Dar es Salaam. Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), John Mnyika amesema kuhamasisha wananchi kujiandikisha kwa wingi kwenye daftari la wakazi ni turufu itakayowawezesha kushinda viti vingi katika uchaguzi wa serikali za mitaa utakaofanyika Novemba 27, 2024.
Uandikishaji wa uchaguzi huo utakaohusisha vijiji 12, 333, vitongoji 64,274 na mitaa 4,269 utafanyika kuanzia Oktoba 11 hadi 20, 2024.
Mnyika amesema hayo leo Alhamisi, Septemba 19, 2024 wakati akifungua mafunzo ya siku mbili kwa viongozi wa Baraza la Wanawake wa chama hicho (Bawacha) nchi nzima yanayofanyikia jijini Dar es Salaam.
Mafunzo hayo yanalenga kuwajenga wanawake hao kisaikolojia kama kundi lenye nguvu katika jamii kutumia ushawishi wao kujiandaa na uchaguzi wa serikali za mitaa kwa kuhamasisha watu kujitokeza kushiriki na kugombea nafasi mbalimbali ili kuingia katika mikondo ya uamuzi.
“Jukumu tunalopaswa kulifanya kuanzia tutakapomaliza mafunzo haya tutumie kila njia ikiwemo mitandao ya kijamii, mikutano, vipindi katika vyombo vya habari, popote pale iwe kwenye mabasi na saluni kuelimisha wananchi kuanzia sasa kuwa kuanzia Oktoba 11 hadi 20 mwaka huu kila mmoja ajiandikishe kwenye Kijiji chake au Kitongoji.
“Katika kila kituo tuhakikishe kuna kuwa na wakala wa Chadema ili kudhibiti taarifa feki, sasa tuone wanawatu CCM wa kujipanga foleni na kutushinda tunajua hawana tutawashinda hapo anzeni na hilo msisubiri kampeni za uchaguzi au siku ya kupiga kura,” amesema Mnyika.
Mnyika katika kujenga hoja hiyo, amesema uboreshaji wa daftari la kudumu la mpiga kura unaoendelea kwa sasa unahusu watu waliopoteza kadi, walihama makazi kuboresha taarifa zao na kuandikisha vijana ambao hawakuandikishwa.
“Kwa wale waliondikishwa hawajahama makazi na anakadi ya mpiga kura hausiki. Wananchi wengi wamekaa kusubiri lakini siri ambayo hawaijui uchaguzi wa Novemba 27 hautatumia daftari la kudumu la mpiga kura kwahiyo hatakama una kadi ya mpiga kura unapaswa ukaandikishwe upya kwenye daftari la wakazi na ratiba ya uandikishwaji itaanza Oktaba 11 hadi 20 mwaka huu,” amesema.
Mnyika amesema wakati joto la kisiasa likiwa chini hakuna kampeni za uchaguzi na watawala wakiendelea kutia hofu wananchi kwa matukio ya utekaji wanataka watu wabaki nyumbani halafu wao wameshatoa maelekezo kwa watu wao kupita huko mitaani kuandika orodha yao ili wahamishe daftari la kudumu la kupiga kura kwenye uchaguzi wa mitaa.
“Umma utakavyoshituka na joto la uchaguzi limepanda watu wakienda kupiga kura waweke sharti kama hujaandikisha daftari la wakazi hawezi kuruhusiwa kupiga kura,” amesema.
Jambo lingine alilosisitiza katika hotuba yake ni kuhamasisha wanawake kugombea nafasi mbalimbali katika uchaguzi huo huku akieleza unahusisha nafasi nyingi na unahitaji wagombea wengi.
“Uchaguzi huu vijiji pekee yake viko 12, 333, Vitongoji 64,274 wakati huo mitaa ikiwa 4,269 ni nafasi nyingi inahitajika zaidi ya wagombea 300,000 ni fursa kwa wanawake kuingia kwenye vyombo vya maamuzi uhamasishaji unahitajika,” amesema.
Katika maelezo yake, Mnyika amesema wakati joto la uchaguzi likiendelea ni muhimu Baraza hilo kuunda timu itakayokuwa mahususi katika kushughulikia suala la dira ya taifa ili kuweka misingi thabiti kwa vijana wao.
“Nilazima suala hili tulitazame kwa mapana yake badala ya kuwaachia watawala kutuandalia mambo yao ambayo mwisho wasiku yatakuja kuleta shida kwa vijana wetu miaka 50 ijayo,” amesema Mnyika.
Mwenyekiti wa Baraza hilo, Sharifa Suleiman amewataka viongozi walichaguliwa kuwa majasiri kwa kutokugopa vitisho vinavyoendelea kujitokeza nchini na badala yake wanapaswa kuongeza mapambano.
“Wito wangu kwa viongozi wateule kujiandaa na uchaguzi na kuhakikisha chama kinaenda kupata ushindi wa kishindo kwa kuhakikisha jamii inashiriki kikamilifu,” amesema Sharifa.
Awali, katika mkutano huo, Katibu Mkuu wa Bawacha, Catherine Ruge amesema uchaguzi huo hautakuwa rahisi huku akieleza dalili zimeshaanza kujionyesha za kuwatisha wananchi.
“Baraza limekuwa likichukua hatua mbalimbali kuona jamii inashiriki kikamilifu chaguzi zilizopo mbele kwani tumeshatengeneza sera ya jinsia na ujumuishwaji kuhakikisha makundi yote yanapata fursa ya kushiriki siasa,” amesema.