Mtasingwa ataja sababu ya kuitosa Yanga

“MUDA ndio muamuzi wa kila jambo. Mengi yalizungumzwa juu yangu wakati wa dirisha la usajili, lakini wakati umeamua mimi kuwa hapa nilipo,” ni maneno ya kiungo wa Azam FC, Adolf Mtasingwa Bitegeko alipokuwa akijibu swali la kuhusishwa na Yanga kwenye usajili wa dirisha kubwa msimu huu.

Mtasingwa ambaye ameongeza mkataba wa miaka miwili wa kuendelea kuitumikia Azam FC amelithibitishia Mwanaspoti kuwa ni kweli alikuwa na ofa kutoka Yanga lakini amefanya uamuzi sahihi kubaki Chamazi kutokana na klabu hiyo kumuamini na kuhusu Jangwani, “labda wakati mwingine”.

Mwanaspoti lilipata nafasi ya kuzungumza na staa huyo ambaye amewahi kucheza soka la kulipwa Marekani na amefunguka mambo mbalimbali ikiwa ni pamoja na kumtaja kiungo Khalid Aucho kuwa alianza kumuangalia tangu akiwa timu ya vijana hadi kuja kucheza naye katika ligi moja.

Kila dirisha la usajili linapofunguliwa duniani kote kuna majina huwa yanatajwa kwenye timu fulani lakini mwisho wa dirisha majina hayo baadhi yanakuwa yamesajiliwa na mengine kuishia kuandikwa na kutamkwa tu hivi ndivyo ilivyotokea kwa Mtasingwa ambaye alikuwa anahusishwa na Yanga.

“Ofa zilikuwa ni nyingi kuanzia kule nilikotoka na kwa hapa Tanzania na imekuwa ikitajwa zaidi Yanga, lakini kulikuwa na ofa nyingi Bongo pia. Sina sababu ya kutaja hizo timu kwa sasa kwani tayari nimefanya uamuzi wa kubaki Azam FC,” anasema na kuongeza;

“Nimefanya uamuzi sahihi kubaki Azam FC, timu ambayo imenilea na kukunikuza kısoka, imani yao kwangu kwa kunipa nafasi ya kucheza ndio iliyonifanya na mimi niheshimu kwa kusaini mkataba na timu hii, kuna maisha mengine baadaye kama itatokea hapo baadaye nitaweza kucheza timu nyingine nje ya Azam FC.”

Akizungumzia suala la Yanga kumuongezea thamani kwenye usajili wake wa miaka miwili aliyoongeza Azam FC, kiungo huyo anasema hawezi kukataa hilo wala kukubali kwani anaamini ni mipango ya Mungu na juhudi zake vimechangia kwa kiasi kikubwa.

“Siwezi kukata kwamba Yanga imeniongezea thamani kusaini mkataba mpya lakini naamini pia kwenye kile nilichokifanya kwani nisingekuwa bora hata hizo timu zilizoleta ofa sidhani kama zingefanya hivyo,” anasema na kuongeza;

“Nitaendeleza juhudi zangu kwa kuhakikisha naipambania Azam FC ifikie malengo na ubora huo huo nitakaouonyesha utaendelea kufungua njia kwangu kunitoa sehemu moja kwenda nyingine kwani naamini sitakaa hapa milele wakati mwingine naweza kucheza nje ya Azam.”

Aucho ni kiungo anayetajwa kwa ubora wake anaoonyesha katika eneo la ulinzi la Yanga akisaidiana na kına Ibrahim Bacca, Dickson Job na Bakari Mwamnyeto na hilo limethibitishwa pia na Mtasingwa ambaye amemsifu staa huyo wa Uganda kuwa ni mchezaji bora na amefurahi kucheza naye katika ligi moja.

“Aucho ni mchezaji ambaye nimeanza kumtazama nikiwa na umri mdogo akiwa kwenye ubora wa hali ya juu, kupata nafasi ya kucheza naye amejiweka kwenye nafasi nzuri kwangu kujipima nina uwezo gani,” anasema na kuongeza;

“Kucheza na Aucho ni mambo mengi nimejifunza kutoka kwake na imenipa nafasi ya kujipima ubora wangu, haikuniwia ugumu kwenda kukabiliana naye kwasababu niliingia kwa kumuheshimu sikuwa mwoga, hilo lilinisaidia kuweza kumudu kucheza vyema.”

