Takwimu zaonyesha umasikini waongezeka Zanzibar

Unguja. Wakati takwimu zikionyesha kiwango cha umasikini kuongezeka Zanzibar, Serikali imeainisha hatua inazochukua kukabiliana na changamoto hiyo.

Kwa mujibu wa Ofisi ya Mtakwimu Mkuu wa Zanzibar, kwa mwaka 2019/20 tathmini ya hali ya umasikini iliainisha wa mahitaji ya msingi ni asilimia 25.7 na umasikini wa chakula ni asilimia 9.3, huku wilaya nne za mikoa ya Pemba zikionekana kuwa na kiwango kikubwa cha umasikini.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Fedha na Mipango, Dk Saada Mkuya ametoa kauli hiyo leo Septemba 19, 2024 katika Baraza la Wawakilishi.

Amesema hufanywa tathimini ya kina juu ya hali ya umasikini Zanzibar kila baada ya miaka mitano na tathmini nyingine imefanyika mwaka 2022.

Alikuwa akijibu swali la Mwakilishi wa Mtambwe, Dk Mohammed Ali Suleiman aliyetaka kujua tathmini ya kitaalamu kuhusu asilimia ya wananchi wanaoishi chini ya mstari na umasikini wa mahitaji ya msingi.

Pia ametaka kujua hatua zinazochukuliwa akisema umasikini ni kikwazo katika kufanikisha malengo na umesababisha hali duni ya maisha kwa wananchi.

Amesema mwaka 2019/20 hali ya umasikini wa mahitaji ya msingi ulikuwa Micheweni asilimia 48.8, Mkoani (44.4), Wete (42.5), Chake Chake (37.3), Kaskazini A (21.9) na Kaskazini B (27.22), Kati (21.5), Mjini (17.9), Kusini (14.8), Magharibi A (14.7) na Magharibi B (9.5).

Kwa upande wa hali ya umasikini wa chakula amesema Micheweni ilikuwa asilimia 18.7, Mkoani (19.4), Wete (17.1), Chake Chake (19), Kaskazini B (7), Kaskazini A (5.1), Kati (6), Mjini (5.7), Kusini (1.7), Magharibi A (5.1), na Magharibi B (2).

Dk Saada amesema Serikali ina mikakati ya muda mrefu na wa kati ya kupunguza umasikini Zanzibar ikiwa ni pamoja na Dira ya Maendelo ya Zanzibar ya 2050 ambayo imepanga kuondoa umasikini wa mahitaji ya msingi kuwa asilimia sufuri ifikapo mwaka 2050.

“Mikakati hiyo hutekelezwa kupitia mipango ya muda wa kati (Zadep 2021-26) na mfupi ambao malengo na shabaha huainishwa ili kuziwezesha taasisi za Serikali na binafsi kutekeleza mipango hiyo kama ilivyokusudiwa,” amesema.

Miongoni mwa mikakati hiyo amesema ni uwezeshaji wananchi kiuchumi, uimarishaji wa mazingira ya ufanyaji biashara, kuimarisha uwekezaji utakaoleta tija kwa wananchi ili kuongeza upatikanaji wa ajira.

Pia, uwezeshaji upatikanaji wa huduma za elimu na afya kwa urahisi zenye ubora na ufanisi.

Mipango mingine ni kukuza rasilimali watu kwa kuimarisha mafunzo kwa watendaji wa Serikali na taasisi binafsi, uboreshaji wa mitalaa kwa vyuo vya amali na vyuo vikuu Zanzibar.

Pia, kujenga utamaduni wa kujifunza na maendeleo ya rasilimali watu kidijitali.

Related Posts