Rachid Taoussi afichua dili la Simba

KOCHA Mkuu wa Azam FC, Rachid Taoussi jiioni ya jana alikuwa uwanjani kuiongoza timu hiyo dhidi ya KMC katika mechi ya Ligi Kuu Bara, lakini mapema amefichua siri, kabla ya kutua klabuni hapo, alishafuatwa na Simba ili atue lakini dili likafa na Wekundu kumchukua Abdelhak Benchikha.

Kocha huyo, pia alisema tangu akiwa kwao, alikuwa anazijua Simba, Yanga na Azam, hivyo ujio wake nchini haumpi shida kwani alishayasoma mazingira mapema.

Ipo hivi. Taoussi alisema akiwa na Raja Casablanca alipokea ofa kutoka Simba wakimhitaji kwa ajili kuinoa timu hiyo lakini alishindwa kufanya hivyo kutokana na kuwa na mkataba na timu hiyo ambayo ilikuwa inashiriki Ligi ya Mabingwa Afrika.

“Nilipokea simu kutoka kwa wakala wangu akinipa taarifa kuhusu Simba, haikuwa rahisi kuondoka Raja Casablanca ambayo ilikuwa inashiriki Ligi ya Mabingwa Afrika pia nilikuwa na mkataba na timu hiyo,” alisema Taoussi.

Alisema Simba baada ya kubaini ana mkataba walirudi nyuma, hawakuonyesha uhitaji naye zaidi na aliendelea kuheshimu mkataba wake hadi alipomaliza na kupokea ofa ya Azam.

“Nimekuja Azam kwa sababu wameleta ofa nikiwa sina timu, hivyo imekuwa rahisi mimi kujiunga na timu hii ambayo itaniongezea uzoefu wa soka la Afrika, pia ni timu ambayo imekamilika kwenye miundombinu yao kuanzia uwekezaji hadi viongozi wao wapo vizuri,” alisema Touassi na kuongeza;

“Pia kabla ya kujiunga na Azam nilipewa sifa za timu ninayokuja, imefanya uwekezaji mzuri kwa ajili ya timu, ndicho nilichokikuta nafurahi kuwa na wachezaji wazuri, mazingira mazuri kuanzia uwanja wa mazoezi, bwawa la kuogelea na Gym vitu ambavyo ni sahihi kwa wachezaji.”

Related Posts