Jeshi la Polisi lazuia mikutano ya Chadema, ACT-Wazalendo

Dar es Salaam. Jeshi la Polisi limezuia mikutano ya hadhara iliyokuwa ihutubiwe na viongozi wa vyama vya siasa vya ACT-Wazalendo na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) iliyokuwa ifanyike Tanga na Dar es Salaam.

Wakati barua ya Jeshi la Polisi kwa Chadema ikieleza zuio hilo ni kutokana na tishio la usalama likihusisha maandamano yaliyopangwa kufanyika Septemba 23, 2024, barua kwa ACT- Wazalendo imewataka viongozi wa chama hicho kuonana na Mkuu wa Polisi Wilaya ya Magomeni.

Msemaji wa Jeshi la Polisi, David Misime alipotafutwa na Mwananchi leo Septemba 20, 2024 kuzungumzia barua hizo amesema, “barua inajieleza vizuri sana.”

Mkutano wa hadhara wa Chadema uliozuiwa ulikuwa ufanyike mkoani Tanga kesho Septemba 21, 2024 na kuhutubiwa na Makamu Mwenyekiti wa chama hicho (Bara), Tundu Lissu.

Kwa upande wa ACT-Wazalendo mkutano ulikuwa ufanyike leo Septemba 20, kwenye viwanja vya Sanifu Kigogo, Dar es Salaam.

Barua iliyoandikwa na Mkuu wa Polisi Wilaya (OCD) ya Tanga Mrakibu wa Polisi D. I. Mwambigiri kwenda kwa Chadema Mkoa wa Tanga jana Septemba 19, 2024, Jeshi hilo linasema mkutano  umezuiwa kwa sababu za kiusalama.

“Ikumbukwe kwamba, viongozi wa Chadema Taifa wametangaza nia ovu ya kufanya maandamano siku ya tarehe 23, Septemba 2024 Jiji la Dar es Salaam. Kutokana na taarifa tulizokuwa nazo ni kwamba mkutano wa hadhara unaotakiwa kufanyika kesho ni maandalizi ya kufanya maandamano baada ya kumaliza mkutano huo,” inasema barua hiyo.

OCD Mwambigiri ametumia kifungu cha 44 cha Sheria ya Jeshi la Polisi na Polisi Wasaidizi Sura ya 322 kuzuia mkutano huo, akisema una dalili za kuleta uvunjifu wa amani ndani ya wilaya na kuhatarisha usalama wa raia na mali zao.

“Kukiukwa kwa maelekezo haya ni kosa la jinai kwa mujibu wa k/f45 cha Sheria ya Jeshi la Polisi na Polisi Wasaidizi; na mtashughulikiwa kwa mujibu wa kanuni ya adhabu sura 16RE 2022,” amesema.

Chadema imepanga kufanya maandamano jijini Dar es Salaam Septemba 23 yanayolenga kuitaka Serikali kutoa maelezo kuhusu matukio ya utekaji na mauaji yakiwamo ya makada wake, akiwamo Ali Kibao.

Kibao alikutwa ameuawa Septemba 7, 2024 eneo la Ununio baada ya kuchukuliwa na watu wasiojulikana eneo la Tegeta Dar es Salaam alipokuwa akisafiri kwa basi la Tashriff kwenda mkoani Tanga Septemba 6. Alizikwa Septemba 9, mkoani humo.

Jeshi la Polisi limepiga marufuku maandamano hayo likisema linatekeleza maagizo ya Rais Samia Suluhu Hassan ya kufanya uchunguzi kuhusu matukio hayo.

Kwa mujibu wa ofisa habari wa Chadema, Apolinary Boniface baada ya mkutano wa hadhara wa Tanga walipangwa kwenda kuhani msiba wa Kibao.

Katika hatua nyingine, Mkuu wa Polisi Wilaya (OCD) ya Magomeni, Dar es Salaam, Mrakibu wa Polisi, E.K Masunga ameagiza kusitishwa mara moja mkutano wa ACT-Wazalendo uliopangwa kufanyika leo Septemba 20, 2024 kwenye viwanja vya Sanifu, Kigogo.

Katika barua aliyokiandikia chama hicho, OCD Masunga amemtaka Katibu wa ACT-Wazalendo Jimbo la Kinondoni kufika ofisini kwake leo.

Akizungumzia zuio hilo, Makamu Mwenyekiti wa ACT- Wazalendo (Bara), Isihaka Mchinjita amesema viongozi wa jimbo walifika kwa OCD leo asubuhi.

“Walichoambiwa ni kwamba wamezuia mikutano kwa sababu ya hofu ya kufanyika maandamano,” amesema.

Mchinjita amesema, “jana (Septemba 19) mkutano wetu wa Kibamba ulizuiwa kwa maneno lakini tulifanya, kwa hiyo leo viongozi wetu walitakiwa kwenda polisi. 

“Nilikwenda Kituo cha Polisi Mburahati kukutana na Mkuu wa Polisi Wilaya ameniambia wanazuia mikutano kutokana na hofu ya maandamano yatakayofanyika Septemba 23.”

Kama una maoni kuhusu habari hii, tuandikie ujumbe kupitia WhatsApp: 0765864917

Related Posts