Mlandizi Queens imesema itapambana msimu huu kuhakikisha inatengeneza timu kisha msimu ujao kuchukua ubingwa.
Ikumbukwe Mlandizi ndio mabingwa wa kwanza wa Ligi Kuu ya Wanawake (WPL) msimu wa 2016/2017 na tangu hapo Simba Queens na JKT Queens zimekuwa zikitawala ligi hiyo.
Kocha wa timu hiyo, Jamila Kassim aliliambia Mwanaspoti, malengo yao kwanza ni kutengeneza kikosi ambacho kitakuja kuwa na ushindani na msimu unaofuata ndiyo watafikiria ubingwa.
Jamila aliongeza, wamekaa nje bila kucheza Ligi Kuu kwa muda mrefu akiamini wamejifunza kitu na sasa wanarudi kwa kishindo.
“Kama mnavyojua sisi ndio tumeweka rekodi ya kwanza ya kuchukua ubingwa, kwangu pia natamani kama kocha niiweke rekodi hiyo, ingawa msimu huu tunataka kutengeneza kikosi cha akina Mwanahamis Omary ‘Gaucho’ wengine wengi,” alisema Jamila na kuongeza;
“Pre Season yetu tayari tumecheza mechi ya kirafiki kubwa na Yanga Princess tukafungwa lakini ilikuwa kipimo kizuri kwetu kujua tunaanzaje Ligi pia tumepanga kucheza mechi mbili na Simba na JKT kujipima zaidi.”
Mlandizi ni moja ya timu mbili zilizopanda daraja msimu huu kutoka Ligi Daraja la Kwanza (FDWL) sambamba na Gets Dodoma zitakazoungana na timu nyingine nane zilizosalia msimu uliopita.