PAZIA la Ligi ya Championship msimu wa 2024/2025 linafunguliwa kesho huku wageni wa michuano hiyo, Geita Gold wakianzia nyumbani Nyankumbu dhidi ya TMA ya Arusha saa 8:00 mchana, huku Kocha Mkuu wa timu hiyo, Amani Josiah akitamba kuanza vizuri.
Geita Gold inashiriki michuano hiyo baada ya kushuka daraja kutoka Ligi Kuu Bara msimu uliopita, ina matumaini ya kufanya vizuri kama ilivyofanya mwaka 2021 ilipopanda Ligi Kuu ikiwa mabingwa wa Championship bila kupoteza mchezo wowote.
Josiah alisema ameridhishwa na kiwango cha timu yake kwenye maandalizi waliyofanya ikiwemo mechi za kirafiki ambazo hawakupoteza mchezo.
Katika mechi hizo za kirafiki, Geita Gold iliibamiza Geita Kombaini mabao 8-1, ikaifunga Pamba Jiji mabao 2-1 na kupata sare ya 1-1 na Kagera Sugar, matokeo na kiwango hicho cha kikosi chake kimempa mzuka kocha huyo ambaye anaamini wataanza vizuri.
“Tumeona makosa na mahali tulipofikia nimeona baadhi ya vitu chanya ambavyo tutaendelea navyo mbali na vitu vya kuendelea kufanyia kazi, kwa muda ambao nimekaa na vijana wangu nimeridhika na jinsi wanavyofanyia kazi maelekezo yangu na wameimarika kisaikolojia na kiufundi,” alisema Josiah.
Alisema licha ya kuwa na kikosi kizuri na wachezaji wengi wazoefu, lakini siku zote Ligi ya Championship imekuwa ngumu na isiyo tabirika, hivyo, hawezi kuichukulia poa timu yoyote ambayo watakutana nayo.