Ligi ya Championship utamu umerudi upyaa

MSIMU mpya wa 2024-2025 wa Ligi ya Championship umerejea tena upya huku makocha wa timu zote 16 zinazoshiriki wakikiri utakuwa na mvuto wa aina yake kutokana na usajili mkubwa uliofanyika wa wachezaji bora na wenye uzoefu wa Ligi Kuu Bara.

Leo michezo miwili ya ufunguzi itapigwa kati ya Mbeya City iliyoikaribisha Bigman FC iliyokuwa inajulikana kwa jina la Mwadui, huku Mtibwa Sugar ikicheza na Green Warriors, Ligi hiyo inaendelea tena kesho kwa michezo mitatu kupigwa.

Mchezo wa mapema saa 8:00 mchana, utapigwa kwenye Uwanja wa Nyankumbu Geita ambapo wenyeji, Geita Gold iliyoshuka daraja msimu uliopita itacheza na TMA ya Arusha, ambayo msimu uliopita ilimaliza Championship nafasi ya tano na pointi zake 54.

Saa 10:00 jioni itachezwa michezo miwili ambapo Cosmopolitan iliyomaliza nafasi ya tisa kwa msimu uliopita na pointi 39, itacheza na wageni waliopanda daraja msimu huu, African Sports ya mjini Tanga kwenye Uwanja wa Mabatini mkoani Pwani.

Songea United iliyofahamika kwa jina la FGA Talents ambayo msimu uliopita ilimaliza nafasi ya 10 na pointi 34, itacheza na Mbeya Kwanza iliyomaliza nafasi ya tatu msimu uliopita na pointi zake 65, kwenye Uwanja wa Majimaji mkoani Ruvuma.

Kesho kwa michezo mitatu kupigwa ambapo saa 8:00 mchana Polisi Tanzania ambayo ilimaliza nafasi ya nane na pointi 39 msimu uliopita, itaikaribisha Mbuni kutoka Arusha kwenye Uwanja wa Ushirika Moshi.

Biashara United iliyocheza michezo ya mtoano ‘Play-Off’ ili kupata tiketi ya kucheza Ligi Kuu Bara msimu huu na kukwama mbele ya Tabora United kwa kuondolewa kwa jumla ya mabao 2-1, itacheza na Transit Camp kwenye Uwanja wa Karume Musoma.

Wageni wengine wa Ligi hiyo Kiluvya United iliyopanda daraja msimu huu, itakuwa wenyeji wa Stand United kutoka mkoani Shinyanga kwenye Uwanja wa Mabatini Pwani, ambayo msimu uliopita ilimaliza nafasi ya 11, baada ya kukusanya pointi 32.

Nyota wa zamani wa Yanga, Azam na Simba, Ivo Mapunda ambaye kwa sasa ni Kocha Mkuu wa Songea United alisema; “Mbali tu na wachezaji bora na wazoefu ila klabu nyingi zimepata michezo mingi ya kirafiki, jambo linaloonyesha wazi haitokuwa Ligi rahisi kabisa.” Klabu zinazoshiriki michuano ya Ligi ya Championship msimu huu ambazo zimewahi kucheza Ligi Kuu Bara ni African Sports, Biashara United, Geita Gold, Mbeya City, Mbeya Kwanza, Mtibwa Sugar, Polisi TZania, Stand United, na Transit Camp.

Related Posts