Mo afanya umafia Dar, amshusha Mpanzu usiku

WAKATI Simba inaendelea kujipanga kuwang’oa Waarabu wa Libya Al Ahli Tripoli, mabosi wa klabu hiyo wana akili nyingine kubwa na bilionea Mohammed Dewji ‘MO’ amewafanyia umafia wa maana watani wao Yanga kwa kumchukua winga mmoja hatari.

Mwanaspoti imepenyezewa taarifa winga Mkongomani, Ellie Mpanzu yupo hapa nchini atika hoteli moja kubwa iliyopo katikati ya Jiji, akija kumalizana na mabosi wa Simba ili dirisha dogo likifunguliwa alimshe Msimbazi.

Inaelezwa Mpanzu alitua usiku wa kuamkia jana tayari kumalizana na Simba kisha kusubiri dirisha dogo lifunguliwe aanze kufanya yake Msimbazi.

Ujio wa Mpanzu na kutua Msimbazi, ni kama Simba imeipiga bao Yanga iliyojaribu kuingilia usajili wa winga huyo wa kushoto.

Inaelezwa MO akimfanyia balaa la fedha kwa Mpanzu kisha kumshusha juzi usiku kimyakimya.

Mpanzu amewasili usiku kwa Ndege ya Shirika la Uholanzi, akitokea Ubelgiji alikokwenda kufanya majaribio na KRC Genk.

Kabla ya Mpanzu kutimkia huko, Simba ilikuwa na hesabu za kumsajili lakini pande hizo mbili zikashindwa kukubaliana na baada ya majaribio hayo kufeli wekundu hao wakarudi tena kwake kimyakimya

Simba ilikuwa inataka kumpa Mpanzu kiasi cha Dola 130,000, lakini Yanga wakaingilia kati wakitaka kumpa Mkongomani huyo Dola 150,000.

Simba inayongozwa na MO iliposikia, ikapanda dau hilo ikampa ofa mpya Mpanzu ya Dola 200,000 winga huyo na uongozi wake ukakubaliana na ofa hiyo ndipo alipoamua kutua Dar usiku mnene kumalizia dili.

Simba akili nyingine iliyoitumia haikutaka Mpanzu (22) aendelee kubaki Ulaya kuhofia Yanga itarudi na nguvu nyingine ikamtumia tiketi haraka na winga huyo fundi wa kutumia mguu wa kushoto akatua juzi.

Mkongomani huyo ambaye aliitumikia AS Vita msimu uliopita, alipokelewa na wasaidizi wawili wa Salim Mhene ‘Try Again’ pale Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere 3 na Jana alitarajiwa kumaliza na Simba kusaini mkataba wa miaka miwili.

Try Again ndiye aliyekuwa anazungumza kuanzia awali na Mpanzu mpaka alipohakikisha anatua nchini huku MO akipitisha bajeti nzima ya kumchukua winga huyo anayejua kufunga kwa mipira ya adhabu.

Related Posts