Mwakilishi ahoji fidia kwa waliopisha miradi ya umeme

Unguja. Wakati mwakilishi wa Mtambwe, Dk Mohammed Ali Suleiman akiwasilisha kilio cha wananchi waliopisha miradi ya umeme bila kulipwa fidia, Serikali imekiri kuwapo changamoto hiyo na kueleza hatua inazochukua ili kuwalipa.

Dk Suleiman ametoa malalamiko hayo leo Septemba 19, 2024 kwenye Baraza la Wawakilishi, huku akiipongeza Serikali kwa kufanikisha miradi ya umeme.

Hata hivyo, amesema kuna kilio kwa wananchi walioharibiwa mazao yao ambao waliahidiwa kulipwa fidia lakini hawakupewa.

Amesema Shirika la Umeme Zanzibar (Zeco) liliwaahidi kuwapa fidia lakini halikutekeleza hivyo akataka kujua iwapo Serikali inajua kadhia hiyo, ni utaratibu upi unaotumika kwa wananchi wanaopisha miradi kama hiyo na lini wanatarajiwa kuwalipa.

Waziri wa Maji, Nishati na Madini, Shaib Kaduara amekiri Serikali kutambua uwepo wa wananchi katika vijiji vya Utaani, Migombani, Mtekofi, Mtemani na Kipangani katika Shehia ya Mtambwe Kusini, ambao wanasubiri malipo ya fidia za vipando (mazao) vyao kutokana na utekelezaji wa mradi wa upelekaji umeme katika vijiji hivyo uliofanywa na Zeco.

Kwa mujibu wa Zawadi, malipo yako katika hatua za mwisho baada ya kukamilika uhakiki wa wananchi na vipando uliyofanywa na mthamini mkuu baada ya kukamilika kwa mradi huo.

Amesema Serikali imeweka utaratibu wa kuwafidia wananchi wote wanaoathiriwa vipando au majengo yao ili kupisha miradi ya maendeleo katika maeneo mbalimbali endapo wapo kwenye maeneo hayo kihalali.

Kupitia Ofisi ya Mthamini Mkuu wa Serikali katika Wizara ya Ardhi na Maendeleo ya Makazi na ofisi za Serikali za mikoa na wilaya, kazi ya uthamini wa vipando au majengo ya wananchi yanayoathirika hutekelezwa mbele ya mwananchi anayeathirika.

“Kazi hii ya uthamini kwenye mashamba hufuatiwa na taratibu zingine za kiserikali ikiwemo uhakiki wa waathirika na vipando kabla ya kukamilisha malipo kwa wahusika,” amesema.

Amesema maeneo yaliyotekelezwa miradi ya upelekaji umeme Kivumoni, Gombe na Uwandani ndiyo pekee ambayo hayajafanyiwa malipo kwa wananchi baada ya kukamilika, miradi ambayo imekamilika ndani ya mwaka wa fedha 2023/24.

Related Posts