo wakati wa ziara ya mwenyekiti wa bodi ya wakurugenzi wa Rea, Meja Jenerali mstaafu, Jacob Kingu mkoani Kigoma kwa ajili ya kukagua shughuli za utekelezaji wa miradi mbalimbali ya umeme vijijini.

Katika ziara hiyo, Kingu amewataka wakandarasi kuhakikisha wanamaliza miradi hiyo kwa muda uliopangwa, akisema hawatasita kuwachukulia hatua za kimkataba mkandarasi yoyote atakayeshindwa kukamilisha miradi hiyo kwa wakati kama ilivyopangwa.

“Tumeshatoa maelekezo, hakuna muda wa nyongeza utakaotolewa kwa mkandarasi atakayeshindwa kutekeleza mradi wake ndani ya muda uliopangwa, labda kwa sababu maalumu.

Tumewaelekeza makandarasi pia wahakikishe malighafi yote yanayohitajika kama nguzo kabla ya msimu wa mvua kuanza ili miradi hiyo isichelewe kama ilivyo dhamira ya Serikali umeme kuwafikia wananchi wote ndani ya muda,” amesisitiza.

Mbali na hilo, Kingu amesema REA imetumia zaidi ya Shi100 bilioni kutekeleza miradi ya kupeleka umeme vijijini mkoani humo.

Mkurugenzi Bodi ya Nishati Vijijini (REB), Balozi Radhia Msuya amesema ziara hiyo ni muendelezo wa kuhakikisha inatembelea miradi inayosimamiwa na Rea ili kuhakikisha inakamilika kwa wakati na kubadilisha hali za wananchi wa vijijini.

Related Posts