Twende Butiama 2024 ni zaidi ya mbio

WAKATI ikiingia msimu wa sita mwaka huu, mbio ya Twende Butiama imezidi kunoga baada ya Benki ya Stanbic kuungana na Vodacom Tanzania kuifanikisha.

Msimu huu waendesha baiskeli wa Twende Butiama wataanza safari Septemba 29 wakipita mikoa 12 huku wakitarajiwa Oktoba 14 kuwa Butiama alipozaliwa baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.

Mbio hiyo inayolenga kumuenzi Mwalimu Nyerere inaunga pia mkono juhudi za serikali katika elimu, mazingira na afya, mambo ambayo pia Rais huyo wa kwanza wa Tanzania aliyasisitiza wakati wa utawala wake.

Mkuu wa Mahusiano ya Vodacom Tanzania, Annette Kanora alisema wameungana na Stanbic Tanzania kwenye msafara wa Twende Butiama wakilenga kuenzi kumbukumbu za Mwalimu Nyerere kwa kusaidia kuboresha huduma za afya, elimu na utunzaji wa mazingira.

Twende Butiama 2024 sio tu ni mbio, lakini inalenga kuongeza uelewa kwa ajili ya kusoma na kuandika, ikizingatia hasa ujuzi wa kidijitali na kifedha.

Alisema mbio hiyo itahusisha pia shughuli mbalimbali za kijamii ikiwemo warsha za elimu, kambi za afya na kampeni za kuhamasisha uelewa wa mazingira, zikifikia jamii kote Tanzania.

Meneja Uhusiano na Chapa wa Stanbic, Annette Nkini alisema; “Kuwekeza katika elimu, afya na kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi ni sehemu kuu ya uwekezaji wetu wa kijamii na juhudi endelevu. Tunafurahi kushirikiana na Vodacom  kuleta athari Chanya kwenye jamii.”

Mwanzilishi wa Twende Butiama, Gabriel Landa alisema msimu huu mbio hiyo itawakutanisha waendesha baiskeli kutoka Tanzania na nje ya nchi.

Akiielezea mbio hiyo, alisema ilianzishwa mwaka 2019 na kikundi cha waendesha baiskeli, ili kuadhimisha upendo wa Mwalimu Nyerere na maono yake kimaendeleo katika maeneo matatu muhimu ya elimu, afya, na utunzaji wa mazingira ambayo yanaweza kuwasaidia Watanzania kupiga hatua kijamii na kiuchumi.

Landa alisema alipata wazo la kuanzisha mbio hiyo akiwa anasafiri kwenda Lindi na alikutana na mtoto wa Mwalimu Nyerere yeye Landa akamwambia waende Butiama ndipo wakaja na wazo la kumuenzi Baba wa Taifa ambaye alisisitiza kutokomeza ujinga, alisitisisitiza kutunza mazingira na afya bora.

Alisema mwaka mbio hiyo itapita kwenye mikoa 12 waendesha baiskeli wakienda kilomita 1846.

Related Posts