LIGI ya Championship itaanza hivi karibuni na itashirikisha timu 16 zitakazosaka nafasi mbili za kupanda moja kwa moja Ligi Kuu na nyingine moja ya kupambania kupanda kwa mechi za mchujo.
Kuna mambo kama mawili hivi nahisi yanaweza kutokea katika Ligi ya Championship msimu kwa namna nilivyofuatilia maandalizi na mipango ya timu shiriki.
Jambo la kwanza ni uwezekano wa kupanda daraja kwa timu tatu za Champioship kwenda Ligi Kuu badala ya mbili kwa sababu kuna timu zimefanya usajili wa wachezaji wazuri kiuwezo kuzidi hata baadhi wanaocheza katika ligi kuu.
Ikitokea mojawapo kati ya timu zilizo na vikosi imara kwenye Championship ikapata nafasi ya kucheza mchujo na timu ya Ligi Kuu inaweza kutoboa kwa vile wachezaji hawatokuwa na uoga wa mechi na watajiona wanastahili kwenda kwenye daraja la juu la ligi.
Ukiondoa hilo, nahisi timu zitakazopanda daraja msimu ujao kutoka Championship kwenda Ligi Kuu zitatokea katika kundi la timu tano ambazo kutokana na maandalizi zinazoonekana zinayafanya kwa ajili ya ligi hiyo.
Timu tano za Championship ambazo nadhani kati ya hizo, mbili au tatu zitapanda Ligi Kuu ni Mtibwa Sugar (Morogoro), Geita Gold (Geita), Mbuni (Arusha), TMA (Arusha) na Songea United (Ruvuma).
Kati ya timu hizo tano, kuna tatu ambazo zinaweza kubebwa kwa ubora wa vikosi ambavyo zimesajili msimu huu ambavyo vinaonekana vinaweza kuwa mwiba kwa timu nyingine za ligi hiyo.
Kuna timu nyingine hapo zitabebwa zaidi na uzoefu ambazo zinao katika kupandisha timu pamoja na mipango ya kimyakimya ambayo zinaendelea kufanya.
Maneno yangu sio sheria na simlazimishi mtu kukubaliana kwa 100% na kile ambacho nimekisema lakini kiuhalisia timu nyingine zitapaswa kufanya kazi kubwa sana ili kutwaa ubingwa au kumaliza katika nafasi ya pili.