MSHIKE mshike wa Ligi Kuu Bara unaendelea tena leo na michezo miwili itapigwa, huku macho na masikio yakielekezwa Uwanja wa Kaitaba Bukoba kwa mechi kali kati ya wenyeji Kagera Sugar dhidi ya KenGold.
Mchezo huo utapigwa saa 1:00 usiku ingawa utatanguliwa na mechi ya mapema saa 10:00 jioni kwenye Uwanja wa Ali Hassan Mwingi mkoani Tabora na wenyeji Tabora United itapambana na Fountain Gate.
Ubora wa mchezo kati ya Kagera na KenGold, unatokana na timu zote kutoshinda michezo yao waliyocheza hadi sasa msimu huu huku kama haitoshi wenyeji licha tu ya kutopata pointi tatu kwenye mechi zao nne ilizocheza ila haijafunga bao lolote.
Kagera inayofundishwa na Mganda, Paul Nkata huenda huu ukawa mchezo wake wa mwisho na timu hiyo ikiwa atashindwa kupata pointi tatu baada ya kuambulia vipigo vitatu na kutoka sare mmoja, jambo linaloonyesha hana maisha marefu kikosini humo.
Timu hiyo ilianza Ligi Kuu Bara kwa kichapo cha bao 1-0, kutoka kwa Singida Black Stars, ikachapwa tena 2-0 na Yanga, 1-0 na Tabora United kisha kulazimishwa suluhu na JKT Tanzania mechi iliyopita.
Kwa upande wa KenGold kutoka jijini Mbeya ambayo ni msimu wake wa kwanza Ligi Kuu Bara baada ya kutwaa ubingwa wa Championship msimu uliopita, haijaonja pia ladha ya ushindi katika michezo yake mitatu iliyocheza, ikichapwa yote.
KenGold ilianza Ligi Kuu Bara kwa kichapo cha mabao mabao 3-1 kutoka kwa Singida Black Stars Agosti 18, 2024, ikachapwa 2-1 na Fountain Gate Septemba 11, 2024, kisha kupoteza kwa bao 1-0, na KMC, mechi yake ya mwisho Septemba 16, 2024.
Licha ya KenGold kutopata ushindi hadi sasa ila inamtegemea nyota mshambuliaji, Joshua Ibrahim ambaye amekuwa na kiwango bora msimu huu, akifunga mabao mawili akiwa na kikosi hicho ambacho amejiunga nacho akitokea Tusker FC ya Kenya.
Kwa upande wa Tabora United na Fountain Gate, timu zote zinakutana zikiwa na pointi saba zikiwa nafasi ya nne na ya tatu baada ya kucheza michezo minne kila mmoja wao, huku hadi sasa zikitofautiana kwa mabao yao ya kufunga na kufungwa tu.
Katika michezo hiyo minne Tabora United inayonolewa na Mkenya, Francis Kimanzi imeshinda miwili, sare mmoja na kupoteza pia mmoja kama ilivyokuwa pia kwa Fountain Gate inayofundishwa na mzawa, Mohamed Muya jambo linaloongeza msisimko zaidi.
Fountain Gate inaingia katika mchezo huu ikimtegemea nyota wa kikosi hicho Seleman Mwalimu ambaye kwenye michezo minne aliyocheza amefunga mabao matatu huku kwa upande wa Tabora United ikiongozwa na Mkongomani, Heritier Makambo mwenye bao moja.
Wakizungumzia maandalizi ya michezo hiyo, kaimu Kocha Mkuu wa KenGold, Jumanne Challe alisema, presha ni kubwa kwao ila anaamini watafanya vizuri huku Kocha wa Kagera Sugar, Paul Nsata akieleza changamoto kubwa kwao ni kwenye umaliziaji tu.