Vita dhidi ya wauzaji wa mbegu feki, Bashe atoa darasa kwa wakulima

Songea. Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe ametangaza vita dhidi ya wauzaji wa mbegu feki za mahindi, na kubainisha kuwa Serikali itachukua hatua kali dhidi ya watakaobainika.

Bashe amebainisha hayo jana Jumatano, Septemba 18, 2024, katika vituo vya uuzaji wa mahindi vya Kizuka na Mgaziniwa wakati akitangaza mpango wa Serikali kutoa mbegu za mahindi za ruzuku kwa wakulima nchini kote katika msimu wa kilimo wa 2024/25.

Tangazo hilo limetolewa siku chache kabla ya ziara ya Rais Samia Suluhu Hassan mkoani Ruvuma inayotarajiwa kuanza Ijumaa, Septemba 20, 2024.

Wakulima hao wamekusanyika katika vituo hivyo kwa wiki kadhaa wakisafisha na kuchambua shehena ya mahindi yao kabla ya kuyauza Wakala wa Hifadhi ya Chakula (NFRA).

Zoezi la usafi na uchambuzi wa bidhaa hiyo limekuja baada ya mahindi yaliyowasilishwa kwa mauzo kugundulika kutokidhi viwango vya ubora kwa ajili ya mauzo hasa nje ya nchi.

NFRA inanunua mazao hayo kwa Sh700 kwa kilo, kiwango cha juu ikilinganishwa na kiasi kisichozidi Sh500 kwa kilo kinachotolewa na wanunuzi binafsi.

Akizungumza katika vituo hivyo kwa nyakati tofauti, Bashe amebainisha kuwa mbegu za mahindi za ruzuku zitafungashwa katika vifungashio vyenye alama ya nembo ya Taasisi ya Uthibitisho wa Mbegu za Tanzania (Tosci), pamoja na nambari za siri zinazoweza kuonekana na wakulima baada ya kukwangua rangi maalumu kwenye kifungashio.

“Mara tu unaponunua mbegu za mahindi za ruzuku, hakikisha unazitambua alama hizi muhimu. Chukua simu yako ya mkononi na piga 150 andika nambari kutoka sehemu iliyokwanguliwa kutoka kwenye kifungashio ikifuatiwa na # kisha bonyeza kitufe cha kutuma,” amesema Bashe.

Bashe amesema mkulima atapokea ujumbe wa maandishi ukiwajulisha kwamba kifungashio cha mbegu ya ruzuku alichonunua ni halali, na kutahadharisha kuwa endapo hakutakuwa na ujumbe utakaopokelewa, atambue kuwa mbegu hizo ni feki.

“Mkulima anapaswa kuripoti kwa ofisa mtendaji wa kijiji mara moja ili mtuhumiwa akamatwe kwa hatua za kisheria kuchukuliwa. Hatua hizo ni pamoja na kutambua mtandao wote wa mbegu feki zilizomfikia mkulima husika,” amesema.

Aidha, aliwahakikishia wakulima katika vituo hivyo kuwa serikali itanunua mahindi yote katika akiba zao na kuwapatia wanunuzi wa mahindi yaliyochambuliwa katika zoezi la kusafisha na kuchambua bidhaa hiyo kwani licha ya kutofaa kwa matumizi ya binadamu, mahindi hayo yanaweza kutumika kutengeneza chakula cha mifugo.

Amesema serikali imepanga kuongeza vifaa vya kusafisha mahindi ili kuharakisha mchakato huo, na kwamba vifaa vya kisasa vya usafishaji na uchambuzi vitafungwa katika vituo mbalimbali katika msimu ujao wa kilimo ili kuwapunguzia wakulima adha wanazokutana nazo mwaka huu.

“Mahindi ya mkoani Ruvuma yamekuwa yakilalamikiwa kwa uchafu. Zoezi la usafishaji ambalo ni taratibu za kimataifa limeanzishwa ili kuhakikisha Tanzania inasafirisha bidhaa bora kwa matumizi ya binadamu,” amesema.

Akizungumzia adha wanayoipata, Nicodem Moyo amesema mbegu bandia ni changamoto kubwa iliyopelekea wakulima kuzalisha bidhaa zenye hitilafu msimu huu.

“Maofisa wa ugani wanapaswa kuwafundisha wakulima kuhusu masuala ya msingi yanayohusiana na ubora wa bidhaa za kilimo jambo ambalo litazuia usumbufu usio wa lazima kama vile usafishaji katika vituo vya uuzaji,” amesema.

Paul Haule amesema kuna haja ya kuongeza maghala ya kuhifadhi bidhaa za kilimo na kubainisha kuwa uhaba wa maghala ni changamoto kwa wakulima hasa baada ya ongezeko la uzalishaji lililotokana na utekelezaji wa mipango mbalimbali ya serikali.

Kwa upande wake, Zena Zawamba amesisitiza umuhimu wa kutoa vifaa vya kisasa vya kusafisha mahindi ili kuwawezesha wakulima kutumia muda wao kwa ufanisi, na kuepuka kutumia muda mwingi kwa usafishaji na uchambuzi wa mazao.

“Nimetumia karibu mwezi katika kituo hiki, muda ambao nimeutumia kuandaa shamba kuelekea msimu mpya wa kilimo ambao upo karibu sana,” amesema Zena.

Akizungumza kwa niaba ya wakulima, diwani wa Kata ya Kilagalo, Festus Nchimbi amesisitiza kuwa vifaa vya kisasa vya kusafisha mahindi vinapaswa kutolewa kwa wakulima, maghala ya kutosha yanapaswa kujengwa, wanunuzi wa mahindi yaliyochambuliwa wanapaswa kutafutwa, na changamoto ya mbegu bandia inapaswa kushughulikiwa.

Related Posts