Kundi la Hezbollah limesema lilifanya mashambulizi yake kwa kutumia roketi aina ya Katyusha na kuelekezwa kwenye kambi kadhaa za jeshi la anga pamoja na makao makuu ya ulinzi wa kivita. Jeshi la Israel limesema makombora 120 yalifyatuliwa katika maeneo ya milima ya Golani, sehemu ya Galilaya na kuwa baadhi ya makombora hayo yalizuiwa.
Timu za zima moto zimeripotiwa kuwa zilikuwa kwenye harakati za kuzima moto uliotokana na mabaki ya silaha zilizowaka moto na kuanguka katika maeneo mbalimbali. Hata hivyo jeshi hilo halikufafanua kuhusu madhara yaliyotokana na mashambulizi hayo
Soma zaidi: Hizbullah, Israel washambuliana vikali
Katika hatua nyingine inayotafsiriwa kuwa ni ya kujibu mashambulizi, jeshi la Israel limefanya mashambulizi Beirut Ijumaa mchana. Kwa mujibu wa Wizara ya Afya ya Lebanon mashambulizi ya Israel Kusini mwa Beirut yamesababisha vifo vya watu wa 8. Watu wengine zaidi ya 50 wamejeruhiwa katika mashambulizi hayo.
Kamanda wa ngazi ya juu wa Hezbollah ameripotiwa kuuwawa
Moja ya vyanzo vilivyo karibu na kundi la Hezbollah awali vilieleza kuwa miongoni mwa waliouwawa ni kiongozi wa ngazi ya juu wa wanamgambo hao. Kimemtaja kiongozi huyo kuwa ni Ibrahim Aqil kamanda wa kikosi chake maalum cha Radwan. Chanzo hicho kiliomba kutotajwa jina kutokana na sababu za kiusalama.
Televisheni ya Al- Mayadeen ya mjini Beirut imearifu kwamba droni moja kutoka Israel ilirusha makombora kadhaa katika eneo lenye watu wengi la Dahiyeh. Kundi la Hezbollah limethibitisha kutokea kwa mashambulizi hayo ya anga.
Soma zaidi: Kiongozi wa Hezbollah akiri kupata “pigo” kufuatia kulipuka kwa vifaa vya mawasiliano
Zaina Harb ni mmoja wa wa raia wa Lebanon walioshuhudia mashambulizi ya Israel aliyenukuliwa akisema, “Tunaambiana na tunamatumaini kuwa vita hivi havitazidi kusambaa na raia hawataathiriwa. Tunajipa matumaini kuwa vita hivi vitaisha haraka iwezekanavyo. Lakini bado tunaendelea kuishi kwa hofu kuwa huenda hali ya mambo ikashindikana kudhibitiwa.”
Hayo yanaendelea wakati Israel kupitia msemaji wa Wizara ya Mambo ya Kigeni Oren Marmorstein ikisema Ijumaa kuwa imewasilisha pingamizi rasmi dhidi ya ombi la mwendesha mashtaka wa Mahakama ya Kimataifa ya Kivita ya Uhalifu ya ICC la kutaka waranti wa kukamatwa kwa Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu.