Nyuki akumbatiwa, Tabora United Ikipigwa nyumbani 

TABORA United wamekuwa na msemo maarufu kwamba ‘nyuki hakumbatiwi’ kutokana na ukali wa mdudu huyo, lakini leo nyuki amekumbatiwa baada ya timu hiyo kukung’utwa mabao 3-1 na Fountain Gate katika mchezo wa Ligi kuu Bara uliochezwa  kwenye Uwanja wa Alhasan Mwinyi mjini Tabora.

Awali, mshambuliaji wa Tabora United, Heritier Makambo alikosa mkwaju wa penati baada ya yeye mwenyewe kuchezewa faulo ndani ya eneo la hatari dakika ya 42, ambapo mbali na nafasi hiyo pia alikosa nafasi tatu  akishindwa kuzitumia katika mchezo huo.

Tabora United imekubali kichapo cha kwanza nyumbani – Fountain Gates  wakipata mabao kupitia kwa Salum Kihimbwa ambaye alifunga  kwa penati dakika ya 27 baada ya kuchezewa madhambi kwenye eneo hatari, huku la pili likifungwa na Edgar William dakika ya 37 la tatu akifunga 90 ilihali lile la kufutia machozi kwa Tabora United likifungwa na Yacouba Sogne kwa shuti kali  lililomshinda Fikirini  Bakari wa Fountain Gate dakika ya 78.

Tangu kuanza kwa Ligi Kuu Bara msimu huu Tabora United imecheza michezo mitano ambapo imefanikiwa kukusanya alama saba ikishinda miwili, sare moja na kupoteza michezo miwili huku Fountain Gate katika michezo mitano imekusanya alama 10.

Akizungumza na Mwanaspoti, Kocha wa Fountain Gate, Mohamed Muyo amesema wachezaji wake wamefuata maelekezo ndiyo maana wamepata matokeo mazuri katika mchezo huo.

“Nawapongeza wachezaji wangu kwa kujituma kupata matokeo kwenye mchezo wetu  na Tabora, haikuwa rahisi lakini tuliwahimiza na tumepata matokeo ugenini jambo ambalo.halikuwa rahisi kulingana na ubora ambao wapinzai wetu walikuwa nao hasa kwenye uwanja wao wa nyumbani.

“Malengo yetu ni kufanya vizuri kwenye ligi hadi mwisho. Ukiangalia timu yangu kwa sasa natumia wachezaji wazawa pekee, lakini uwezo wao umekuwa ukipanda siku hadi siku, hivyo tutaendelea kufanya vyema mpaka mwisho wa msimu wa ligi. Kikubwa mashabiki zwaendelee kutuunga mkono ili tupate tunachotaka kila mchezo,” amesema

Kocha wa Tabora United, Francis Manzi amewapongeza  wachezaji wake licha ya kichapo.

“Nawapongeza wachezaji kwa kumaliza mchezo salama. Malengo yalikuwa kupata alama tatu, lakini wapinzani wetu wakawa imara ila wachezaji walijituma,” amesema.

“Mchezo haukuwa upande wetu, lakini niwaombe mashabiki wetu wasikate tamaa kwani michezo bado ipo na tutapambana kuhakikisha tunashinda na kurejea kwenye hali yetu.

“Washambuliaji wetu walipata nafasi kadhaa lakini hawakuzitumia ipasavyo jambo ambalo.limetufanya tupate bao moja kwenye huu mchezo, makosa tumeyaona na tutayafanyia kazi kuhakikisha tunareja tukiwa imara zaidi kwenye michezo inayofuata.” 

Baada ya mchezo kukamilika, mshambuliaji wa Fountain Gate,  Kihimbwa amepewa tuzo ya mchezaji bora wa mchezo huo.

Related Posts