Simulizi ya kijana anayewasaidia nyoka wasiuawe na binadamu

Morogoro. Ukistaajabu ya Mussa, hutayaona ya Filauni. Ndivyo unaweza kuelezea kisa cha kijana huyu anayejiita ‘rafiki wa nyoka’ kutokana na ukaribu alioujenga na mnyama huyo.

Nyoka ni kiumbe hatari anayeogopwa na wengi kutokana na asili yake ya kuuma na sumu yake kuweza kusababisha kifo au kumdhuru aliyeumwa. Anapoonekana kwenye makazi ya watu, anakuwa adui wa binadamu, kwani hupambana kumuua.

Wakati watu wakiwaogopa nyoka, hali ni tofauti kwa kijana Issa Njipwile, mkazi wa kata ya Kisawasawa, Wilaya ya Kilombero mkoani Morogoro. Yeye amekuwa akiwakamata nyoka wanaopatikana kwenye makazi ya watu na kuwarudisha porini wakiwa hai.

Ujasiri wake wa kuwashika nyoka na kuwaokoa wasiuawe na binadamu umempa umaarufu kijijini na sasa anajulikana kama “Issa Manyoka”.

Akizungumza na Mwananchi leo Jumatano Septemba 18, 2024, Issa amesema amekuwa akikamata nyoka wanaoingia kwenye makazi ya watu nashambani kwa lengo la kuwaokoa wasiuawe na watu na baada ya kuwakamata huwarudisha porini.

“Sipendi kuona nyoka anauawa na ninaamini ni kiumbe anayeishi porini, hivyo anapoonekana kwenye makazi ya watu ni kama amepotea njia tu, na kwa kuwa hata binadamu huwa anapotea njia, basi ni vema nyoka anapoonekana kwenye makazi ya watu akamatwe na kurudishwa kwenye makazi yake ya asili.

 “Nyoka niliowahi kuwakamata na kuwarudisha porini ni pamoja na kobra, moma, kifutu, ndugulu, kigao, swaga, sangalaza na aina nyingine na wamenigonga mara nyingi ambazo hazihesabiki, lakini sijawahi kwenda hospitali kutibiwa wala kutumia dawa. Kutokana na urafiki wangu na nyoka, mwili wangu tayari umejitemgenezea kinga dhidi ya sumu ya nyoka,” amesema.

Issa amesema mara nyingi nyoka wamekuwa wakionekana kwenye makazi ya watu kipindi cha kiangazi ambapo wadudu wa porini wanaoliwa na nyoka wanakuwa wamepunguza, na pia mapori mengi katika kipindi hicho yanasafishwa kwa ajili ya kuandaa mashamba, hivyo nyoka hukimbilia kwenye nyumba za watu kutafuta malisho ambayo ni wadudu wa nyumbani kama panya, mende, mchwa na kumbikumbi.

Kijana huyo amesema nyoka wanaoonekana katika kipindi hicho, ni wale wanaozalisha sumu kali kwa ajili ya kujihami na kupambana na binadamu wanaotaka kuwadhuru pindi wanapoingia kwenye makazi yao.

Katika kipindi hicho cha kiangazi, maji kwenye mito na hao wamekuwa wakikaa sehemu zenye majimaji, ikiwemo kando ya mito, visima na kwenye vivuli vya miti na mazao kama migomba na miwa.

Issa anayejishughulisha na kilimo na biashara ndogondogo, amesema ameanza kazi ya kukamata na kutoa nyoka tangu akiwa na umri wa mdogo na kwa historia, kazi kama hiyo alikuwa akifanya babu yake ambaye kwa sasa ni marehemu.

“Tangu nikiwa na umri mdogo nilikuwa ni mtoto nisiyeogopa wadudu, hivyo nilikuwa nakamata kila mdudu ninayemuona. Siku moja nilikuta watu wanampiga nyoka, kiukweli niliumia, niliamua kumuokoa kwa kumshika na kumrudisha porini, tangu siku hiyo nikapata ujasiri, nikawa nawakamata na kuwarudisha porini,” amesema.

Akieleza mbinu anazotumia wakati wa ukamataji, Issa amesema huwa anapiga mluzi na kuimba nyimbo fulani ambazo zinamfanya nyoka ajue yuko kwenye mikono salama na anapomkamata huwa anawahi kumshika mkiani ambako ndiko sumu na nguvu ya nyoka iliko, hivyo nyoka hulegea na kutulia.

Amesema tangu ameanza shughuli hizo, nyoka wakubwa aliowakamata walikuwa ni aina ya kobra ambao walikuwa kwenye shamba la mwanakijiji mmoja na alipigiwa simu kwenda kuwakamata nyoka hao ambao walikuwa wamejificha kwenye kichuguu.

