KAMISHNA wa Ubia kati ya Sekta ya Umma na Binafsi (PPP), David Kafulila, amevitaka vyuo vya umma nchini kutumia sekta binafsi kujenga mabweni na miradi mbalimbali kwa ubia na sekta binafsi bila kutegemea fedha za Serikali. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).
Amesema miradi ya ubia inainufaisha zaidi serikali kwani inapata teknolojia mpya na za kisasa kutoka sekta binafsi na kusaidia uchumi wake kuendeshwa kisasa zaidi na kwa ufanisi.
Aliyasema hayo jana jijini Dar es Salaam wakati akizungumza kwenye mkutano wa wadau wa chuo hicho kilichojadili utekelezaji wa mradi wa ubia wa ujenzi wa mabweni yatakayokuwa na uwezo wa kuchukua wanafunzi 12,000.
“CBE imeonyesha njia, imetengeneza template ambayo vyuo vingine vinapaswa kuiga kwa kujenga mabweni kwa ubia bila kuomba Hazina fedha za uendeshaji,” alisema Kafulila.
Alisema mamlaka zote za serikali zinazotekeleza miradi mbalimbali ziangalie uwezekano wa kuhusisha sekta binafsi kwenye utekelezaji wa miradi hiyo badala ya kusubiri fedha za serikali.
Alisema kila mradi ambao sekta binafsi inaweza kuutekeleza ni vyema taasisi za serikali zikaingia ubia nazo ili kuharakisha utekelezaji wake na kuokoa fedha za serikali ambazo zingetumika.
“Kila mradi ambao sekta binafsi inaweza kuutekeleza kwa teknolojia ya hali ya juu kuliko serikali basi apewe autekeleze ili tujenge uchumi wa kisasa ambao sekta binafsi ndiyo inanafasi kubwa ya kutengeneza ajira nyingi,” alisema
Aliipongeza menejimenti ya CBE kwa kuratibu mradi wa ujenzi wa mabweni hayo ambayo yatakapokamilika yataondoa uhaba wa makazi ya wanafunzi kwenye kampasi ya chuo hicho hapa jijini Dar es Salaam.
Kafulila alisema serikali iliamua kuweka utaratibu wa kuweka miradi kwa ubia ili kunufaika na mambo manne ikiwemo kutekeleza miradi yake bila kutumia fedha zake au mikopo kutoka mataifa ya nje.
“Utaratibu wa ubia unaleta unafuu kwa serikali kwasababu miradi inajengwa bila kutegemea fedha zake lakini utaratibu huu wa ubia unafanya serikali ivute teknolojia ya kujenga baadhi ya miradi, teknolojia ambayo kwa kiasi kikubwa inapatikana sekta binafsi,” alisema
Alisema kwa utaratibu wa ubia serikali inanufaika na teknolojia ya kisasa ambayo inapatikana kwenye sekta binafsi na kupata fursa ya kuleta weledi kwenye taasisi zake kama CBE.
“Kwa mfano mabweni haya yatakapojengwa na kukamilika mwekezaji atalipa kodi kwa serikali lakini kama ingejenga yenyewe ingekuwa huduma tu na hakuna kodi ambayo serikali ingepata kwa hiyo utaratibu huu unainufaisha sana serikali,” alisema.
Mkuu wa chuo hicho, Profesa Edda Lwoga, alisema mabweni hayo yatakayojengwa kwenye kampasi kuu ya Dar es Salaam yatakuwa na uwezo wa kuchukua wanafunzi 2,728 hivyo kupunguza pengo kubwa la malazi kwa wanafunzi.
Alisema kwa sasa kampasi ya CBE Dar es Salaam ina jumla ya wanafunzi 12,000, ambapo kwa upande wa malazi kampasi ina majengo mawili tu ya bweni yenye uwezo wa kuchukua vitanda 160 pekee vya malazi kwa wanafunzi wa kike na kiume hivyo vinakidhi uhitaji wa malazi kwa asilimia 1.3 tu.
Mkuu wa chuo alisema mradi huo utakapokamilika unatarajiwa kupunguza changamoto ya malazi kutoka asilimia 1.34 iliyopo mpaka asilimia 30 ya mahitaji ya wanafunzi kwa bweni.
“Hali iyopo imesababisha uhitaji mkubwa wa malazi ya wanafunzi kwa asilimia 98.6 hivyo wengi wanalazimika kutafuta malazi nje ya chuo kwa gharama kubwa, jambo linalosababisha baadhi ya wanafunzi kushindwa kumudu gharama hizo,” alisema.