Anasema Aucho ni mchezaji ambaye licha ya kudumu muda mrefu, anakubali kipaji chake na amekuwa akiheshimu anachokifanya na kujifunza mengi kutoka kwake.

“Nafurahi kujifunza kutoka kwa wachezaji ninaocheza nao na hata walio timu pinzani, huwezi kuwa bora bila kukutana na changamoto kutokana na ubora wa wengine, mimi siku zote najifunza na nitaendelea kuwa mwanafunzi.”

Mara ya kwanza Azam FC kushiriki Ligi ya Mabingwa Afrika ilikuwa ni mwaka 2014 baada ya kutwaa taji la Ligi Kuu Bara 2013/14. Nyota wengi waliocheza michuano hiyo mwaka huo hawapo kikosini, lakini msimu huu baada ya kupata nafasi ya uwakilishi walipomaliza katika nafasi ya pili kwenye Ligi Kuu Bara, takriban kikosi chote kilichopo sasa, kimepata uzoefu tofauti kutokana na kuondolewa katika hatua ya awali akisema sababu ni uchanga wao kwenye michuano hiyo.

“Ligi ya Mabingwa Afrika ni mashindano makubwa sana, ili upate nafasi lazima uwe bora kwenye ligi unayocheza kwa kuhakikisha unamaliza ndani ya nafasi mbili za juu kwa Tanzania kwasababu tuna nafasi nne kimataifa (nyingine mbili hushiriki Kombe la Shirikisho Afrika),” alisema na kuongeza;

“Kwa upande wangu mimi ni mara yangu ya kwanza kucheza Ligi ya Mabingwa pia kuna idadi kubwa ya wachezaji kama mimi ambao tumecheza msimu huu, kushindwa kufikia malengo kuna tulipokosea, lakini zaidi tumejifunza na tutarudi kwa nguvu msimu ujao.”

Mtasingwa anasema ushiriki wao ulikuwa ni darasa, wamejifunza na wamepata kitu kwenye michuano hiyo na sasa wamerudi kwenye ligi kupambania nafasi nyingine mwakani ili warudi kwa nguvu katika soka la Afrika.

“Hakuna mchezaji ambaye hapendi mashindano makubwa, tuliumia kama wachezaji na hatuwezi kusema yale yalikuwa ni matarajio yetu kuishia hapo, tulitamani kuendelea lakini maji yalizidi unga, nafasi nyingine ikipatikana tutajua pa kuanzia kwani tumejifunza mengi,” anasema.

Tanzania kuna mastaa wengi wanaofanya poa uwanjani lakini darasani hawakuwa vyema na wengine wakaamua kuachana na shule kwa ajili ya kuwekeza nguvu kwenye vipaji vya soka hili ni tofauti kwa kiungo Mtasingwa ambaye amebainisha kuwa mpira ni mchezo wa muda mfupi hivyo elimu kwake ni sahihi na ndio maana ameamua kuwekeza nguvu huko pia kama anavyofunguka hapa.

“Mpira ni mchezo wa muda mfupi, nimeamua kujiwekea mazingira mazuri nje ya soka na ndio maana niliamua kuingia darasani ikiwa ni mipango ya wazazi lakini kadri umri ulivyokuwa unaenda nikawekeza nguvu zaidi darasani,” anasema na kuongeza;

“Maisha yanakupeleka sehemu tofauti sana, kuna sehemu nimepita sikuwahi kutarajia kama nitafika, nimesomea uchumi, lakini naamini pia kwenye kilimo kisha kadri umri unavyokwenda unaamua uwekeze wapi.”

Anasema elimu yake aliyoisomea amejiwekea mazingira mengine ili akiacha mpira na kadri anavyokua yeye ndiye atakaeamua nguvu zake awekeze wapi akiwa na machaguo zaidi ya matatu kilimo, uchumi na soka ambalo amekuwa akicheza.

Amecheza msimu mmoja sasa kwenye Ligi Kuu Bara na huu ni msimu wake wa pili, lakini ameanza kwa ubora akitoka kucheza soka huko Iceland na ametaja sababu ya ubora wake kuwa mazingira mazuri ya timu aliyopo sambamba na wachezaji wazuri aliokutana nao kikosini.

