Beki Msenegali amchomoa Fei Toto

BEKI wa kushoto wa Azam FC, Cheikh Sidibe amesema hakuna mchezaji asiyetamani kucheza na kiungo wa timu hiyo, Feisal Salum ‘Fei Toto’, kutokana na aina ya uchezaji wake, huku akimpa miaka miwili kucheza Tanzania.

Akizungumza na Mwanaspoti, Sidibe ambaye ni raia wa Senegal alisema anafurahi kucheza timu moja na kiungo huyo na ubora wake umekuwa ukitoa chagamoto kwa mastaa wengi wa ndani na kigeni wanaocheza naye nafasi moja.

“Sio bora kwa Azam tu, pia ni msaada kwa timu yake ya taifa. Hivi karibuni amefunga bao bora kwenye mchezo wa kuwania kufuzu Afcon 2025, hiki anachokifanya kinatoa changamoto sio kwa wachezaji wazawa pekee hadi wa kigeni, kwa sababu amekuwa akiwaweka benchi kutokana na ubora alionao,” alisema Sidibe na kuongeza;

“Ni mchezaji mwenye uwezo wa kutengeneza mashambulizi, anakaba na ni mwepesi kupanda na kushuka amekuwa bora eneo hilo, siyo mwoga wa kufanya maamuzi na ndiyo maana mabao mengi anayofunga ni mazuri.”

Sidibe alisema pia kiungo huyo ni rafiki wa kila mtu, mcheshi na ana masihara mengi nje ya uwanja kitu ambacho kinamfanya awe pamoja na kila mtu.

“Anachokifanya sasa kwenye ligi kama atakiendeleza kwenye michuano ya kufuzu Afcon tutakuwa tunazungumzia mambo mengine hapo baadaye, sioni kama ataendelea kucheza soka la Afrika ni mchezaji mzuri na bora,” alisema beki huyo na kuongeza;

“Ubora wa Fei Toto alionao sasa na nidhamu yake ya mchezo anazidi kuwa mchezaji mkubwa na mimi namuona mbali sana, hakuna mchezaji ambaye hatamani kucheza na kiungo huyo ukiondoa wale wanaocheza nafasi moja ambao wanapata wakati mgumu kumuondoa kwenye nafasi aliyopo.”

Beki huyo ambaye alipata kadi nyekundu kwenye mchezo wao wa ligi dhidi ya Pamba Jiji, alimuomba Fei Toto kuendelea kupambania nafasi aliyonayo kwenye taifa lake na Azam FC ili akacheze soka la kulipwa nje ya Tanzania.

Related Posts