UWEPO wa makipa watatu wenye uzoefu kwenye kikosi cha Namungo ambao ni Beno Kakolanya, Erick Molongi na Jonathan Nahimana umelifanya benchi la ufundi la timu hiyo kugawanya muda wa kucheza kwa makipa hao.
Katika mchezo wa ligi dhidi ya Coastal Union alishuhudiwa kwa mara ya pili msimu huu kipa wa kimataifa kutoka DR Congo, Molongi akipewa nafasi na Mwinyi Zahera kuanza katika kikosi cha kwanza.
Huku Kakolanya akitupwa nje ya orodha ya hata ya wachezaji wa akiba, jambo ambalo lilionekana kuzua minong’ono ambayo kocha, Mwinyi Zahera anaijibu kwa kusema huo ni utaratibu ambao wameuweka kutokana na ubora wa makipa wote watatu ambao wamekuwa nao kwenye kikosi chao.
“Hakuna tatizo lolote kwa Beno, tumekuwa tukitoa nafasi kwa kila mchezaji na ukiangalia makipa wote ni wazuri bado kuna michezo mingi mbele na kila mchezaji ambaye atakuwa akionyesha kiwango atapata nafasi.
“Tumeona tutoe mechi mbili kwa kila mmoja, Beno alishacheza za kwake na sasa ni muda wa wengine,” amesema kocha huyo wa zamani wa Yanga.
Beno katika mechi zake mbili ambazo alicheza dhidi ya Fountain Gate na Dodoma Jiji aliruhusu mabao matatu, Molongi ameruhusu mabao mawili na yalikuwa katika mchezo wa kwanza wa ligi dhidi ya Tabora United na ndiye kipa pekee mwenye ‘clean sheet’.