“Situmii uchawi wala mazingaombwe, nina shughuli zangu maalumu za kunipa riziki ya kula kila siku, isipokuwa anapoonekana nyoka shamba au kwenye makazi ya watu, naitwa kwenda kutoa msaada kwa binadamu na nyoka mwenyewe, ili wote wawe salama.

“Nikishamkamata nyoka, namuweka kwenye mfuko, natafuta pori lisilokuwa na makazi ya watu, namwachia aendelee na maisha yake ya asili, kwa ufupi mimi ni rafiki wa nyoka,” amesema Njipwile.

Amebainisha kwamba hapa duniani anawaogopa wanyama wakali kama tembo, simba, mamba na viboko kwa sababu wana nguvu kubwa, lakini nyoka ni kiumbe mdogo na pia zipo dawa za kumtibu mtu aliyegongwa na nyoka.

“Siwezi kumuogopa nyoka kwa sababu dawa za kumtibu mtu aliyegongwa na nyoka nazijua japo sijawahi kuzitumia. Nikigongwa na nyoka, nachanja pale kwenye jeraha, natoa meno naendelea na maisha yangu mengine, sifungi kamba wala siweki dawa, nadhani hizi sumu zimegeuka kuwa kinga kwenye mwili wangu,” amesema kijana huyo.

Akitoa ushuhuda kuhusu ujasiri wa kijana huyo, mmoja wa wakazi wa Kata ya Kisawasawa, Elizabeth Mwakalambo, amesema yeye ni miongoni mwa walioshuhudia kijana huyo akikamata na kuokoa nyoka shambani kwake na kwenye maeneo mengine kijijini hapo.

“Siku hiyo nikiwa shamba, ghafla nilisikia mlio kama kufoka hivi, niliposogelea karibu nikaona ni nyoka, nikampigia simu Issa akaja, alichofanya cha kwanza alichimba shimo kubwa jirani ya kile kichuguu alimokuwemo nyoka na kisha akaanza kubomoa kile kichuguu na ghafla nyoka mkubwa aina ya kobra alitoka na kutumbukia kwenye shimo na baada ya hapo Issa aliingiza mkono kwenye shimo na kumkamata yule nyoka,” amesema Mwakalambo.

Mwanamke huyo ameongeza kuwa: “Baada ya kumtia kwenye mfuko ghafla, tukasikia mlio mwingine mahali palepale, akaendelea kutifuatifua pale kwenye kichuguu na kumtoa nyoka mwingine. Siwezi kujua kama wale nyoka walikuwa mtu na mke wake au mtu na mtoto wake, maana wote wanalingana ukubwa na muonekano.”

Mwakalambo amesema kijana huyo kijijini hapo amejizolea umaarufu mkubwa kwa kuwakamata na kuwaokoa nyoka wanaotaka kuangamizwa kwa kupigwa na kutokana na ujasiri wake huo, wamempa jina la “Issa Manyoka”.

“Kama kuna namna Serikali inaweza kumshika mkono, basi wamshike maana bado ni kijana mdogo na anahitaji kuwezeshwa ili afike mbali. Anawajua nyoka na tabia zake zote, ameweza kupata ajira ama kujiajiri kupitia ujasiri wake huu,” amesema Mwakalambo.

Kwa upande wake, diwani wa Kisawasawa, Daniel Songo amesema kijana huyo amekuwa msaada mkubwa kijijini hapo, hasa pale nyoka wakubwa wanapoingia kwenye nyumba za watu na kuhatarisha usalama.

“Huku vijijini nyoka ni wengine na kuna wakati hasa wa mavuno, nyoka wanakuwa wengi majumbani, huyu kijana anayejiita rafiki wa nyoka amekuwa msaada kwa wananchi, lakini pia kwa nyoka wenyewe. Nimebahatika kumuona akikamata na kuokoa nyoka wanaotaka kuuawa, kwa kweli huyu kijana ni jasiri,” amesema Songo.

Amesema katika kumsaidia kijana huyo yeye kama diwani amekuwa akimpeleka kwenye maonyesho ya wakulima Nanenane na maonyesho mengine kwa ajili ya kuonyesha ujasiri wake katika kukamata nyoka na kupitia maonyesho hayo amekuwa akipata fedha kidogo za kujikimu.

Hata hivyo, amesema fedha hizo zimekuwa ni za msimu, hivyo ipo haja kwa mamlaka mbalimbali zilizojihusisha na masuala ya utalii na maliasili kumshika mkono kijana huyo na kumpa shughuli maalumu inayohusu kipaji chake.

Related Posts