Morogoro. Mwandishi wa habari aliyekuwa akiandikia Gazeti la The Guardian mkoani Morogoro, Michael Sikapundwa amefariki dunia baada ya kupata ajali ya gari wakati akirudi nyumbani kutoka kazini.
Mwenyekiti wa klabu ya waandishi wa habari mkoani Morogoro, Nickson Mkilanya amethibitisha kifo cha mwandishi huyo ambaye siku chache zilizopita amerudi akitokea China alikokwenda kusoma.
Mkilanya amesema, Sikapundwa alipata ajali na kufikwa na umauti majira ya saa tano usiku eneo la Tungi barabara ya Morogoro – Dar es Salaam akiwa na gari yake ndogo na kwa sasa mwili umehifadhiwa katika Hospitali ya Rufaa Mkoa wa Morogoro.
“Ni kweli Sikapundwa amefariki dunia, taarifa nilizopata ni kwamba aligonga karavati na gari lake liliserereka na kusababisha kifo chake.
“Kwa sasa tunaendelea kuwasiliana na ndugu na jamaa na baada ya kuwapata ndio tutajua taratibu za mazishi zitakuwaje,” amesema Mkilanya.
Katibu wa klabu ya waandishi wa habari mkoa huo, Lilian Kasenene aliyekuwa na marehemu saa chache kabla ya kupata ajali na kufariki dunia, amesema kuwa alikutana naye maeneo ya barabara ya Kitope akiwa amekaa kwenye duka la rafiki yake.
“Kwa kweli kifo ni fumbo. Muda wa jioni nilikutana na Sikapundwa kwenye duka moja maeneo ya barabara ya Kitope tukaongea kidogo na akawa anatusimulia maisha ya China alipokwenda kusoma baadaye tukaachana.
Muda wa saa sita usiku nikapata taarifa kuwa amefariki kwa ajali, nimefika hospitali na nimeshuhudia mwili wake ukipokewa na kuhifadhiwa pale chumba cha maiti, kwa kweli nimeumia sana,” amesema Kasenene.
Katika uhai wake Sikapundwa aliwahi kuandikia pia Gazeti la The Citizen linalochapishwa na Kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL) kutokea Morogoro.