VISION CARE YATOA MSAADA MUHIMBILI WA MASHINE YA UPASUAJI MTOTO WA JICHO KUPITIA TUNDU DOGO YENYE THAMANI YA TZS. 30 MIL.

 

 

 
Hospitali ya Taifa Muhimbili imepokea msaada wa mashine ya kisasa yenye thamani ya TZS. 30 Mil kutoka taasisi ya kimataifa ya Vision Care kwa ajili kuboresha huduma za upasuaji wa mtoto wa jicho kupitia tundu dogo ili kuongeza ufanisi na ubora zaidi katika kutoa huduma hiyo.
 
Akikabidhi msaada huo Mwenyekiti wa taasisi hiyo duniani, Dkt. Dong Hae Kim amesema mashine hiyo itasaidia kuboresha huduma za upasuaji pamoja na kuwajengea uwezo wataalam wa MNH na badaye kufundisha wenzao waliopo hospitali mbalimbali za Kanda na Mikoa hapa nchini.
 
“Tumekuwa na ushirikiano na Muhimbili kwa zaidi ya miaka nane. Hospitali hii inatambulika kama kituo kikubwa cha tiba nchini, hivyo ni muhimu wataalam wake kuendelea kupata mafunzo ili kuimarisha huduma za kibingwa na ufanisi wa utoaji huduma hizo,” amesema Dkt. Kim.
 
Kwa upande wake Bingwa wa Magonjwa ya Macho na Mkuu wa Idara ya hiyo MNH, Dkt. Joachim Kilemile amesema awali upasuaji wa mtoto wa jicho ulikua ukifanyika kutumia tundu kubwa na sasa kwa kutumia teknolojia hiyo inamuwezesha mgonjwa kuona haraka na kuruhusiwa kutoka hospitalini mapema zaidi.
 
Naye Kaimu Mkurugenzi wa Huduma za Upasuaji ambaye pia alimwakilisha Mkurugenzi Mtendaji wa MNH, Dkt Ibrahimu Mkoma ameishukuru Serikali ya Korea Kusini kupitia Shirika la Maendeleo la KOICA na Vision Care kwa msaada huo, akisema kuwa juhudi hizi zinaendana na lengo la serikali ya kusogeza huduma karibu na wananchi ambazo hapo awali walilazimika kuzifuata nje ya nchi.
 
Mapema wiki hii Hospitali imeanza kambi ya upasuaji wa mtoto wa jicho ambapo mpaka sasa wagonjwa 23 wamepatiwa huduma hii.

 

Related Posts