Dar es Salaam. Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (Latra) imerejesha huduma ya usafirishaji kwa mabasi sita kati ya 10 ya kampuni ya Katarama yaliyokuwa yamesitishiwa safari kwa muda usiojulikana.
Septemba 13, 2024, Latra ilisitisha leseni ya safari ya mabasi 10 ya kampuni kwa madai ya kuchezea mifumo ya mwenendo wa mabasi (VTB) iliyowekwa kwenye mabasi hayo.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Septemba 20, 2024 Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano na Mawasiliano Latra, Salum Pazzy amesema usitishwaji wa safari ulifanywa kwa mujibu wa kanuni za leseni za usafirishaji ya 27(d) na 27(2) kwa magari ya abiria.
“Hatua hiyo ilifuatia uchunguzi wa awali uliofanyika na kubaini kosa la kuingilia mfumo wa kufuatilia mwenendo wa mabasi kwa njia ya kubadili sehemu ya kifaa na kuweka kingine kinachosababisha utumaji wa taarifa potofu katika mfumo wa VTS,” amesema Pazzy.
Amesema uchunguzi huo wa awali kosa hilo lilibainika katika mabasi mawili namba T420EBR na T836EBR na mara baada ya kusitisha huduma Latra ilifanya uchunguzi kwa mabasi yote 10 na kubaini mabasi mengine mawili namba T835EBR na T485DXP yakiwa yamefanyiwa aina hiyo hiyo ya kubadili mfumo.
Hivyo amesema mamlaka imerejesha huduma kwa mabasi sita ambayo yanafanya safari kutoka Dar es Salaam kulekea katika mikoa ya Mwanza na Bukoba T212ECR (Mwanza), T587EHC (Mwanza), T315EHW (Mwanza), T314 EHW (Mwanza), T446EHW (Bukoba) na T431EHW (Bukoba).
Pazzy amewataka wasafirishaji wa abiria kufuatilia magari yao yanayotoa huduma na yaliyopewa leseni kwa mujibu wa sheria, ili wajiepushe na uvunjifu wa sheria, taratibu na kanuni, kwani mamlaka hiyo haitasita kuchukua hatua.
Kwa wasafirishaji wa usiku amesema watumie dhamana hiyo vizuri kwani abiria wengi wamepokea vizuri usafiri wa muda huo na Latra haitasita kuwachukulia hatua wanaovunja sheria.
Kuhusu wasafirishaji waliopewa onyo kali ambao ni Abood, BM Super Feo, Pazi amesema wanawafuatilia kwa karibu na watakaobainika bado wana changamoto, watachukuliwa hatua pamoja na kuwanyang’anya ratiba ya kutoa huduma usiku.
Meneja wa operesheni wa kampuni ya Katarama, Elimboto Njoka amesema wamepitia kipindi kigumu cha kusitishiwa huduma, lakini wameshukuru kupewa nafasi ya kuzungumza na kupewa maelekezo.
“Tutazingatia yale ambayo ni upungufu katika masharti yetu ya leseni zetu hayo tutaenda kuyafanyia kazi na tunaamni tutakuwa watu bora katika huduma ya usafirishaji,” amesema Njoka.