DC Mapunda: Watoto wafundishwe kupanda miti wangali wadogo

Dar es Salaam. Katika juhudi za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, Mkuu wa Wilaya ya Temeke, Sixtus Mapunda amewataka walimu na viongozi wa shule za sekondari na msingi wilayani humo kuendeleza upandaji miti.

Akizungumza leo Septemba 20, 2024 katika tukio maalum la upandaji miti katika shule zaidi ya 20 ndani ya Wilaya ya Temeke, Mapunda ameziomba Kampuni ya Bima ya Afya na Maisha ya Jubilee na Aga Khan Foundation (AKF) kumsaidia kwenye kampeni hiyo inayolenga kupanda miti isiyopungua 100. ikiwepo miti ya matunda, vivuli hata mapambo.

“Kwa shule za msingi kwa hawa watoto umuhimu wa mazingira unapaswa kuanza kwa kila mmoja kupewa mti wake aulee tangu darasa la kwanza mpaka darasa la saba, tumeona pale kumbe nafasi sio tatizo ambapo unaweza kuweka miti 200 kwenye mita 10,” amesema Mapunda.

Pia, amesema baada ya kuelekeza shuleni inabidi kuhamia kwenye familia kwa wanafunzi kutoa elimu kwa wazazi kwa kuwa ameona na kujifunza kutoka shuleni.

“Ndani ya miaka mitatu naamini Dar es Salaam itakuwa imebadilika katika kiwango cha juu, kwa sasa ukienda Masaki unaona kuna miti ukifika Mikocheni hali inabadilika unakuta imesakafiwa na ukikaa Mbagala halafu uende Chamazi ni kama unaishi dunia tofauti,” amesema Mapunda.

Mapunda ametoa wito kwa wananchi kupanda miti inayowasaidia huku akitolea mfano vyungu vya maua ambavyo vinaweza kutumika kupanda mboga mboga na kusaidia watoto ili kupunguza tatizo la vitamini C.

“Wanafunzi wamepanda miti mingi lakini haiwasidii zaidi ya kivuli, wanaweza kupanda chainizi na kabichi ili muda wa kula iwasaidie kupata mboga, wapande miti ya mpera, mipapai kupata matunda,” amesema.

Mkurugenzi Mtendaji Aga khan Foundation, Atteeya Sumar amesema jitihada hizo za upandaji miti ni sehemu ya mpango wa shirika la Aga Khan Development Network (AKDN) kupunguza uzalishaji wa hewa ya ukaa hadi kufikia sifuri ifikapo mwaka 2030, pamoja na kupanda miti milioni 50 duniani kote.

Amesema hadi sasa, Aga Khan Foundation Tanzania imepanda misitu midogo  125 katika maeneo ya Lindi, Dar es Salaam, na Zanzibar, ambapo  misitu hiyo imeanzishwa shuleni.

“Kwa kupitia mpango huu, misitu midogo inatarajiwa kutoa mchango mkubwa kwa mfumo wa ikolojia ya mijini, ikiwa ni sehemu ya mkakati wa kimataifa wa kulinda mazingira,” amesema Sumar.

Mkurugenzi Mkuu wa Bima ya Afya ya Jubilee Dk Haron Adamson amesema lengo lao ni kuhakikisha wanakuwa kinara kwenye kutunza na kuhifadhi mazingira kwa kufanya miradi midogo midogo ya upandaji miti.

“Katika kuhamasisha upandaji miti leo tumepanda miti 200 kwenye Shule ya Msingi Madenge ambayo ni mchanganyiko ikiwemo ya matunda, dawa na vivuli huku tukifahamu kuwa miti hii itaboresha hali ya mazingira pamoja na afya kwa watoto wetu wanaosoma hapa,” amesema Dk Haron.

Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Madenge Hadija Hussein amesema wanafunzi wanapenda kujifunza kwa kuona hivyo dhana hiyo itasaidia kwa uwepo wa misitu shuleni.

“Kuwepo kwa msitu ambao umeoteshwa hapa utasaidia si tu kwa kujifunza lakini pia kwa ajili ya matunda, dawa na kupata hewa safi,” amesema Hadija.

Related Posts