Dar es Salaam. Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Mipango na Uwekezaji, Profesa Kitila Mkumbo amesema uwekezaji katika viwanda ndio msingi wa kukuza uchumi.
Profesa Mkumbo amesisitiza kuwa maendeleo ya nchi yeyote huonekana katika uwekezaji na katu hakuna nchi duniani iliyoendelea bila uwekezaji.
Waziri huyo ametoa kauli hiyo jana Septemba 18, 2024 wakati akizindua ukumbi wa maonyesho wa kisasa wa BFG Africa uliojengwa na kampuni ya kimataifa ya BFG International.
“Kama tunataka kuzalisha ajira, kushughulikia masuala ya umaskini kwa njia endelevu, itatubidi kuwekeza kwenye viwanda,”amesema.
Profesa Mkumbo amesema changamoto ambayo imeendelea kuikabili Tanzania ni uchumi wake kutegemea uagizaji wa bidhaa zinazouzwa nje ya nchi, hali inayohamisha fedha za kigeni kwenda kwenye nchi zenye viwanda.
“Tunawashukuru kwa kuzindua ukumbi huu kwa sababu linasaidia ajenda yetu ya kiuchumi hasa nilipoona neno viwanda’. Uundaji wa viwanda ni muhimu kwa maendeleo na ustawi wa kiuchumi wa Afrika,” amesema.
Rais wa BFG International, Dk Samer Aljishi amesema kuingia kwa BFG Africa kwenye soko kunalenga kupunguza mahitaji makubwa ya bidhaa maalumu katika sekta za viwanda, ujenzi, na usafirishaji.
“Kwa utaalam wake uliothibitishwa katika uzalishaji wa malighafi kwa ajili ya boti, treni, mabasi na magari mengine, kampuni hiyo iko tayari kukidhi mahitaji ya soko la Tanzania na Afrika Mashariki,” amesema.
Mwenyekiti wa BFG Africa Masimo Magerman amesema kampuni hiyo inajivunia kuongoza matumizi ya bidhaa iliyochanganywa (composites) barani Afrika.
“BFG Africa imekuwa ikifanya kazi Kusini mwa Afrika kwa miaka mitano, na imepata sifa ya kutoa bidhaa za hali ya juu kwa bei za ushindani, zikiwa na huduma bora na za kuaminika,” amesema Magerman.
“Tunaona Dar es Salaam kama lango litakalotuwezesha kupanua wigo wa bidhaa na huduma zetu barani Afrika, huku BFG Tanzania ikitumika kama msingi wa ukuaji wa soko la kundi hili,” amesema.
“Kwa uwekezaji huu mkubwa, BFG Africa ina matumaini ya kuimarisha nafasi ya Tanzania kama kitovu cha kikanda cha ukuaji wa viwanda na ubora wa uzalishaji,” aliendelea kusema.
Amesema kampuni hiyo inatarajia kusaidia kupunguza utegemezi wa soko la Afrika Mashariki kwa bidhaa zinazoagizwa kutoka nje, huku ikiunda nafasi nyingi za ajira kwa soko la ajira la Tanzania.
Magerman alisema BFG Africa inaamini kuwa mpango huu utachangia kwa kiasi kikubwa katika maendeleo ya viwanda na uchumi wa kanda hiyo, akibainisha kuwa Tanzania na Zanzibar ndio maeneo ya awali ya kuzingatia.
“Dira yetu ni kuanzisha kiwanda cha uzalishaji wa ndani ambacho si tu kitatimiza mahitaji ya soko la kikanda bali pia kitaongeza ajira na kuwezesha uhamishaji wa ujuzi kwa wafanyakazi wa ndani,” alihitimisha.