NYOTA wa JKT Tanzania, Edward Songo amesema moja ya usajili wa wachezaji wa kigeni waliomvutia msimu huu hadi sasa ni mshambuliaji wa Simba raia wa Cameroon, Leonel Ateba aliyejiunga nao akitokea USM Alger ya Algeria.
Songo aliyewahi kutwaa tuzo ya mchezaji na mfungaji bora wa Ligi ya Championship msimu wa 2022-2023 akiwa na timu hiyo baada ya kufunga mabao 18 alisema Ateba kwa jinsi alivyomuona ni mshambuliaji hatari na anahitaji kupewa muda tu.
“Jamaa ananivutia sana kwa sababu hana mambo mengi zaidi ya kuwaza lango la mpinzani, kwa wachezaji wa kigeni ni moja ya washambuliaji bora msimu huu, nafikiri kama ataendelea kuaminiwa na kupunguziwa presha atafanya mambo makubwa,” alisema.
Songo aliyefunga mabao matatu ya Ligi Kuu Bara msimu uliopita, aliongeza, Ateba kwake anamfananisha na mshambuliaji wa Manchester City ya England, Erling Haaland kwa jinsi anavyojitengenezea mazingira mazuri akikutana na mpinzani.
Tangu ajiunge na Simba, Ateba amecheza michezo miwili tu na mmoja ni wa kirafiki dhidi ya Al Hilal ya Sudan ambao alifunga bao moja katika sare ya 1-1 na wa Kombe la Shirikisho Afrika mbele ya Al Ahli Tripoli ya Libya ulioisha suluhu.
Ateba alijiunga na USM Alger Januari mwaka huu akitokea Dynamo Douala FC ya kwao Cameroon, huku msimu uliopita nyota huyo alicheza jumla ya michezo 23, ya mashindano tofauti tofauti na alifunga jumla ya mabao matatu na kuasisti saba.
Nyota huyo aliyewahi kuzichezea timu mbalimbali zikiwemo za Cotonsport na PWD Bamenda, anakumbukwa zaidi mwaka 2023, alipoibuka Mfungaji Bora wa Ligi ya Cameroon baada ya kufunga mabao 21, yaliyomfanya kuitwa kikosi cha timu ya taifa ya Cameroon kilichoshiriki fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (Afcon) 2023 zilizofanyika mapema mwaka huu Ivory Coast.