Dereva, kondakta na abiria mbaroni wakidaiwa kumpiga trafiki

Jeshi la Polisi mkoani Mara linawashikilia watu 18 wakiwamo abiria 16, dereva na kondakta kwa tuhuma za kumpiga askari wa usalama barabarani aliyekuwa akikagua gari walilokuwa wamepanda.

Tukio hilo limetokea juzi Jumatano Septemba 18, 2024, saa 12 jioni.

Ofisa Mnadhimu wa Jeshi la Polisi Trafiki Kuu, Butusyo Mwambelo amesema askari huyo alikumbwa na kipigo wakati akijaribu kushusha abiria waliokuwa wamesimama kwenye gari.

 Hata hivyo, kondakta wa gari hilo alifunga mlango na wote waliokuwa ndani ya gari, akiwamo dereva, kondakta na abiria, walianza kumshambulia askari huyo.

“Askari wetu alikuwa akitekeleza wajibu wake wa kuwataka abiria waliokuwa wamesimama kwenye gari washuke, lakini ghafla walimzonga kwa maneno ya kebehi, na kondakta akafunga mlango wa gari. Ndipo dereva, kondakta na abiria wao wakaanza kumpiga askari akiwa ndani ya gari. Je, kweli tumefika hatua hiyo kama Watanzania?” amesema Mwambelo.

Mwambelo ametoa maelezo hayo wakati wa operesheni ya ukaguzi wa magari iliyofanyika Septemba 19, 2024, katika Kituo Kikuu cha Mabasi cha Geita na kusisitiza kuwa tukio hilo ni la kusikitisha na halitavumiliwa. Amesema Jeshi la Polisi limechukua hatua za haraka kuhakikisha wote waliohusika katika tukio hilo wanawajibishwa kisheria.

Akizungumzia operesheni ya ukaguzi wa magari na utendaji kazi wa madereva na kondakta, Mwambelo amesema jeshi limeanza operesheni kutokana na kukithiri kwa ajali za barabarani zinazosababishwa na madereva kukiuka sheria.

Amesema magari yanayotoka mkoa mmoja kwenda mwingine yamefungwa mfumo wa vidhibiti mwendo vinavyopiga ‘alam’ pindi dereva anapozidisha mwendo na kuwataka abiria wanaposikia ‘alam’ kutoa taarifa ili kuzuia  ajali zisizo za lazima.

“Mnapoona dereva anakiuka sheria za usalama barabarani toeni taarifa msisubiri tukio litokee muanze kulaumu ajali nyingi zinazotokea zinasababishwa na binadamu dereva hawi makini na hajali watumiaji wengine wa barabara,”amesema.

Amesema wapo madereva wanaochezea mfumo na kuondoa ‘alam’ huku akionya kuwa, atakayebainika atafutiwa leseni kwa miezi mitatu na ikitokea amerudia atafutiwa leseni kabisa.

Mkuu wa Usalama Barabarani Mkoa wa Geita,  Aloyce Jacob amesema elimu inayotolewa itasadia kupunguza ajali za barabarani.

Mmoja wa abiria, Jeremia Elias amesema pamoja na elimu inayotolewa na polisi changamoto kubwa ipo kwa madereva ambao huongeza mwendo wanapovuka eneo lenye askari.

Related Posts