“Kuna mastaa walikuja Tanzania wakitoka mataifa bora ya soka na wakiwa bora lakini walishindwa kuendana na kasi ya Ligi Kuu Bara, kwangu imekuwa tofauti, namshukuru Mungu kwa hili na naamini kadri muda unavyokwenda nitakuwa bora zaidi,” anasema na kuongeza;

“Sababu kubwa nafikiri pia mazingira ya timu ninayoitumikia, yanaweza kuwa chachu ya ubora wangu kwani kuna kila kitu ambacho mchezaji anatakiwa kuwa nacho ili kukuza kipaji chake, nimetoka kucheza nje na nimekuja Azam FC nimekutana na mazingira rafiki.”

Mbali na Azam kumiliki uwanja wake wa mechi, ni klabu ambayo ina vitu vingine vingi ambavyo amekiri vimechangia kumvutia kubaki katika timu hiyo ikiwamo benchi la ufundi, wachezaji na viongozi imara ambao walimuhakikishia mambo mazuri.

Licha ya kumtaja Aucho kuwa ni kiungo bora asiyeisha ubora, Mtasingwa amesema Yahya Zayd wa Azam FC ni mchezaji wa kutazamwa kutokana na kucheza maeneo mengi uwanjani kwa ubora huku akiweka wazi kuwa anafurahishwa na uchezaji wa mchezaji huyo akipangwa eneo la kiungo.

“Eneo la kiungo kwa Tanzania limebarikiwa kuwa na vipaji vingi licha ya wageni pia kuja kutuongezea changamoto, namkubali sana Zayd amekuwa bora sana katika eneo la kiungo, hana woga na ni mtulivu katika kufanya uamuzi. Ukishakuwa na mchezaji wa aina kama yake kikosini hupaswi kuwa na wasiwasi,” anasema na kuongeza;

“Uwepo wake sambamba na Yanick Bangala, Ever Meza kutoka Klabu ya Leonnes ya Colombia imekuwa chachu kwangu kupambana kuhakikisha nakuwa bora ili kutoa mwanya kwa kocha kuniamini na kunipa nafasi ya kucheza kitu ambacho kwa kiasi chake nimefanikiwa lakini haina maana kuwa waliopo hawana uwezo.”

Mtasingwa anasema mastaa wote anaocheza nao nafasi moja wana uwezo mkubwa na wamekuwa wakimpa changamoto ya kupambana zaidi ili kujiweka kwenye nafasi ya kucheza.

Baada ya kushindwa kufikia malengo kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika, Mtasingwa amesema wao kama wachezaji wamekaa pamoja na kukubaliana kuhakikisha wanapambana kutwaa mataji ya ndani msimu huu ili kurudi kwenye uwakilishi kimataifa.

“Tunatambua mashabiki wanatamani kuona tunafika mbali kwenye michuano ya kimataifa, sisi pia kama wachezaji tunaumia na tuna malengo makubwa ya kufanya vyema kwenye michuano hiyo ambayo kwa ukanda wa Afrika ndio michuano mikubwa, tunaomba radhi kwa mashabiki na tunaahidi msimu huu licha ya kuanza vibaya mechi za mwanzo tutahakikisha tunarudi kimataifa kwa nguvu,” anasema na kuongeza;

“Ili kushiriki Ligi ya Mabingwa kwenye ligi inachukua mwaka kupambania taji hivyo tutahakikisha tunatwaa taji na kujiweka kwenye mazingira mazuri ya kutokurudia makosa kimataifa kwani msimu huu tumejifunza.”

Azam FC ilikuwa bora msimu ulioisha ikimaliza katika nafasi ya pili na kupata nafasi ya kuiwakilisha nchi kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya miaka 10, msimu huu wameanza na sare lakini kiungo huyo nyota wa kikosi hicho amesema licha ya kuanza vibaya haijawatoa mchezoni na malengo yao ni yale yale.

“Tumecheza mechi mbili ambazo matokeo yake hatujafurahishwa nayo, lakini bado tuna mechi nyingi, tunatakiwa kufanya mabadiliko ya aina ya uchezaji kwa kuongeza kasi kiuchezaji, tuna mchezo na KMC mechi ijayo, ubora na mbinu zinatakiwa,” anasema na kuongeza;

“Msimu uliopita tulikuwa bora sana, hivyo timu lazima zitakuja kwa kupambana, tunatakiwa kujipanga zaidi.”

Related Posts